TANGAZO


Monday, January 13, 2014

Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa yakutana Zanzibar

*Yamteu mwanachama wake, Mahmoud Thabit Kombo kuwa mgombea wa uwakilishi Jimbo la Kiembesamaki
*Kesho kuchukua fomu ya kugombea


Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, Rais Jakaya Mrisho Kikwete akikiongoza kikao cha Kamati Kuu, kilichofanyika mjini Unguja leo.

Na mwandishi wetu
KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa imefanya kikao cha siku moja leo, Januari 13, 2014, mjini Zanzibar chini ya Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Dk. Jakaya Kikwete.

Katika taarifa iliyotolewa leo na Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, imesema kuwa pamoja na mambo mengine Kamati hiyo, imeipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Wazanzibari na Watanzania wote kwa ujumla kwa kuadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Aidha, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepongezwa kwa maandalizi mazuri na yenye kufana ya sherehe hizo za Mapinduzi yaliyoadhimishwa jana visiwani humo.

Kamati Kuu pia imeeleza kutambua kwake na kupongeza hatua kubwa ya maendeleo zilizofikiwa tangu mapinduzi hayo ya mwaka 1964 mpaka leo.

Kamati Kuu imetoa wito wa kuyalinda na kuyaendeleza yale mema yote yatokanayo na mapinduzi hayo na mafanikio yaliyoletwa na serikali inayoongozwa na chama hicho visiwani humo.

Aidha Kamati Kuu hiyo, imemtangaza mwanachama wake,  Mahmoud Thabit Kombo kuwa mgombea wa kiti cha Uwakilishi kwenye Jimbo la Kiembesamaki na pia kuelezea kuwa mgombea huo kesho kuwa atachukua fomu za tume za kugombea.

Aidha, Kamati hiyo, ilielezea kuwa uzinduzi wa kampeni za chama hicho, utafanyika Januari 22, mwaka huu, katika Viwanja vya Kiembesamaki, ambapo mgeni wake rasmi atakuwa Mjumbe wa Kamati Kuu na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohamed Gharib Bilal.

Kampeni za CCM zitafungwa tarehe 01/02/2014 huko Chukwani na mgeni Rasmi atakuwa Mjumbe wa Kamati Kuu na Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Ndg. Balozi Seif Ali Idi.

Pia imeelezea kuwa kampeni za chama hicho zitaendeshwa na Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Dimani, viongozi na wanachama wa Wilaya hiyo na kufafanua kuwa ngazi zingine za CCM zitashirikiana na ngazi ya wilaya kuhakikisha cha hicho kinaunyakua tena ushindi wa jimbo hilo, lililokuwa likishikiliwa na mwanachama aliyefukuzwa, Mansour Yussuf Himid.


Aidha, Kamati Kuu hiyo, imetaka uchaguzi huo kuendeshwa kwa amani na utulivu na kuutakia kila lakheri kuanzia kwenye kampeni na hatimaye uchaguzi huo.

No comments:

Post a Comment