Baadhi ya waandishi wa habari, wakimsikiliza Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba wakati alipokuwa akisoma maazimio ya Baraza Kuu la Uongozi Taifa la chama hicho, jijini Dar es Salaam leo. (Picha zote na Kassim Mbarouk-www.bayana.blogspot.com)
BARAZA Kuu la
Uongozi Taifa la The Civic United Front (CUF- Chama Cha Wananchi) limekutana katika
kikao chake cha kawaida kwa mujibu wa Katiba ya Chama, kikao ambacho
kimeongozwa na Mwenyekiti wa Chama Taifa, Mhe. Prof Ibrahim Lipumba na kufanyika
katika Ukumbi wa Shabani Hamisi Mloo , Dar es salaam, tarehe 21-22 Dec, 2013. Katika kikao
hicho, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limepokea, limejadili na kuzifanyia
maamuzi Agenda zilizowasilishwa na Kamati ya Utendaji ya Taifa na kufikia
maazimio yafuatayo:-
1.
KUHUSU MPANGO MKAKATI WA CHAMA
Baraza Kuu limepokea Taarifa ya
Mpango Mkakati wa Chama kuelekea Chaguzi za Serikali za Mitaa,Vijiji na
Vitongoji 2014 na Uchaguzi Mkuu 2015, na limeridhia Mpango huo baada ya
Kujadili kwa Kina na linaamini kupitia Mpango huu Chama kitapata Mafanikio
Makubwa.
2.
KUHUSU UCHAGUZI WA NDANI YA CHAMA
(a)
Baraza Kuu
limepokea Taarifa ya Maendeleo ya Uchaguzi wa Ndani ya Chama na kuridhia utaratibu
unaoendelea katika Uchaguzi na kuiagiza Kamati Tendaji kusimamia kwa karibu
Uchaguzi huo.
(b)
Baraza Kuu linatoa
wito kwa Wanachama wa CUF kushiriki kwenye Uchaguzi kwa kufuata taratibu za
kidemokrasia bila ya kufanya kampeni za kuchafuana wala kutoa au kupokea rushwa.
3.
KUHUSU TAARIFA ZA FEDHA
Baraza Kuu
la Uongozi ilinampongeza Mkurugenzi wa Fedha kwa kuandaa Taarifa za Fedha
kuanzia za kila mwaka toka 2009 mpaka 2012 na kuziwasilisha kwa Msajili wa
Vyama na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa wakati.
4.
KUHUSU MAPENDEKEZO YA KAMATI YA BUNGE JUU YA OPERESHENI
TOKOMEZA UJANGIRI
(a)
Baraza Kuu linapongeza
Bunge la Jamuhuri ya Muungano na kukubaliana na Mapendekezo hayo yaliotolewa na
Kamati ndogo ilioongozwa na Mhe. James Limbeli nakupelekea Mawaziri watatu
kuvuliwa nyadhifa zao na Mmoja kujiuzulu mwenyewe. Kamati hii imetoa
mapendekezo mazuri juu ya uhalifu na unyanywasaji waliofanyiwa Wananchi.
(b)
Baraza Kuu
linamtaka Waziri Mkuu kuwajibika kwa matokeo ya Operesheni Tokomeza Ujangiri,
kwa kuwa yeye ndiye chanzo kikuu cha udhalilishaji wa wananchi na hata kupoteza
maisha kwa baadhi ya wananchi. Kauli yake ya PIGA TU, TUMECHOKA aliyoitamka
ndani ya Bunge imehamasisha unyanywasaji wa Wananchi unaofanywa na vyombo vya
dola, kwa hivyo Waziri Mkuu anapaswa kujiuzulu kwa matukio haya. La sivyo Rais
amfukuze kazi.
(c)
Baraza Kuu linatoa
wito kwa Serikali kuwachukulia hatua za kisheria wale wote waliohusika na
uvunjwaji wa Haki za Binadamu na unyanyasaji wa Wananchi kwa kuwafikisha
Mahakamani.
(d)
Baraza Kuu linatoa
wito kwa Serikali kutazama utaratibu wa kuwalipa fidia Wananchi wote walioathirika
na Vitendo hivyo.
5.
RAIS SHEIN AJIFUNZE TOKA KWA RAIS KIKWETE
Baraza Kuu
la Uongozi linamtaka Rais wa Serikali ya Zanzibar kuiga mfano wa Rais Kikwete
katika kushughulikia kero zinazoibuliwa na Vikao vya Baraza la Wawakilishi kwa
kuwawajibisha Mawaziri wanaohusika kama ambavyo Rais Kikwete amekua akifanya
katika kuunga mkono hoja zinazoibuliwa
Bungeni.
6.
KUHUSU TUHUMA ZA KATIBU MKUU WA CCM DHIDI YA MAWAZIRI
MIZIGO
Baraza Kuu
la Uongozi limesisitiza kuwa mara kadhaa CUF imekua ikieleza na kuonyesha OMBWE
LA UONGOZI ndani ya Nchi yetu unaosababishwa na CCM na Serikali yake. CUF
inaona kwamba, kutokana na Hoja nzito zinazojengwa na Katibu Mkuu wa CCM na
Katibu wa Itikadi wa CCM ni kielelezo tosha cha uwepo wa OMBWE LA UONGOZI.
Katika hali kama hii ambapo Katibu Mkuu wa Chama kinachotawala anaposhindwa
kujenga hoja kwenye vikao vya Chama chake na kuwachukulia hatua wahusika na
badala yake analazimika kujenga kwenye mikutano ya hadhara inaonyesha kuwa tuna
Serikali inayokosa usimamizi kutokana na udhaifu wa Chama kinachounda Serikali.
7.
KUHUSU UVUNJIFU WA HAKI ZA BINADAMU UNAOFANYWA NA VYOMBO
VYA DOLA
Baraza Kuu
linatoa wito kwa vyombo vya dola kuwa na weledi na uadilifu na kuheshimu na
kulinda haki za binadamu za wananchi. Vyombo vya dola viache kujibu malalamiko
na hoja za wananchi kwa matumizi makubwa kupita kiasi ya nguvu za dola.
Matumizi ya nguvu kubwa kupita kiasi ya vyombo vya dola ni tatizo kubwa
linalokua kwa kasi ndani ya nchi yetu. Wakati mwingine imefikia wananchi kuamua
kujibu mapigo kwa kuchukua hatua za sheria mikononi mwao. CUF Inatoa wito kwa
Vyombo vya Dola kuheshimu sheria na haki za binadamu na wasitekeleze amri za
wanasiasa zisizojali utawala wa sheria na haki za binadamu ili kujijengea
heshima na kupunguza uhasama baina ya vyombo vya dola na wananchi.
8.
KUHUSU MIGOGORO YA WAKULIMA NA WAFUGAJI
Baraza Kuu
linatoa wito kwa Serikali kutafuta utaratibu wa kumaliza migogoro kati ya wakulima
na wafugaji ambayo inachochewa na kukithiri kwa rushwa kwa viongozi wa serikali
katika ngazi ya vijiji, kata na wilaya. Ni muhimu kuwa na sera nzuri zinazotenga maeneo ya ufugaji na
kuhamasisha ufugaji wa kisasa unaozingatia ulinzi wa mazingira na kuitumia
mifugo kuongeza kipato na kuboresha maisha ya wafugaji. Sera hii itapunguza tatizo
la uhasama kati ya wakulima na wafugaji ambalo limekua tatizo kubwa ndani ya nchi
yetu.
9.
WITO KWA SERIKALI KUTOTUMIA VYOMBO VYA DOLA KIOPERESHENI
Baraza Kuu Iinatoa
wito kwa Serikali kujenga uwezo endelevu wa kusimamia sheria za nchi ikiwemo
kulinda hifadhi za taifa na kuepuka kulazimika kutumia operesheni baada ya
tatizo kuwa sugu. Serikali isilitumie Jeshi la Wananchi wa Tanzania katika
kushughulikia masuala ya uvunjifu wa sheria katika maeneo mbali mbali ya nchi
yetu, na badala yake kazi hiyo ifanywe na Jeshi la Polisi kwa mujibu wa taratibu
za kisheria. Jeshi la Polisi liongezewe uwezo wa kutimiza majukumu yake huku
likiheshimu haki za kisheria za watuhumiwa. Jeshi la Wananchi liachiwe majukumu
yake ya kulinda mipaka ya nchi yetu. CUF Inaona kwamba si vyema kulitumia Jeshi
letu la kulinda mipaka ya nchi katika Operesheni zinazohusu uvunjaji wa sheria
unaofanywa na wananchi. Askari wa JWTZ hawana mafunzo ya kukamata mwananchi
mwenye tuhuma za uhalifu bila kuvunja haki zake za kisheria.
10.
KUHUSU MUUNDO WA MUUNGANO NA MCHAKATO WA KATIBA
Baraza Kuu linaamini
kwamba rasimu ya mwisho ya katiba ya Tume ya Jaji Warioba haitakuwa na mabadiliko
makubwa kuhusu muundo wa muungano wa serikali tatu uliopendekezwa katika rasimu
ya kwanza ya katiba. Baraza Kuu linaamini kwamba uwepo wa serikali tatu katika
muundo wa muungano ni jambo muhimu na ni njia mojawapo ya kumaliza kero za muungano.
Baraza Kuu linaitaka Serikali kusimamia kikamilifu mchakato wa Katiba Mpya ili
iweze kupatikana kabla ya Uchaguzi wa 2015. Ni wazi wananchi hawatakubali
kuingia kwenye Uchaguzi 2015 kwa kwa kutumia katiba ya sasa ambayo imekataliwa
na Watanzania wengi waliotoa maoni yao kwa Tume ya Jaji Warioba.
11.
KUHUSU HOJA YA UUNDAJI WA SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA
Baraza Kuu linamshauri
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, aunde Serikali ya Umoja wa Kitaifa
ili iweze kusaidia kupatikana kwa Katiba mpya katika kipindi hiki cha mpito.
Uwepo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa utarahisisha mjadala wa Bunge la Katiba
na kulifanya bunge la Katiba kuchukua sura ya Kitaifa zaidi na hivyo kurahisha
upatikanaji wa Katiba ya Taifa kwa misingi ya utashi wa Wananchi. Serikali ya
Umoja wa Kitaifa itampa fursa Rais kuteua Baraza la Mawaziri lililo imara na
kuondokana na Mawaziri wanaonekana ni mizigo ili ashughulikie matatizo mazito
yanayolikabili taifa ikiwemo ongezeka ya gharama ya maisha, ukosefu wa ajira,
kuporomoka kwa elimu, huduma hafifu za afya na maji safi na salama na ukosefu
wa umeme wa uhakika.
12.
MKUTANO WA WADAU KUJADILI RASIMU YA KATIBA KABLA YA
KUANZA BUNGE LA KATIBA
Baraza Kuu linatoa wito wa
kuwepo mkutano wa wadau hususan vyama vya siasa na asasi za kiraia kujadili
rasimu ya mwisho ya katiba kwa lengo la kufikia maridhiano ya mambo muhimu yaliyomo
ndani ya rasimu ya katiba ili kurahisisha kazi ya Bunge la Katiba kufikaia
muafaka kuhusu vipenger muhimu vya katiba mpya
13.
KUHUSU VITAMBULISHO VYA TAIFA VYA NIDA
Baraza Kuu
linakumbusha kauli ya Mheshimiwa Rais Kikwete mwezi wa Februari 2013, siku ya
uzinduzi wa vitambulisho vya taifa katika viwanja vya Karimjee Hall, alieleza
kuwa vitambulisho hivyo ndivyo vitakavyotumika katika kura ya maoni na uchaguzi
mkuu ujao. Kasi ya uandikishaji wa vitambulisho hivyo ni ndogo sana na haiwezi
kufanikisha kuwapa vitambulisho Watanzania wote wenye umri wa miaka 18 au zaidi
kabla ya kura ya maoni na hata mwaka 2015. Mpaka hivi sasa mwaka wa 2013
unamalizika Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) haijakamilisha utoaji wa
vitambulisho mkoa wa Dar es Salaam. Lakini pia kuna vikwazo vingi katika
uandikishaji wa vitambulisho hivyo na hasa pale unpohitajika kupata barua toka
kwa Mjumbe wa Nyumba kumi kumi, ambae Sheria haimtambui na kwa hakika wajumbe
hawa ni wa CCM. Baraza Kuu linatoa wito kwa Serikali kuondosha utaratibu huu wa
kutumia Wajumbe wa Nyumba kumi kumi katika zoezi hili il kuleta ufanisi.
14.
KUHUSU DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA KATIKA
KUFANIKISHA KURA YA MAONI YA KATIBA
Baraza Kuu
limesikitishwa na hali ya kuwa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura halijaboreshwa
tangu kumalizika uchaguzi wa 2015. Sensa ya mwaka 2012 inaonyesha kuwa kuna
wananchi zaidi ya milioni 3.5 watakaokuwa wamefikisha umri wa miaka 18 kati ya
2010 na 2014. Wananchi wengi na hasa vijana wamepoteza vitambulisho vyaovya
kupigia kura. Baraza Kuu linatoa wito kwa serikali na Tume ya Uchaguzi
kuboresha daftari la wapiga kuandikisha wapiga kura wapya na kwapa vitambulisho
vipya waliopoteza vitambulisho vya ili kutoa fursa kwa wananchi wenye haki ya
kupiga kura kushiriki kupiga kura ya maoni ya kuridhia au kukataa Rasimu ya
Katiba baada ya kujadiliwa na kupitishwa na BUNGE LA KATIBA la Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania.
15.
DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA LA ZANZIBAR
Baraza Kuu
linaitaka Serikali ya Mapinduzi iongeze uwajibikaji na kutoa Haki za kimsingi
za Wananchi wa Zanzibar ikiwemo utoaji wa ZANID na kuandikisha Wananchi
waliofikisha umri wa Miaka 18 katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wa
Zanzibar chini ya ZEC. Sheria ya ZANID inavunja Katiba ya Zanzibar kifungu cha
5 kinachoeleza kuwa “Zanzibar itafuata mfumo wa Kidemokrasia wa Vyama Vingi vya
Siasa wenye kuheshimu utawala wa sheria, haki za binaadamu, usawa, amani, haki
na uadilifu.” Na kifungu cha 7 (1) kinachoeleza kuwa “Kila Mzanzibari aliyetimiza umri wa miaka
kumi na nane anayo haki ya kupiga kura katika uchaguzi unaofanywa Zanzibar na wananchi.” Baraza Kuu linatoa wito kwa Tume ya Uchaguzi ya Taifa
(NEC) kuwaandikisha Wazanzibari wote walionyimwa ZANID alau wapate fursa ya
kupiga kura ya maoni kama Wazanzibari kuikubali au kuikataa Katiba Mpya
itakayopitishwa na Bunge la Katiba.
16.
UKOSEFU WA UADILIFU NA UZEMBE WA ZEC
Baraza Kuu
la Uongozi linalaani upoteaji wa Takwimu za Uandikishaji wa Daftari la Kudumu
la Wapiga Kura kwa Majimbo ya Donge, Kitope, Bumbwini, Mfenesini na Bububu. Baraza
Kuu linaitaka ZEC kuwaandikisha wananchi wote bila usumbufu waliyokuwemo ndani
ya daftari ambazo takwimu zake zinasemekana zimefutika.
17.
KUHUSU MBINU ZA KUPUNGUZA MAJIMBO YA PEMBA
Baraza Kuu
limejadili kwa kina uvumi na mbinu za ZEC kutaka kupunguza baadhi ya majimbo
kwa upande wa Pemba na kuongeza majimbo kwa upande wa Unguja. Baraza Kuu
linaipinga vikali dhana hii inayoweza kuturudisha kwenye siasa za uhasama
katika kipindi hiki ambacho Zanzibar imeshaanza kutulia. Baraza Kuu linaitaka
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ZEC kutopunguza Majimbo ya Uchaguzi ya
Pemba
18.
KUHUSU SHEREHE YA MIAKA 50 YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR
Baraza Kuu
linaipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kutimiza Miaka 50 ya Mapinduzi
ya Zanzibar, na linaitaka kuendeleza maridhiano, mshikamano na umoja wa Kitaifa
uliopo hivi sasa na kutumia umoja huo kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Baraza Kuu Linawataka Wazanzibari kutumia sherehe za Mapinduzi Matukufu ya
Zanzibar kuimarisha umoja wao na kuendelea kuondosha siasa za chuki zilizodumu
kwa miaka mingi na linatoa wito kwa Wazanzibari na Watanzania wote na hususan
wana CUF kushiriki kikamilifu katika kusheherkea miaka 50 ya Mapinduzi.
19.
KUHUSU MGOGORO WA CHADEMA
Baraza Kuu linatoa wito kwa CHADEMA
kumaliza mgogoro wao ili kuweka nguvu kwenye Bunge la Katiba. Suala la kupata
Katiba Mpya yenye misingi imara ya demokrasia na utawala bora linapaswa kupewa
kipaumbele na kuwaunganisha viongozi wa CHADEMA katika kulisimamia. Kwa hali
ilivyosasa na kama itaendelea kuwa hivyo, basi ni dhahiri kwamba nguvu kubwa ya
CHADEMA itaelekezwa kwenye kushughulika na mgogoro wao, jambo ambalo litaathiri
ushiriki wao katika mjadala wa Katiba kwenye Bunge la Katiba. Katika mchakato
wa kupata katiba mpya CHADEMA ni miongoni mwa vyama vilivyotoa mchango mkubwa.
Umoja wa CHADEMA unahitajika kuhakikisha kuwa Chama hicho kinaitumia fursa hii
muhimu na adimu kwa maslahi ya taifa letu.
20.
WITO KWA VYAMA KUWEKA MASLAHI YA TAIFA KWENYE BUNGE LA
KATIBA
Baraza Kuu linatoa wito kwa Vyama Vyenye Wabunge kuacha
kupigania maslahi ya Vyama vyao wakati wa Mjadala wa Bunge la Katiba. Ni
dhahiri kwamba Katiba inayoandikwa ni Katiba ya Nchi na si ya Chama chochote,
hivyo ni muhimu kwa wabunge wa Bunge la Katiba kuwa Wazalendo, kwa kutoa
michango itayowezesha kupatikana Katiba bora ya Nchi yetu badala ya kutoa
michango itayowezesha kupatikana kwa Katiba yenye maslahi na Vyama vyetu.
MWISHO;
The Civic United Front (CUF-Chama Cha Wananchi) na viongozi wake
inawahakikishia Watanzania wote kuwa Wabunge na Wawakilishi wa CUF watakaoingia
katika Bunge la Katiba watakuwa wazalendo na waadilifu na wataweka mbele
maslahi ya taifa letu na wananchi wa pande mbili za Muungano wetu ili tupate
katiba yenye misingi imara ya demokrasia na utawala bora na itakayohakikisha
kuwa raslimali na maliasili ya taifa letu inatumiwa kwa manufaa ya wananchi
wote.
HAKI SAWA KWA WOTE.
Imetolewa na;
Baraza Kuu
La Uongozi
Taifa, Tarehe 24 Disemba 2013
PROF IBRAHIM HARUNA
LIPUMBA MWENYEKITI WA CUF TAIFA.
No comments:
Post a Comment