*Wananchi watakiwa kuendeleza ushirika kwa kujiunga na vikundi vya Maendeleo katika maeneo yao
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na Uwezeshaji Dkt. Mary Nagu (kulia), akimkabidhi nyaraka za Utendaji kazi Mwenyekiti wa Baraza jipya la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Omari Issa wakati wa uzinduzi wa baraza hilo leo jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Baraza jipya la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Omari Issa akizungumza na Wajumbe wa baraza hilo, mara baada ya uzinduzi wake leo, jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji Dkt. Mary Nagu (katikati), akizungumza jambo na Mwenyekiti wa Baraza jipya la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Omari Issa (kushoto) na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dk. Anacleti Kashuliza leo, jijini Dar es Salaam.
Wajumbe na Viongozi wa Baraza jipya la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Wakiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Nchi , Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na Uwezeshaji Dkt. Mary Nagu. (Picha na Aron Msigwa - MAELEZO)
Na Aron Msigwa –MAELEZO, Dar es salaam.
SERIKALI imesema kuwa itaendelea kuunga mkono juhudi za uzalishaji mali zinazofanywa na wananchi waliojiunga katika vikundi mbalimbali vya uzalishaji mali katika maeneo mbalimbali nchini.
Kauli hiyo, imetolewa leo, jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi , Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na Uwezeshaji Dkt. Mary Nagu wakati akizindua Baraza jipya la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ..
Amesema kuwa serikali inatambua na inaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na wananchi katika kujiletea maendeleo kupitia ushiriki walio nao katika vikundi mbalimbali walivyovianzisha katika maeneo yao na kufafanua kuwa serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu inaendelea kuunga mkono juhudi hizo kwa kuanzisha Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi.
Dkt. Nagu amesema Baraza hilo lina jukumu kubwa ya kusimamia na kuratibu utekelezaji wa sera ya Taifa ya Uwezeshaji wananchi kiuchumi ya mwaka 2004 na kufafanuam kuwa utekelezaji wa mikakati na malengo ya Dira ya maendeleo ya mwaka 2025 ya kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati itaweza kufikiwa iwapo watanzania watashiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Ameongeza kuwa Baraza hilo lina jukumu la kuwaelimisha wananchi kuhusu tafsiri ya uwezeshaji Wananchi kiuchumi ambayo kwa muda mrefu imekua ikipotoshwa na kusisitiza kuwa dhana ya uwezeshaji sio kupitia mitaji pekee bali ni kujenga uwezo wa wananchi kuweza kuziona fursa zinazowazunguka na kuweza kuzitumia kwa maendeleo yao.
“ Nchi zinazoweza kuendelea ni zile ambazo zimejenga uwezo kwenye ushirika, lazima tujenge uwezo wa vikundi vyetu ili tuweze kugundua wapi tunakwama na kutatua changamoto zilizopo ili tupige hatua maana uwezeshaji sio kupitia mitaji au kupewa mkopo maana kuna watu tayari wana mitaji lakini hawawezi kufanya kitu hao tunachokifanya tunawajengea uwezo” Amesisitiza Dkt. Nagu.
Ameeleza kuwa ipo haja kwa vikundi mbalimbali vilivyojiunga katika ushirika kuendelea kujenga uwezo ili viweze kufanya makubwa na kuaminiwa na wadau mbalimbali pamoja na serikali huku akitoa mfano wa uamuzi wa serikali kununua samani zinazotengenezwa na watanzania.
Dkt. Nagu amesema kuwa serikali imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya uboreshaji wa miundombinu inayolenga kuwawezesha wananchi kiuchumi ikiwemo huduma za afya na elimu na kuwataka wajumbe wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kuweka umuhimu katika maeneo yatakayoleta matokeo ya haraka na yanayogusa maisha ya wananchi wengi hususan kwenye kilimo, Ufugaji, Uvuvi, Misitu,Ufugaji Nyuki na Utalii.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza hilo Bw. Omari Issa akizungumza mara baada ya kuzinduliwa kwa baraza hilo amesema baraza hilo litaendelea kuwajengea uwezo wananchi kuzitumia fursa zinazowazunguka kujiletea maendeleo.
Amesema baraza litaendelea kutoa elimu kwa wananchi kwa kuwahamasisha kujenga uwezo katika vikundi vya ushirika ili waweze kumiliki uchumi wa nchi huku akifafanua kuwa wananchi walio wengi wanahitaji elimu kuhusu dhana ya uwezeshaji Kiuchumi na namna ya kutumia fursa na mikopo wanayopata kutoka katika taasisi mbalimbali za fedha kupata faida .
Baraza hilo lenye wajumbe 9 litadumu kwa miaka 3 huku likiwa na jukumu la kuhakikisha linawasaidia wananchi kumiliki na kunufaika na fursa za kiuchumi zilizopo nchini.
No comments:
Post a Comment