TANGAZO


Tuesday, February 25, 2014

Vijana kuandaliwa kuwa chachu ya maendeleo ya Jamii



 

Mkuu wa Kampuni ya TATA Africa Holdings (Tanzania) Ltd Bw. Prashant Shukla akielezea jinsi watakavyoweza kushirikiana na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuwawezesha vijana kuleta maendeleo katika jamii, kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Pro. Elisante Ole Gabriel na katikati ni Mkuu wa kitengo cha kozi fupi na ushauri chuo cha Mzumbe Pro. Shiv K. Tripathi. (Picha zote na Genofeva Matemu - MAELEZO)




Mkuu wa kitengo cha kozi fupi na ushauri chuo cha Mzumbe Pro. Shiv K. Tripathi akichangia wakati wa majadiliano ya awali jinsi ya kuendeleza vijana kwa maendeleo ya jamii, kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Pro. Elisante Ole Gabriel na kushoto ni Mkuu wa Kampuni ya TATA Africa Holdings (Tanzania) Ltd Bw. Prashant Shukla.



Mkurugenzi Maendeleo ya Vijana Bw. James Kajugusi akielezea kuhusu moja ya kituo cha vijana kinacho jishughulisha na ufundi makanika kilichopo Ilonga Morogoro, kulia ni Mkuu wa Kampuni ya TATA Africa Holdings (Tanzania) Ltd Bw. Prashant Shukla wakati wa majadiliano ya awali ya kuendeleza vijana kwa maendeleo ya jamii.



Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo        Pro. Elisante Ole Gabriel akifafanua jambo wakati alipokutana na Mkuu wa Kampuni ya TATA Africa Holdings (Tanzania) Ltd kujadili jinsi watakavyoweza kushirikiana kuanzisha program ya kuwaendeleza vijana kwa maendeleo ya jamii. Kushoto ni Bw. Prashant Shukla Mkuu ya kampuni hiyo na katikati ni Mkuu wa kitengo cha kozi fupi na ushauri chuo cha Mzumbe Pro. Shiv K. Tripathi ofisini kwake leo jijini Dar es Salaam.



Na Genofeva Matemu (MAELEZO)
Jumanne 25/02/2014.

Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa kushirikiana na kampuni ya TATA Africa Holdings (Tanzania) Ltd imeadhimia kuanzisha programu ya kuendeleza maendeleo ya jamii kwa kutumia vijana waliopo katika ajira mbalimbali kwa kuwajengea uwezo utakaowawezesha kuleta maendeleo katika jamii yao.

Hayo yameafikiwa wakati Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Pro. Elisante Ole Gabriel alipokutana kwa ajili ya majadiliano ya awali na Mkuu wa Kampuni ya TATA Africa Holdings (Tanzania) Ltd Bw. Prashant Shukla pamoja na Mkuu wa kitengo cha kozi fupi na ushauri chuo cha Mzumbe Pro. Shiv K. Tripathi ofisini kwake leo jijini Dar es Salaam.

Lengo kuu la majadiliano hayo ni kupata ufafanuzi wa awali na kutambua maeneo ambayo Wizara itaweza kushirikiana na kampuni hiyo ili kuongeza ajira kwa vijana haswa ajira ya kujitegemea, pamoja na kuwajengea uwezo vijana katika masuala ya ujasiriamali, uongozi na ufundi makanika.

“Programu itakayoanzishwa italenga vijana hususani wale wanaojihusisha na ufundi makanika, madereva wa daladala, pamoja na waendesha pikipiki kwa maana ya usalama wao, usalama wa pikipiki na ujasiriamali utakaowawezesha kujipatia kipato na kuleta maendeleo katika jamii” amesema Pro. Gabriel.
Kwa upande wake Mkuu wa Kampuni ya TATA Africa Holdings (Tanzania) Ltd Bw. Prashant Shukla ameiahidi Wizara kushirikiana nayo bega kwa bega muda wote ili kuhakikisha kuwa tatizo la vijana mitahani linaisha na kuwa na vijana ambao wanauelewa na uwezo wa kuleta maendeleo katika jamii yao.

Naye Mkurugenzi Maendeleo ya Vijana Bw. James Kajugusi ameitaka kampuni hiyo kushirikiana na Wizara kwa kuchukua fursa ya kuboresha karakana ya Ufundi makanika iliyopo katika kituo cha vijana Ilonga Morogoro kama njia mojawapo ya kuwakomboa vijana na kuleta maendeleo.

No comments:

Post a Comment