TANGAZO


Friday, November 15, 2013

Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi Serikalini (GEPF), wasajili wanachama 18,050 katika mpango wa hiyari wa Akiba ya Uzeeni



Mkurugenzi wa Masoko na uendeshaji toka mfuko wa hifadhi ya jamii GEPF Bw. Anselim Peter akieleza kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu mfumo mpya unaowapa fursa wananchi walio katika sekta isiyo rasmi kujiwekea akiba katika mfuko huo. Kushoto ni Meneja Masoko na Huduma kwa Wateja, Bw. Aloyce Ntukamazima. (Picha zote na Frank Mvungi, Maelezo)
Mkurugenzi wa Masoko na Uendeshaji toka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii GEPF, Bw. Anselim Peter akieleza kwa waandishi wa habari (hawapo pichani), kuhusu mfumo mpya unaowapa fursa wananchi walio katika sekta isiyo rasmi kujiwekea akiba katika mfuko huo, kushoto ni Meneja Masoko na Huduma kwa wateja Bw. Aloyce Ntukamazima,kulia ni Afisa Habari wa Idara ya Habari Maelezo Bi. Fatma Salum.


Na Frank Mvungi, Maelezo
MFUKO wa Akiba ya Wafanyakazi Serikalini (GEPF), umefanikiwa kusajili wanachama 18,050 katika mpango wa hiari wa kujiwekea akiba ya uzeeni.

Hayo yamesemwa na  Mkurugenzi wa Masoko na Uendeshaji Bw. Anselim Peter wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es salaam mapema leo.

Akifafanua Bw. Anselim amesema mfuko huo umetoa fursa kwa wananchi na watu wote walio katika sekta isiyo rasmi kujiwekea akiba ya uzeeni katika mfuko huo ambapo mpango huo unawapa nafasi wanachama kutuma michango yao kwa njia ya mitandao ya simu.

Aliongeza kuwa katika mpango huo akiba za wanachama zimefikia fedha za Tanzania zaidi ya bilioni 3 ikiwa  ni kiashiria kuwa wananchi wamekuwa na mwitikio mzuri wa kujiunga na mfuko huo.

Akifafanua zaidi  Anselim amesema matarajio yao kufikia mwaka 2014 ni kusajili wanachama 33,226 ili kufanya mfuko huo kukua kadiri ya malengo iliyojiwekea.

Alibainisha pia kuwa akiba za wanachama zitafikia zaidi ya bilioni 5 ikiwa ni hatua muhimu katika kukua kwa mfuko huo.

Mpango wa hiari wa kujiwekea akiba ya uzeeni (VSRS) ulibuniwa mwaka 2009 ili kutoa fursa kwa watu wote kuweka akiba ambayo itawasaidia kupambana na majanga mbalimbali.mpango huu ni matokeo ya mageuzi katika sekta ambayo kila mtu mwenye uwezo wa kuzalisha kipato anaweza kujiunga na hifadhi ya jamii.

No comments:

Post a Comment