TANGAZO


Friday, December 27, 2013

Mtu mmoja auawa katika mapigano Cairo

 

vikosi vya usalama vikiwafukuza waandamanaji Cairo
 
Mtu mmoja ameuawa katika mapigano kati ya wanafunzi wanaokiunga mkono Chama cha Muslim Brotherhood na wakazi jijini Cairo nchini Misri, maafisa wameeleza.
Maafisa mjini humo wamesema kuwa mwanafunzi mmoja alipoteza maisha baada ya pande hizo mbili kushambuliana kwa risasi katika mji wa Nasr.
 
Tukio hilo limetokea siku moja baada ya Serikali ya Misri kukitaja chama cha Muslim Brotherhood kuwa kundi la kigaidi.
Katika tukio jingine, watu watano wamejeruhiwa kwa bomu lililokuwa karibu na basi moja mjini Nasr, bomu hilo lilitegwa na kulipuka wakati basi hilo lilipokuwa likipita karibu na eneo lilipotegwa bomu.
Hakuna kundi lolote lililokiri kuhusika na tukio hilo.
Siku ya alhamisi, takriban wafuasi 16 wa chama cha Muslim Brotherhood walikamatwa wakishutumiwa kujihusisha na kundi hilo linalodaiwa kuwa la kigaidi.

Miongoni mwa waliokamatwa ni Mtoto wa Naibu Kiongozi wa Chama hicho.
Shirika la Habari la Misri, Mena limesema Watu hao walikamatwa na kushutumiwa kuchochea machafuko na mapigano dhidi ya Jeshi na Polisi.

Siku ya jumanne, Watu 16 waliuawa na zaidi ya 100 walijeruhiwa katika shambulio la bomu lililokuwa limetegwa kwenye gari katika jengo la usalama mjini Mansoura, Maafisa wameeleza.
Serikali imesema kuwa Muslim Brotherhood inahusika na shambulio hilo, madai ambayo yamepingwa vikali na Chama hicho.

Kundi lenye uhusiano na Al Qaeda, Ansar Beit al-Maqdis (washindi wa Yerusalemu) walikiri kuhusika na shambulio hilo.

No comments:

Post a Comment