Waandamanaji nchini Thailand wameanza kuweka vizuizi barabarani
katika baadhi ya maeneo ya mji mkuu Bangkok, katika harakati za kuiangusha
serikali kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa Februari Pili mwaka huu.
Waandamanaji hao wanaweka vizuizi na kudhibiti makutano ya barabara muhimu
mjini humo.Waandamanji hao ambao walianza kampeni yao mwezi Novemba mwaka jana, wanataka kuiondoa serikali ya waziri mkuu Yingluck Shinawatra na kuliweka "baraza la wananchi" lisilochaguliwa.
Wanasema Bi Yingluck ni wakala wa kaka yake, waziri mkuu wa zamani wa Thailand Thaksin Shinawatra, ambaye aliondolewa madarakani na jeshi mwaka 2006 na kwa sasa anaishi uhamishoni.
Waandamanaji wanashutumu sera za vyama washirika wa Thaksin, kwamba zimeharibu demokrasia nchini humo.
Vyama washirika wa Thaksin vinaungwa mkono kwa kiasi kikubwa na wapiga kura kutoka maeneo ya vijijini na vimeshinda mara nne katika uchaguzi uliopita. Chama kikuu cha upinzani kwa sasa kinagomea uchaguzi wa Februari Pili.
Jumapili usiku, mtu mwenye silaha ambaye hakutambulika aliwashambulia waandamanaji katika eneo la maandamano, na kumuua mtu mmoja.
Polisi wanasema mtu huyo mwenye silaha pia alifyatua risasi kuelekea katika makao makuu ya chama cha upinzani, japo hakuna taarifa za vifo.
No comments:
Post a Comment