Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma (kulia), akipongezwa na Sheikhe Mkuu wa Waislam mkoani Iringa, Juma Alli Tagalile kwa kuwafuturisha waumini wa dini ya Kiislam jana. (Picha na Francis Godwin Blog)
Na Francis Godwin, Iringa
MKUU wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma amewataka viongozi wa dini ya Kiislam mkoani Iringa pamoja na viongozi wa dini nyingine zote kuendelea kushirikiana na Serikali ya Awamu ya nne, chini ya Rais Dk. Jakaya Kikwete kudumisha amani na utulivu .
Dk. Ishengoma ametoa rai hiyo jana katika viwanja vya Ikulu ndogo mjini Iringa, wakati akiwafuturisha waumini wa dini ya Kiislam mkoani Iringa wanaoendelea na mfungo wa mwezi mtukufu wa ramadhan.
Pamoja na kuwapongeza waumini hao wa dini ya Kiislam kwa kuendelea na mfungo wa mwezi mtukufu wa ramadhan ila bado amewataka kuendelea na mfungo huo huku wakijikita katika maombi ya kuliombea Taifa la Tanzania na mkoa wa Iringa ili usiingie katika machafuko yatakayosababishwa na uvunjifu wa amani .
" Kwanza nawapongeza sana ndugu zangu waumini wa dini ya Kiislam kwa kuingia katika mfungo wa ramadhani na kuendelea na mfunngo huo ....ila nawaombeni tushirikiane katika kudumisha amani na utulivu katika mkoa wetu wa Iringa na iwapo Iringa ikahubiri amani na mikoa mingine itaiga mfano wa Iringa na kuja kujifunza kwetu"
Alisema kuwa moja kati ya mafanikio katika Taifa ni pale ambapo nchi inaendelea kuwa na amani jambo litakalomfanya Rais wetu Dr Jakaya Kikwete kuendelea vema na mikakati ya kimaendeleo kama anavyoendelea kulitumikia Taifa .
Aidha aliwataka waumini wa dini ya Kiislam mkoa wa Iringa kuendelea na ushirikiano na kuwa ofisi yake itaendelea kuwa karibu na dini zote bila ubaguzi na kuwa kama alivyoanza mwaka jana ataendelea kuwafuturisha waumini hao wa dini ya Kiislam kila mwaka .
Mbali ya kutoa ahadi hiyo ya kuendelea kutoa futari kwa waumini hao wa dini ya Kiislam mkoani Iringa bado aliwataka kwa wakati mwingine atakapowaalika basi kukumbuka kufika na wake zao hata kama ni zaidi ya mmoja wanapaswa kufika pamoja kushiriki futari hiyo.
Kwa upande wake Shekhe mkuu wa waislam mkoa wa Iringa Juma Tagalile alimpongeza mkuu huyo wa mkoa kwa kuwakumbuka waumini wa dini ya Kiislam na hata kuamua kuandaa futari hiyo .
Pia alisema kwa upande wao wataendelea kutoa ushirikiano kwa serikali katika kudumisha amani na utulivu nchini.
Awali MC wa sherehe hiyo katibu tarafa ya Iringa mjini Twaha Kimbama alisema kuwa mbali ya waumini hao wa dini ya Kiislam kualikwa pia mkuu huyo wa mkoa alialika watu mbali mbali wakiwemo viongozi wa dini ya Kikristo mjini Iringa ambao hawakupata kutokea hata mmoja tofauti na mwaka jana ambapo wengi wao walipata kushiriki.
No comments:
Post a Comment