TANGAZO


Thursday, October 3, 2013

Mfuko wa Bima ya Afya yaelezea Mpango wa Huduma za Matibabu kwa mama wajawazito wa Mikoa ya Mbeya na Tanga

Ofisa Mawasiliano Mwandamizi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Bw. Luhende Singu (kushoto), akieleza kwa waandishi wa habari (hawapo pichani), kuhuasu mpango wa huduma za matibabu kwa mama wajawazito na watoto kwa Mikoa ya Mbeya na Tanga, wakati wa mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) leo, Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Ofisa habari Idara ya Habari (MAELEZO) Bw. Frank Mvungi.
Ofisa Msimamizi wa Mradi huo, toka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Dk. Daudi Bunyinyiga akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani), kuhusu faida na malengo ya  mradi huo, aliyotaja kuwa ni kusaidia wanawake wajawazito na watoto wanaotoka katika familia zisizo na uwezo ambao watalipia shilingi elfu kumi (10,000) kwa mwaka ili kupunguza vifo vya akina mama wajawazito, wakati wa mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) leo, Jijini Dar es Salaam. (Picha na Eliphace Marwa-MAELEZO)
                       

1.0          UTANGULIZI:
Historia ya NHIF – Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ulianzishwa kwa Sheria Namba 8 ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuanza shughuli zake rasmi Julai 1, 2001.

2.0          UTEKELEZAJI WA MPANGO WA KFW:
Pamoja na majukumu mengine, NHIF imekuwa ikishirikiana na wadau wa ndani ya nje ya nchi katika kutekeleza miradi mbalimbali inayohusu afya.  Hivi sasa NHIF kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya watu wa Ujerumani -KFW- inaendesha mradi wa huduma za matibabu kwa Mama Wajawazito  wasio na uwezo na watoto katika mikoa ya Tanga na Mbeya. Hii ni kufuatia makubalino yaliyofanywa kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Ujerumani, ambao lengo lake ni kupunguza vifa vya mama wajawazito na watoto nchini.

3.0 HISTORIA YA MPANGO WA KFW:
Mpango huu wa miaka mitatu umeanza utekelezwa mwezi Februari mwaka 2012 na unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka 2014.
Mpango huu ambao unatekelezwa katika mikoa ya Tanga na Mbeya unawapa fursa akina mama wajawazito wasio na uwezo kupata huduma ya upimaji na matibabu bure ukilenga kupunguza vifo vya watoto wachanga na madhara mengine ambayo yanawakabili wanawake wajawazito na watoto wao wachanga ili kufikia malengo ya Milenia hususani namba 4 na 5.
4.0 SIFA ZA WANACHAMA:
Mwanachama au mnufaika wa mpango wa KFW ni mwanamke yeyote mja mzito mkazi wa mkoa wa Mbeya au Tanga, ambaye amejaza fomu ya kujiandikisha kupata huduma za vipimo na matibabu kupitia mpangp huu.


5.0 MUDA WA KUNUFAIKA NA MPANGO WA KFW:
 Mama mjamzito atanufaika na huduma za vipimo na matiba katika muda wote wa ujauzito wake na miezi mitatu baada ya kujifungua. Baada ya miezi mitatu tangu kujifungua mama wa mtoto na familia yake wanapatiwa kadi ya Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) kwa kupitia mradi huu wa NHIF/KFW ya mwaka mmoja kwa mujibu wa taratibu za matibabu za Halmashauri inayohusika.

Kadi hiyo inampa nafasi mama mwenye mtoto na familia yake (mumewe na watoto wasiozidi wanne wenye umri wa chini ya miaka kumi na nane) kupata matibabu bure katika vituo vya matibabu ndani ya Halmashauri husika.
MAFANIKIO YA MPANGO WA KFW:
Hadi sasa familia 53,253 zinapata huduma za matibabu kupitia mpango huu, kati ya lengo la familia 70,000 katika kipindi cha miaka mitatu. Lengo tarajiwa hadi kufikia tarehe 30 Septemba 2013 ilikuwa ni kusajili wanachama 40,834 ambayo ni sawa na asilimia 130 ya lengo tarajiwa.
GHARAMA ZA UTEKELEZAJI:
Tangu kuanza kwa utekelezaji wa mpango huo kiasi cha Shilingi Bilioni 2,481,700,138.40/= zimetumika ambapo kiasi cha Shilingi 1,145,367,000/= kimetumika kugharamia matibabu kwa familia za akina mama waliojiunga na mpango huu na malipo kwa ajili ya kuwapatia kadi katika Mfuko wa Afya ya Jamii – CHF.
Aidha kiasi cha Shilingi 347,204,780/= zimetumika kutoa elimu kwa umma kupitia redio, vipeperushi, magazeti na kuandaa mifumo ya taarifa.
Pia Shilingi 989,128,358.40 zimetengwa kwa ajili ya kuboresha miundombinu kwa kununua vifaa tiba kwa ajili ya vituo vya matibabu katika mkoa wa Tanga na Mbeya.
CHANGAMOTO ZA MPANGO HUU:
1.     Vituo vya kutolea huduma kuwa na upungufu wa dawa ambapo walengwa wanalazimika kutembea mwendo mrefu ili kufauta huduma katika vituo vilivyosajiliwa na NHIF.
2.     Mwitikio mdogo wa watoa huduma katika kuwasilisha madai yao baada ya kutoa huduma kwa kundi hili maalumu,

HITIMISHO:
NHIF inatarajia kuwa mpango huu utasadia kupunguza changamoto zinazoikabili sekta ya afya hapa nchini katika kuhudumia wakina mama wajawazito na kuwaweka katika mazingira salama ya kujifungua na kuwapa uhakika wa huduma za matibabu, wao na watoto wao baada ya kujifungua.

 Kauli mbiu yetu ni “Afya Bora Ndiyo Mambo Yote.” 

No comments:

Post a Comment