Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akifuatana na Balozi Mdogo wa Oman nchini
Tanzania, anayefanyia kazi zake Zanzibar, Saleh Suleiman Al
Harth, alipofika leo, Ikulu Mjini Zanzibar, kumuaga Rais baada ya kumaliza muda wake wa kazi nchini.
Na Said Ameir, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
amempongeza na kumshukuru Balozi Mdogo wa Oman anayemaliza muda wake Bwana Saleh
Suleiman Al Harth kwa jitihada zake kubwa za kuimarisha ushirikiano kati ya
Zanzibar na Oman wakati wote alipokuwa nchini.
Dk.
Shein ametoa pongezi na shukrani hizo jana wakati alipokuwa akizungumza na
Balozi mdogo huyo Ofisini kwake Ikulu ambako alikwenda kumuaga.
Mheshimiwa
Rais alibainisha katika mazungumzo hayo kuwa katika kipindi ambacho balozi huyo
amekuwepo nchini ushirikiano kati ya Zanzibar na Oman
umeimarika na kumekuwepo na mafanikio makubwa katika ushirikiano huo kwa pande
zote mbili.
“Kipindi
kifupi ulichokuwepo hapa, tumeshuhudia mafanikio makubwa katika uhusiano na
ushirikiano wetu wa kihistoria” alieleza Dk. Shein.
Aliongeza
kuwa ni muhimu kwa ushirikiano huo kuimarishwa zaidi na zaidi sio tu kutokana na
historia bali pia udugu na ukaribu wa watu wa Zanzibar na Oman.
Dk.
Shein alimueleza Balozi Al Harth kuwa Serikali na wananchi wa Zanzibar
wanathamini sana mchango unaotolewa na Serikali ya Oman kwa maendeleo ya
Zanzibar na kwamba daima wataendelea kushirikiana kuimarisha uhusiano na
ushirikiano uliopo kwa faida ya Serikali na wananchi wa nchi mbili
hizo.
Mheshimiwa
Rais alitumia fursa hiyo kutoa salamu za heri kwa Mfalme wa Oman Sultan Qaboos
na viongozi wengine wa nchi hiyo.
Kwa
upande wake Balozi Al Harth alimueleza Mheshimiwa Rais kuwa anaondoka Zanzibar
na kumbukumbu nzuri ya ukarimu na ushirikiano alioupata kutoka kwa Serikali na
wananchi wa Zanzibar wakati wote alipokuwa nchini.
“Nimetekeleza
majukumu yangu vizuri lakini nieleze ukweli nimesaidiwa sana na viongozi wa
watendaji wa Serikali” alieleza Balozi Al Harth na kubainisha kuwa hali hiyo
ilimfanya aifurahie kazi yake wakati wote.


No comments:
Post a Comment