TANGAZO


Monday, November 4, 2013

Mwakilishi wa Save the Children aaga kwa Rais Shein

Dk. Shein: Tutaendelea kufanyakazi kwa karibu na Shirika la Save the Children
 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Mwakilishi wa Shirika la Save The Children Bw. Mubarak Maman, alipofika kumuaga Rais leo, Ikulu Mjini Zanzibar, baada ya kumaliza muda wake wa kazi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Mwakilishi wa Shirika la Save The Children Bw. Mubarak Maman (katikati), alipofika kumuaga Rais leo, baada ya kumaliza muda wake wa kazi. Pia akiwa na Bibi Mali Nilsson (kushoto), ambaye alifika kujitambulisha Ikulu Mjini Zanzibar, kushika nafasi ya kuwa mwakilishi mpya wa shirika hilo, la Save The Children.  (Picha zote na Ramadhan Othman, Ikulu)

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameuhakikishia ujumbe wa Shirika la Save the Children kuwa Serikali itaendelea kufanyakazi nalo kwa karibu kwa kuwa lengo lao ni moja tu la kuhakikisha ulinzi, ustawi na maendeleo ya watoto nchini.
Katika mazungumzo yaliyofanyika leo, ofisini kwake Ikulu na Ujumbe wa Shirika hilo ulioongozwa na Mkurugenzi Mkaazi wake nchini Tanzania Bwana Steve Thorme, Dk. Shein amesisitiza kuwa Serikali yake inalipa kipaumbele suala la ulinzi na maendeleo ya mtoto hivyo ushirikiano na washirika wengine ni jambo linalokaribishwa.
“Tuko makini sana katika masuala ya watoto na kinamama na kwa kuwa masuala haya ni mtambuka ushirikiano na washirika wetu katika kuleta ustawi na maendeleo ya watoto ni suala tunalolipa umuhimu wa kipekee katika Serikali yetu”alisema Dk. Shein.
Rais aliueleza ujumbe huo kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaunga mkono shughuli za Shirika hilo nchini na kubainisha kuwa inathamini sana mchango wake mkubwa katika kuimarisha hali ya watoto na ustawi wao nchini.
“Sote tuna lengo moja la kuimarisha hali ya watoto nchini na ustawi wao hivyo nyinyi mnatuhitaji katika shughuli zenu na halikadhalika sisi Serikali tunawahitaji kutimiza malengo yetu ya kuimarisha hali ya watoto wetu nchini”alieleza.
Rais alibainisha kuwa amekuwa akifuatlia shughuli za shirika hilo tangu lilipoanzisha shughuli zake miaka ya themanini huko kisiwani Pemba na baadae Unguja na kwamba Serikali inaridhishwa na utendaji wake na misaada inayotoa humu nchini kwa maendeleo ya watoto.
“Si jambo la kunishangaza kusikia kuwa shughuli zenu hapa Zanzibar zimekuwa mfano kwa nchi nyingine kuja kujifunza na hili ni jambo la kujivunia kwetu sote kwa kuwa ni matokeo ya ushirikiano wetu”aliuambia ujumbe huo.
Dk. Shein amesema kuwa kuwafanyia mambo mazuri watoto kama kuwalinda dhidi ya unyanyasi pamoja na kuwapatia haki zao za msingi ni muhimu katika kujenga jamii yenye mustakabala mzuri na kuwa vitendo vyovyote za unyanyasaji wa watoto vinaichukuiza Serikali.
“Unyanyasaji watoto unanichukiza mimi binafsi na kuichukiza Serikali yangu na ndio maana tumechukua hatua mbalimbali kuhakikisha ulinzi na malezi bora ya watoto wetu” Dk. Shein aliongeza.
Dk. Shein alieleza matumaini yake kuwa ushirikiano wa karibu zaidi kati ya Serikali na Shirika hilo utatoa matokeo mazuri zaidi katika kuimarisha hali za watoto na kuwajenga sio tu mustakabali mzuri wa maisha yao binafsi bali pia taifa kwa ujumla.
Hata hivyo Dk. Shein alieleza kuwa pamoja na mafanikio yaliyopatikana bado kuna changamoto ambazo ni sehemu ya maisha na kwamba ni wajibu wa kila siku wa Serikali kuzifanyia kazi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika hilo Bwana Steve Thorme alieleza kufurahishwa kwake na mafanikio ya Zanzibar katika kuwapatia watoto ulinzi, haki na maendeleo pamoja na changamoto kadhaa Serikali inazopambana nazo.
“Tumefurahishwa sana na mafanikio mliyoyapata katika sekta hii ya watoto na Shirika letu lina shauku kubwa kubadilishana uzoefu kwa manufaa ya washirika wetu kwingineko”alieleza Bwana Thorme.
Aliongeza kuwa shirika lake hivi sasa linafanya mageuzi katika uendeshaji wa shughuli zake kwa kuliunganisha kuwa moja ili kuyaleta masuala ya watoto katika ngazi ya kimataifa kwa sauti moja.
“Tunafanya mageuzi katika shirika letu ili kuwa shirika moja lenye dira na dhima moja kuhusu watoto tofauti na hapo awali ambako kila nchi au kundi la nchi lilikuwa likifanya mambo kivyake vyake”Bwana Thorme alieleza.
Bwana Thorme ambaye alifuatana na mwakilishi wa shirika hilo Zanzibar Bibi Mali Nilsson alieleza kuwa chini ya mabadiliko hayo shirika litakuwa likifanya tathmini ya shughuli zake na kubadilishana uzoefu na nchi walengwa ili kuleta ufanisi na kuchochea matokeo mazuri zaidi katika shughuli zake.
“Tunataka kusikia maoni kutoka kwa jamii tunayoshirikiana nayo juu ya shughuli zetu kwani wao ndio walengwa iwe ni kuhusu kupiga vita utumikishaji watoto au harakati dhidi ya matumizi ya viboko maskulini” alieleza Bwana Thorme.
Katika mazungumzo ilibainika kuwa Zanzibar imepiga hatua mbele zaidi kulinganisha na nchi nyingi jirani katika kulinda haki na maendeleo ya motto na kujenga ustawi wao.
Kuanzishwa kwa sheria ya haki na ulinzi wa watoto pamoja na kuanzishwa mahkama ya watoto ni miongoni mwa masuala ya kijivunia katika kuwapa ulinzi  watoto.
Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, wanawake na Watoto Mheshimiwa Zainab Omar, Katibu Mkuu wa wizara hiyo Bibi Amina Abdalla Juma na Naibu Katibu Mkuu Bwana Mshamu Abdalla Khamis.       

No comments:

Post a Comment