TANGAZO


Wednesday, October 16, 2013

Maelfu watoroka ghasia Afrika ya Kati



Waasi wa Seleka wanasemekana kuzua rabsha upya katika maeneo ya Magharibi mwa nchi
Shirika la misaada la Medecins Sans Frontieres (MSF), limesema kuwa maelfu ya watu wamelazimika kutoroka makwao katika Jamuhuri ya Afrika ya Kati kutokana na ghasia zilizoibuka upya.
Nchi hiyo yenye utajiri wa madini, imekuwa ikikumbwa na misukosuko, tangu waasi kumng'oa mamlakani Rais Francois Bozize mnamo mwezi Machi.
Serikali ya Ufaransa wiki hii ilisema kuwa itatuma wanajeshi wa ziada nchini humo katika juhudi zake za kumaliza mgogoro nchini humo.
Wafanyakazi wa afya kutoka katika shirika hilo, wanasema kuwa wanashuhudia visa vya mauaji nchini humo.
Wanawake na watoto ni miongoni mwa watu waliothirika zaidi na ambao wanatibiwa kwa majeraha ya risasi , panga na silaha zengine za kijadi magharibi mwa nchi.
Wafanyakazi wa mashirika ya misaada pia wamekuwa wakishambuliwa.
Vijiji vyote vimeteketezwa na shirika hilo limesema kuwa limepokea visa vya mashambulizi yanayotokana na migawanyiko ya kidini.
Mapigano kati ya makundi ya kutoa ulinzi kwa wanakijiji pamoja na waasi wa zamani yamewalazimisha maelfu kutoroka makwao huku shirika hilo likisema kuwa hali ya kibinadamu sasa ni ya kusikitisha sana na inahitaji kushughulikiwa kwa dharura.

No comments:

Post a Comment