1. UTANGLIZI
Mfuko wa Kuhifadhi Wanyamapori Tanzania (TWPF) ulianzishwa
mwaka 1978 baada ya kufanya marekebisho (ammendmend) ya kifungu cha 69 cha
Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori (Wildlife Conservation Act) Na. 12 ya mwaka
1974. Marekebisho hayo yalitangazwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 21 la tarehe
22 Mei, 1981.
Sheria
ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya sasa Na.5 ya mwaka 2009 inabainisha uwepo wa
Mfuko kisheria katika kifungu cha 91(1).
Mfuko ulianzishwa kwa lengo la kuiongezea Idara ya
Wanyamapori uwezo wa kifedha wa kutekeleza majukumu yake ya ulinzi wa wanyamapori.
Serikali ilitambua kuwa ulinzi wa wanyamapori unahitaji fedha nyingi na fedha
kutoka Hazina hazikidhi mahitaji yaliyopo.
Mfuko
hugharamia majukumu mbalimbali ya Idara ya Wanyamapori ikiwa ni pamoja na uzuiaji ujangili, uendelezaji wa mapori ya akiba,
usimamizi wa matumizi ya wanyamapori, utunzaji wa kanzidata na kuwezesha watumishi kuhudhuria mafunzo
mbalimbali.
2. UZUIAJI UJANGILI
Mfuko
hugharamia shughuli za doria ndani na nje ya Mapori ya Akiba na doria za
kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu ikiwa ni pamoja na kukabiliana na
tatizo la kunguru weusi katika mikoa mbalimbali nchini.
Mfuko
hufanya malipo ya kifuta machozi kwa wananchi ambao ndugu zao wameuawa au
kujeruhiwa na wanyamapori. Aidha, Mfuko hulipa kifuta jasho kwa wananchi ambao
mashamba yao yameharibiwa na wanyamapori. Wananchi ambao mashamba yao yameharibiwa
na wanyamapori wanatakiwa kutoa taarifa kwenye ofisi ya kijiji iliyopo karibu
ndani ya siku tatu tangu uharibifu ulipotokea. Uongozi wa kijiji husika hutoa
taarifa Wilayani ili wataalam wa kilimo na wanyamapori wafanye tathmini ya
uharibifu uliotokea.
Kwa upande
wa watu wanaojeruhiwa au kuuawa na wanyamapori ni lazima uharibifu uthibitishwe
na dakatari. Aidha, ni lazima awepo shahidi kutoka katika eneo husika ambaye si
ndugu wa familia iliyoathirika ili kuepuka udanganyifu. Uongozi wa wilaya
husika hutuma maombi ya fedha za kifuta jasho/machozi kwa Mkurugenzi wa Idara
ya Wanyamapori. Aidha, Afisa kutoka Makao Makuu ya Idara ya Wanyamapori hutembelea
eneo husika ili kuhakiki uharibifu uliotokea kabla ya kufanya malipo endapo
kuna haja ya kufanya hivyo. Baada ya taratibu kukamilika fedha za kifuta
jasho/machozi hutumwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri husika ambapo huwapatiwa
waathirika au ndugu wa familia iliyoathirika.
Viwango vya
malipo ya kifuta jasho/machozi ni kama ifuatavyo:-
(a) Kupoteza
maisha (kifo) – shilingi 1,000,000/=
(b) Ulemavu wa
kudumu – shilingi 500,000/=
(c) Kujeruhiwa –
shilingi 200,000/=
(d) Uharibifu wa
mazao (kuanzia ekari 1 - 5):
(i)
Umbali wa kilo mita 0.5 kutoka
eneo la hifadhi – Hakuna malipo
(ii)
Umbali kuanzia kilo mita 1 – 4 kutoka eneo la
hifadhi – 25,000/=
(iii)
Umbali kilo mita 4 – 5 kutoka eneo la hifadhi – 75,000/=
(iv)
Umbali zaidi ya kilo mita 5 kutoka eneo la hifadhi
– 100,000/=
(e) Kifo cha
ng’ombe – 50,000/=
(f)
Kifo cha kondoo, mbuzi, nguruwe,
punda – 50,000/=
(g) Vifo vya
wanyama wengine – 10,000/=
3. UENDELEZAJI WANYAMAPORI
Mfuko
hugharimia shughuli mbalimbali za usimamizi wa wanyamapori ikiwa ni pamoja na
usimamizi wa maeneo ya jumuiya za hifadhi za wanyamapori (WMAs), kutoa elimu ya
uhifadhi kwa jamii, usimamizi wa maeneo ya ardhoevu na uendelezaji wa
miundombinu (nyumba za watumishi, barabara, mipaka na viwanja vya ndege) katika
mapori ya akiba.
4. UTAFITI, TAKWIMU NA MAFUNZO
Mfuko
hugharamia mafunzo ya muda mrefu kwa watumishi wa Idara ya Wanyamapori
wanaosoma katika vyuo vya Mweka na Pasiansi. Pia hugharamia mafunzo ya muda
mfupi kwa watumishi wa Idara katika vyuo mbalimbali ndani ya nchi. Aidha, Mfuko
huchangia uendeshaji wa vyuo vilivyo chini ya Idara ambavyo ni Pasiansi na
Likuyu-Sekamaganga.
Pia
Mfuko huchangia gharama za utafiti na kuidadi wanyamapori kupitia taasisi ya
Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI).
5. MATUMIZI YA
WANYAMAPORI
Mfuko hugharamia usimamizi wa
matumizi ya wanyamapori ambazo ni: ukusanyaji wa maduhuli, usimamizi wa
uwindaji wa kitalii na wa wenyeji, utalii wa picha, biashara ya wanyamapori hai
na mazao yatokanayo na wanyamapori, mashamba na bustani za ufugaji wa
wanyamapori.
6.
MIRADI YA MAENDELEO YA JAMII
Mfuko huchangia utekelezaji wa baadhi
ya miradi ya maendeleo kwenye jamii zinazozunguka maeneo yaliyohifadhiwa.
Miradi hiyo ni ile ya maji, afya, elimu na miradi ya vikundi vya wajasiriamali.
Mfuko huchangia kwenye miradi hiyo ili kuwezesha wananchi kuona faida za kuhifadhi
wanyamapori.
Miradi hiyo ni pamoja na: ujenzi
wa uzio wa shule ya walemavu- Ilembula (Njombe), ujenzi wa vyoo, mabafu na
ununuzi wa vitanda- shule ya sekondari ya Namanga (Longido), ukarabati wa bwawa
katika kijiji cha Mwakiloba- Wilaya ya Magu, ujenzi wa zahanati katika kata ya
Kwadelo- Kondoa, kuchangia ununuzi wa sare na vifaa vya shule kwa ajili ya
watoto yatima 168 katika Wilaya za Nachingwea, Kilwa, Lindi vijijini na Liwale,
ujenzi wa madarasa katika shule ya Sekondari ya Luduga- Njombe, ununuzi wa
mashine ya kusaga ya kikundi cha Enaboishu kijiji cha Kitendeni- Wilaya ya
Longido na Ujenzi wa bweni katika Shule ya Sekondari Wiliam Lukuvi- Iringa.
7.
CHANGAMOTO
Katika kutekeleza majukumu yake
Mfuko unakabiliwa na changamoto mbalimbali kubwa ikiwa ni ufinyu wa bajeti ikilinganishwa
na mahitaji yaliyopo.
8.
MIKAKATI
Katika kukabiliana na changamoto hizo
Mfuko unaendelea kutafuta vyanzo vipya vya mapato zaidi ya biashara ya uwindaji
wa kitalii ambao ndicho chanzo kikuu cha mapato kwa sasa. Miradi ya maendeleo
ya Mfuko imebuniwa ili kuiendeleza kwa ajili ya kuongeza mapato ya Mfuko.
Miradi hiyo ni Ujenzi wa Jengo la Kakakuona, Pori la Akiba Pande, Bustani ya
Wanyamapori ya Tabora, Bustani ya Wanyamapori ya Ruhila (Songea) na Kambi ya
Utalii katika Pori la Akiba Selous. Miradi hiyo iko katika hatua mbalimbali za
kuiendeleza.
9.
HITIMISHO
Utekelezaji wa majukumu ya Mfuko
hauwezi kufanikiwa bila nguvu ya pamoja na ushirikiano kutoka kwa wananchi
husasan katika kupambana na ujangili. Hivyo, wananchi wanapaswa kushiriki
kikamilifu katika ulinzi wa wanyamapori na mazingira yao kwa faida ya kizazi
cha sasa na kizazi kijacho cha watanzania.
No comments:
Post a Comment