*Watanzania watakiwa kujenga tabia ya kupima afya na kufanya mazoezi
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi, akitoa tamko la Serikali kuhusu Siku ya Ugonjwa wa Kisukari Duniani inayoadhimishwa kila mwaka Novemba 14. Kulia ni Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk.S eif Rashid.
Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Donan Mmbando, akitoa ufafanuzi wa namna ya
kujikinga na ugonjwa wa kisukari leo, jijini Dar es Salaam wakati mkutano na
waandishi wa habari.
(Picha zote na Aron Msigwa -
MAELEZO)
Na Aron Msigwa
–MAELEZO.
WATANZANIA wametakiwa kujenga
utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara, kupima afya na kuepuka tabia
hatarishi zinazochangia uwezekano wa kupata ugonjwa wa kisukari.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar
es salaam na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hussein Mwinyi wakati akitoa
tamko la Serikali kuhusu Siku ya Ugonjwa wa Kisukari Duniani inayoadhimishwa
kila mwaka Novemba 14.
Amesema Tanzania kama zilivyo nchi
nyingine inaadhimisha siku hiyo kwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa
kushirikiana na Chama cha Ugonjwa wa kisukari Tanzania kutoa elimu ya umuhimu wa
kuzuia na kujikinga na madhra mbalimbali yatokanayo na ugonjwa huo.
Amesema maadhimisho ya Siku ya
Kisukari Duniani 2013 yataongozwa na kauli mbiu isemayo “Linda Maisha yajayo
dhidi ya Ugonjwa kisukari” inayolenga kuhamasisha jamii juu ya matatizo
mbalimbali yanayotokana na ugonjwa wa kisukari katika jamii.
Ameeleza kuwa athari za ugonjwa wa
kisukari katika mwili wa binadamu hutokea wakati sukari katika damu inapokuwa
nyingi kupita kiwango cha kawaida kwa muda mrefu na kuongeza kuwa tafiti
zinaonyesha kuwa mwaka 2007 kulikua na wagonjwa milioni 246 duniani huku mwaka
2012 kukiwa na wagonjwa milioni 371 ambapo nusu ya idadi ya wagonjwa hao walikua
hawajaanza kupata matibabu.
Kuhusu dalili za ugonjwa huo Dkt.
Mwinyi amesema kuwa ni rahisi kuzitambua na huambatana na mgonjwa kuwa na kiu
isiyoisha, kukojoa mara kwa mara, kupungua uzito, kusikia njaa kila wakati na
mwili kukosa nguvu na kuongeza kuwa athari za ugonjwa huo ni kubwa kutokana na
ugonjwa huo kuharibu mishipa ya damu na fahamu, macho, figo, kusababisha upofu,
moyo na figo kushindwa kufanya kazi na miguu kufa nganzi na kuwa na
vidonda.
Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa asilimia 80
ya wagonjwa wote duniani wanaishi katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania na
kuongeza kuwa utafiti uliofanyika mwaka 2012 nchini Tanzania kwa kuzihusisha
wilaya 50 unaonyesha kuwa asilimia 9.1 ya watanzania wenye umri wa miaka 25 na
kuendelea wana ugonjwa wa kisukari.
“Ni jambo lililo wazi kuwa lazima
tubadili tabia hasa tabia hatarishi zinazochangia ugonjwa wa kisukari zikiwemo
unywaji wa pombe kupita kiasi, ulaji usiofaa, ulaji usiofaa na tabia ya kupuuza
kufanya mazoezi”, sasa Tanzania katika nchi 10 za Afrika zinazoongoza kwa
kisukari barani Afrika inashika nafasi ya 8” Amesema Dkt. Mwinyi.
Kuhusu sababu zinazochangia ugonjwa
huo Dkt. Mwinyi amesema kuwa ni pamoja na tabia ya ulaji usiofaa hasa matumizi
ya chumvi kwa wingi , mafuta na sukari, uzito uliozidi, unene uliokithiri,
kutofanya mazoezi , uvutaji wa sigara na bidhaa zitokanazo na tumbaku pamoja,
kula vyakula vyenye mafuta mengi hasa yatokanayo na wanyama, sukari nyingi,kula
chakula kupita kiasi, kukoboa nafaka, kutokula mbogamboga na matunda na unywaji
wa pombe kupita kiasi.
Ameeleza kuwa jamii inapaswa kuepuka
mambo yanayochangia chakula kilicholiwa kutotumika vizuri ikiwemo tabia ya kukaa
muda mrefu bila kufanya mazoezi huku akisisitiza kuwa unywaji wa pombe kupita
kiasi huharibu maini na kusababisha utapiamlo kwa wale wanaoishia kunywa pombe
Zaidi bila kula chakula.
“ Natoa ushauri hasa kwa watumishi
kuepuka kuketi ofisini, darasani au kuangalia runinga kwa muda mrefu na hata
kutumia lifti kwenda ghorofani badala ya ngazi na matumizi ya magari katika
umbali mfupi unaoweza kufikika kwa kutembea tu”
Dkt. Mwinyi ameleza kuwa serikali
imejipanga kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazotokana na ugonjwa huo na
kusisitiza kuwa utekelezaji wa Sera ya Afya ya mwaka 2007 unaendelea kwa
kuhakikisha kuwa utoaji wa hudunma za magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo
kisukari unafanyika kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ndani na nje ya
nchi.
Ameeleza kuwa serikali kwa kutambua
gharama za kutibu ugonjwa wa kisukari kuanzia mwaka 1983 ilitoa msamaha wa
matibabu kwa wagonjwa wote wa kisukari kutochangia gharama za matibabu pia
kuhakikisha kuwa dawa muhimu zinapatikana katika kliniki mbalimbali zilizopo
nchini.
Kwa upande wake Mganga mkuu wa
Serikali Dkt. Donan Mmbando amewataka vijana kote nchini ambao ni kundi kubwa
kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara na kuepuka maisha ya anasa
ambayo huwaweka katika hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa kisukari.
Amesema mapambano ya ugonjwa wa
kisukari yanahitaji ushiriki wa kila mwananchi hasa kuzingatia kanuni za Afya na
kujenga mazoea ya kufanya mazoezi mara mara.
No comments:
Post a Comment