TANGAZO


Friday, December 13, 2013

Lowassa anusurika kufa

*Ndege aliyopanda yapasuka matairi manne
*Alikuwa akitua uwanja wa Ndege wa Arusha

Aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa

Na Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amenusurika kifo baada ya ndege aliyokuwa akisafiria kupasuka matairi yote manne ya nyuma.
 
Lowassa alikuwa akisafiri kwa kutumia ndege ya Shirika la Ndege  la Precision aina ya ATR, ambapo wakati ilipokuwa ikitaka kutua ilipasuka matari yote manne ya nyuma.

Tukio hilo lilitokea leo mchana katika Uwanja wa Ndege wa Arusha ambapo katika ndege hiyo mbali ya Lowassa kulikuwa na abiria wengine.

Kutokana na ajali hiyo hofu kubwa ilitanda uwanjani hapo na hasa abiria waliokuwa ndani ya ndege hiyo akiwemo Lowassa.
 
Hata hivyo, baada ya ndege kufanikiwa kutua, abiria na watu walioshuhudia walisema kuwa , ajali hiyo ilikuwa mbaya na kupona kwa abiria hao ni mipango ya Mungu maana ilikuwa ajali mbaya.
 
Kwa mujibu wa mashuhuda waliokuwa eneo hilo, walisema kuwa hofu kubwa ilikuwa ni kwa Lowassa lakini baada ya kuona amesalimika walisema Mungu anampenda na kumpigania kwa
kila jambo.

"Yaani Mungu ni mkubwa kwa kweli, ametunusuru maisha yetu na kiongozi kipenzi chetu Lowassa...Mungu atamlinda jamani...siamini," alisikika akisema mama mmoja miongoni mwa
abiria hao, wakati akishuka.

Lowassa ni miongoni mwa wana CCM wanaotajwa kuwania urais 2015 na amekuwa na nguvu kubwa katika harakati hizo.
 
Lowassa ni Mbunge wa Monduli, jimbo ambalo anatoka Waziri Mkuu aliyekuwa kipenzi cha Mwalimu Julius Nyerere na watanzania,  Edward Moringe Sokione.
 
Sokoine alifariki katika ajali ya gari mwaka 1994 na inaaminika mwalimu alikuwa akimuandaa kurithi kiti cha urais.
 
Hata hivyo harakati za Lowassa kuwania urais baada ya Rais Jakaya Kikwete zimekuwa za waziwazi ingawa mwenye hajatamka rasmi kugombea au kutogombea.
 
Lowassa amekuwa akizungumza maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kushiriki katika masuala ya maendeleo ya Watanzania lakini pia amekuwa akichangia fedha kwa ajili ya maendeleo.

No comments:

Post a Comment