TANGAZO


Tuesday, February 25, 2014

Serikali kubadili mfumo wa uzalishaji ili kuleta tija katika sekta ya Kilimo

Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Mhandisi Christopher Chiza akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kuhusu mikakati mbalimbali ya wizara yake katika kuendeleza sekta ya kilimo nchini. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Raphael Daluti na kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Assah Mwambene. (Picha na Fatma Salum)

Na Georgina Misama- MAELEZO.
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imelenga kubadili mfumo wa uzalishaji ili kuleta tija katika sekta ya Kilimo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Mhandisi Christopher Chiza, wakati wa mkutano na waandishi wa habari jana Jijini Dar Es Salaam.

Waziri Chiza alisema kuwa katika mfumo huo maeneo makuu matatu ya kipaumbele, ambayo ni kuwepo kwa mashamba makubwa ya uwekezaji yapatayo 25 kwa ajili ya kilimo cha mpunga na Miwa, kuwa na skimu za umwagiliaji 78 kwa ajili ya kilimo cha mpunga na maghala 275 ya mahindi kwa kutumia mfumo wa pamoja.

“Ili kuendana na kasi ya mfumo wa matokeo makubwa sasa, Serikali imeajapanga kuondokana na kilimo cha mazoea na kujikita kwenye kilio cha kisasa hasa kwenye mazao ya kipaumbele ambayo ni mpunga, miwa na mahindi” alisema Waziri Chiza.

Waziri Chiza alifanunua kuwa Serikali imejikita kwenye uzalishaji wa mazao hayo ili kukabiliana na changamoto zilizo kwenye sekta hiyo ikiwemo  mfumuko wa bei.

Ili kukabiliana na upungufu wa chakula katika baadhi ya maeneo nchini Waziri Chiza alisema kuwa Serikali imeidhinisha tani 23,312 za chakula cha msaada ili kisambazwe kwa waathirika 828,063 ambao walionekana kuwa na upungufu wa chakula katika wilaya 54 za mikoa 16.

Hifadhi ya Taifa ya Chakula hivi sasa ina tani 226,769.544 ambapo tani 226,270.862 ni za mahindi na tani 498.682 ni za mtama, ambapo kiasi hicho kinajumuisha tani 25,452.644 za mahindi kutoka msimu uliopita

No comments:

Post a Comment