Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama awaongoza waombolezaji kwenye mazishi
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, (katikati), Kamanda wa Polisi mkoani
Kilimanjaro, Robert Boaz (kulia) na Kaimu Kamanda, Mkoa wa Kilimanjaro, Koka
Moita wakiwa katika ibada ya maziko ya aliyekuwa Kamanda wa Usalama Barabarani,
James Kombe, iliyofanyika leo, nyumbani kwake Msae, Mwika, mkoani
Kilimanjaro. (Picha na Amina Mbwambo)
Na Amina Mbwambo, Moshi
MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama,
leo amewaongoza maelfu ya waombolezaji katika mazishi ya aliyekuwa Mkuu wa
Kitengo cha Usalama Barabarani, Kamishna mstaafu, James Kombe (63),
aliyefariki dunia October 21, mwaka huu katika Hospitali ya Ocean Road, jijini
Dar es Salaam baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Kombe aliyeitumikia
Jeshi la Polisi kwa muda wa miaka 24, katika
nyadhifa mbalimbali, alizikwa
jana saa 9:40, alasiri, Nyumbani kwake katika kijiji cha Msae, Kata ya Mwika,
Jimbo la Vunjo, Wilaya ya Moshi Vijijini, mkoani Kilimanjaro, baada ya ibada
ya maziko iliyofanyika katika Usharika wa Msae-Lyakrima na kuongozwa na
Askofu Mkuu wa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini, Dk. Martin
Shao.
Akitoa Salamu za Rambirambi, Gama alisema serikali imeguswa na
msiba huo huku akimuelezea Marehemu Kombe kama mtu muadilifu, mwaminifu
na mtu asiyekuwa na ubinafsi na mzalendo aliyeitumikia
Taifa lake kwa nguvu zake zote hadi dakika za mwisho za uhai wake.
“Ni
kweli mazingira yetu kikazi yanatofautiana, lakini ni wazi kuwa kuna mengi ya
kujifunza na kujivunia kutoka kwa Kamishna Kombe enzi za uhai wake, Marehemu
ameacha historia iliyotukuka nyuma yake, alikuwa ni mtu mwadilifu sana,
mwaminifu, mzalendo na mchapa kazi aliyejitoleakulitumikia Jeshi la Polisi na
Taifa kwa ujumla,” alisema Gama.
Kuhusu swala la uwajibikaji na
utendaji kazi, Gama alisema wananchi wengi kwa sasa wanashindwa kufanya kazi
za maendeleo hasa mkoani Kilimanjaro katika maeneo ya Rombo, Marangu na Mwika
kutokana na kukithiri kwa vitendo vya Unywaji pombe holela ambapo aliagiza
wakuu wa Wilaya kuhakikisha wanasimamia na kudhibiti hali hiyo.
Awali
akiongoza ibada ya Maziko, Askofu Mkuu wa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini, Dk.
Martin Shao, aliwataka waumini wa dini ya Kikristo, wananchi pamoja na
watumishi katika Jeshi la Polisi kufanya yale yaliomema ikiwa kweli wanataka
kuenziwa kama ilivyo kwa marehemu Kombe.
Dk. Shao katika ibada hiyo,
alimuelezea marehemu Kombe kama mtu anayestahili kuenziwa daima kama
anavyoenziwa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kutoka na
utendaji wake kazi uliotukuka, uzalendo na Uadilifu pamoja na uwajibikaji
katika kuhakikisha Amani ya Tanzania na usalama wa Wananchi
wake.
Kabla ya kifo chake, Kamishna Kombe, alikuwa anasumbuliwa na
ugonjwa wa Kansa ambao ulianza kumsumbua Juni mwaka jana na
kutibiwa katika Hospitali ya Rufaa KCMC, mjini Moshi.
James Kombe,
aliyezaliwa mwaka 1950, mwika Kilimanjaro ameacha mjane mmoja, Maria Kombe na
watoto watano na kwamba alilitumikia Jeshi la polisi kuanzia Machi, mwaka
1970 na kulitumikia mpaka alipostaafu mwaka 2010.
Akisoma historia ya
Marehemu, Kamanda wa kikosi cha usalama
Barabarani, Joseph Mwakabonga alisema
Kamishna Kombe, alijiunga na Mafunzo ya awali machi 23 mwaka 70 na kumaliza
Agosti 28 mwaka huo, huko Mopshi baada ya kuhitimu elimu ya Sekondari mwaka
1969 nchini Uganda.
Alisema alipandishwa vyeo kama Mkaguzi wa polisi
(1977), Kamishna msaidizi (1995), Mkaguzi wa Polisi (1986), Mrakibu
Mwandamizi (1991) na Kamishna Msaidizi wa Polisi (2002) hadi alipostaafu
2010.
No comments:
Post a Comment