Mshukiwa wa ugaidi aliyekamatwa na wanajeshi wa Marekani nchini
Libya mapema mwezi huu wakati wa operesheni ya jeshi hilo mjini Tripoli,
amefikishwa mahakamani kwa mara ya pili mjini New York.
Abu Anas al-Liby anayeshukiwa kuwa mmoja wa viongozi wa kundi la kigaidi la
Al Qaeeda aliwakilishwa na wakili wa serikali ya Libya.Hata hivyo amekanusha madai dhidi yake.
Bwana Liby, mwenye umri wa miaka 49, ambaye jina lake halisi ni Nazih Abdul-Hamed al-Ruqai, alifikishwa mahakamani kujadili kuhusu mawakili wake.
Wakati wa kwanza kwa Liby kufikishwa mahakamani, aliwakilishwa na mawakili walioteuliwa na mahakama baada ya kusema kuwa hangeweza kumudu gharama ya mawakili wake.
Hata hivyo inaarifiwa baadaye serikali ya Libya ilimwajiri wakili kuweza kumwakilisha Liby.
Wakili huyo, Bernard Kleinman, alisema kuwa itachukua muda wa miezi kadhaa kudurusu stakabadhi nyingi kabla ya kesi hiyo kuanza rasmi.
Pia alisema sharti Liby arejeshewe Quran yake iliyochukuliwa na wanajeshi hao wakati wa kukamatwa kwake.
Alisema kuwa anawakilisha mshukiwa mmoja anayezuiliwa katika jela la Guantanamo Bay,nchini Cuba.
Bwana Liby anatarajiwa kurejea tena mahakamani tarehe 12 Disemba.
Kumekuwa na ghadhabu nchini Libya kufuatia kukamatwa kwa Al Liby na wanajeshi wa Marekani baadhi wakidai kuwa serikali ya Libya ilihusika.
No comments:
Post a Comment