Na Mahmoud Zubeiry wa Bin Zubeiry Blog, Dar es Salaam
AZAM FC imepata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Ferroviario de Beira ya Msumbiji katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Awali Kombe la Shirikisho Afrika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam jioni hii.
Shukrani kwake mshambuliaji kutoka Ivory Coast, Kipre Herman Tchetche aliyefunga bao hilo pekee dakika ya 41 baada ya kutengewa pasi nzuri ya kichwa na Mganda Brian Umony na kufumua shuti kali.
Mchezo ulikuwa mkali dakika zote 90 na mashambulizi yalikuwa ya pande zote mbili.
Mshambuliaji wa Ivory Coast, Kipre Tchetche na Mganda Umony kwa pamoja na Mzanzibari Khamis Mcha ‘Vialli’ walikuwa mwiba kwa safu ya ulinzi ya Ferroviario.
Kipindi cha pili, Ferroviario walicharuka zaidi na Azam nao walipoteza nafasi kama tatu za kufunga mabao mwanzoni.
Refa Mutaz Abdelbasit Khairalla na wasaidizi wake Waleed Ahmed Ali na Aarif Hassan Eltom wote kutoka Sudan walionekana kabisa kuwapendelea wageni katika maamuzi yao.
Dakika ya 70 beki mmoja wa Ferroviario aliunawa mpira wazi wazi kwenye eneo la hatari kufuatia shuti la Kipre Tchetche mbele ya refa, lakini akapeta.
Kiungo mkabaji wa Ferroviario, de Beira akipiga tik tak dhidi ya mshambuliaji wa Azam FC, Brian Umony leo Chamazi |
Matokeo hayo yanamaanisha Azam itakuwa na kazi ngumu katika mchezo wa marudiano wiki mbili zijazo nchini Msumbiji, wakitakiwa kulazimisha sare ili kusonga mbele.
Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Mwadini Ali, Erasto Nyoni, Malika Ndeule, Aggrey Morris, Said Mourad, Kipre Balou, Salum Abubakar, Himid Mao, Khamis Mcha/John Bocco dk61, Kipre Tchetche na Brian Umony/Jabir Aziz dk81.
Ferroviarrio; William Manyatera, Zefanis Matsinhe, Emidio Matsinhe, Abrao Cura/Kiki Simao, Edson Morais, Reinildo Mandava, Valter Mandava/Hery Antony, Antonio Machava, Manuel Fernandes, Mario Sinamunda na Manuel Correia/Dje Buzana.
No comments:
Post a Comment