TANGAZO


Tuesday, August 6, 2013

BOHARI KUU YA DAWA (MSD) yaeleza kuhusu Utendaji na Majukumu yake kwa jamii

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Isaya Mzoro, akieleza kwa vyombo vya habari kuhusu utendaji na mipango ya bohari hiyo katika mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara ya Habari leo, Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari, Zamaradi Kawawa. (Picha na Hassan Silayo- Maelezo)

Bohari ya Dawa (MSD) ni mojawapo ya Idara chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, inayojiendesha chini ya Bodi ya Wadhamini iliyoundwa kwa mujibu wa sheria namba 13 ya mwaka 1993.
Bohari ya Dawa yenye makao yake makuu mjini DSM, eneo la Keko Mwanga, Barabara ya Nyerere  ina jumla ya kanda tisa katika mikoa ya Mwanza, Tabora, Mbeya, Iringa, Dodoma Tanga, Moshi, Mtwara na Dar Es Salaam
i.                    MAJUKUMU YA MSD
Majukumu ya msingi ya Bohari ya Dawa yako matatu, ambayo ni Kununua, Kuhifadhi  na Kusambaza  dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara  kwenye hospitali, vituo vya afya, zahanati za umma, na taasisi zilizoidhinishwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
ii.                  UTENDAJI
Utendaji wa MSD unaongozwa na Sera ya Afya  ya mwaka 2007 na Mpango Mkakati wa Kati wa miaka Mitano ( 2007  -2013). Lengo kuu la mpango mkakati huu ni kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwenye mnyororo mzima wa ugavi nchini.
iii.                UPATIKANAJI WA DAWA
Upatikanaji wa dawa kwa Bohari ya Dawa umekuwa unaongezeka (kulingana na bajeti ya serikali) mwaka hadi mwaka.Tafiti zilizofanywa mwaka 2010-2011 na wadau mbali mbali (wakiwemo GIZ na USAID) zimeonyesha kuwa hali ya upatikanaji wa dawa katika hospitali za umma umeongezeka na kufikia kati ya asilimia 70 hadi 75.
Bohari hununua dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara  kwa ajili ya vituo vya kutolea huduma ya afya kutoka vyanzo mbalimbali ndani na nje ya nchi. Hata hivyo asilimia 80 ya dawa huagizwa kutoka nje ya nchi huku asilimia 95 ya vifaa tiba huagizwa kutoka nje ya nchi. Vitendanishi vya maabara kwa asilimia 100 huagizwa kutoka nje ya nchi.
Bohari ya Dawa hununua dawa na vifaa tiba kwa kuzingatia miongozo ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii. Miongozo hiyo pamoja na mambo mengine inaelekeza kuwa Dawa, Vifaa na Vifaa Tiba vyote lazima visajiliwe TFDA na PHLB kabla ya kuagizwa na kusambazwa. Dawa, Vifaa na Vifaa Tiba hukaguliwa na wakala hizo. Aidha ubora wake hupimwa na kukaguliwa kwa ushirikiano wa taasisi za serikali kama vile TBS, GCLA na BICO(UDSM)
Bohari ya Dawa pia hununua dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara kwa kuzingatia  sheria ya Manunuzi ya Umma.
iv.                 UHIFADHI
Mahitaji halisi ya maghala kwa MSD ni mita za mraba 60,000. Katika kipindi cha nyuma MSD ilikuwa na maghala yenye uwezo wa mita za mraba 20,845 ambayo ilikuwa inayamiliki yenyewe na maghala ya kukodi yenye ukubwa wa mita za mraba 24,443.
Kwa sasa maghala mapya ya kisasa yenye ukubwa wa mita za mraba 10,000 ambayo yamejengwa kwa msaada wa pamoja kati ya Shirika la misaada la Kimataifa la serikali ya Marekani (USAID) na Mfuko wa Kimataifa wa Kupambana na UKIMWI, Malaria na Kifua Kikuu (GFATM)pamoja na Global Fund yamekamilika katika kanda za  Dar es Salaam, Dodoma na Mbeya. Mwishoni mwa mwaka jana ghala la Keko lilizinduliwa, mwaka huu mwezi Mei ghala la Dodoma lilizinduliwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Ujenzi wa maghala mengine ya kisasa yenye ukubwa wa mita za mraba 8,000 unaendelea katika kanda za Tabora na Tanga na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu ( Agosti, 2013).
v.                   USAMBAZAJI DAWA NA VIFAA TIBA
Tangu mwaka 2010 MSD imekuwa ikipeleka dawa moja kwa moja hadi katika hospitali, vituo vya afya na zahanati kwa mikoa Kumi. Hatua hii ilitokana na maagizo ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, katika jaribio la kwanza la kupeleka dawa na vifaa tiba moja kwa moja hadi vituo vya kutolea huduma za tiba katika kanda ya Tanga.

 Jaribio hilo lilifanikiwa kwa kiasi kikubwa ambapo mnamo mwaka 2011/2012 mikoa mingine tisa ikaingizwa katika utaratibu wa kufikisha Dawa na Vifaa Tiba moja kwa moja hadi hospitali, vituo vya Afya na zahanati. Mikoa hiyo ni pamoja na Shinyanga, Lindi, Dodoma, Kigoma, Manyara, Dar es salaam, Rukwa, Pwani na Ruvuma

Katika mwaka huu wa fedha MSD inaendeleza mpango huo wa kupeleka dawa moja kwa moja hadi vituo vya kutolea huduma za afya katika mikoa mikoa 15 iliyokuwa imebaki.

vi.                 MABORESHO
a.       Bohari ya Dawa kwa kushirikiana na wahisani ina mpango wa kupanua maghala kwa kukamilisha ujenzi wa awamu ya pili ili kuongeza nafasi za kuhifadhia Dawa na Vifaa Tiba. Tayari maghala ya kisasa yaliyokamilika yameanza shughuli za kuhidadhi Dawa na Vifaa tiba.
b.      MSD  inatumia mfumo wa EPICOR 9 tangu mwezi Agosti, 2012. Wafanyakazi katika ngazi zote wanapatiwa mafunzo endelevu katika utoaji huduma kwa haraka na ufanisi.
c.       Kuongea na Taasisi shiriki katika Mnyororo wa ugavi(TFDA & TBS na TRA)  ili kupunguza muda wa kugomboa bidhaa

vii.               CHANGAMOTO
a.       Ongezeko kubwa la Mahitaji kulinganisha na uwezo wa Serikali.
b.      Ucheleweshaji wa kufikishwa pesa MSD kutoka Hazina.
c.       Halmashauri kutokutumia vyanzo vingine vya fedha (NHIF, CHF, Basket Fund, Cost Sharing) kununua dawa na kutegemea fedha za Serikali kuu(kupitia MSD) tu.
d.      Uhaba wa viwanda vya dawa nchini
e.      Taratibu za ununuzi kuchukua muda mrefu (miezi 6 - 9). (Ununuzi wa dawa unafuata taratibu zinazotakiwa kufuatwa na bidhaa nyingine za kawaida, hazina utofauti wa taratibu wala kipaumbele)
f.        Baadhi ya Zahanati na Vituo vya Afya kutoleta Maombi ya Dawa na vifaa tiba katika Kanda za MSD (Kama utaratibu unavyoelekeza)

viii.             MATARAJIO
a.       Kushirikisha sekta binafsi katika kusambaza dawa na vifaa tiba.
b.      Kubandika orodha ya dawa na vifaa tiba vilivyokabidhiwa kituoni mara tu baada ya kukabidhi.
c.       Kuendelea kuweka nembo ya GOT kwenye vidonge ili kuzitambua dawa ambazo ni mali ya umma.
d.      Kushirikisha sekta binafsi katika kutoa huduma ya dawa na vifaa tiba wakati MSD haina bidhaa hizo kwenye maghala yake.
e.      Kuendelea kuwahimiza waganga wafawidhi wa vituo vya kutolea huduma kutayarisha na kuleta Maombi ya Dawa na Vifaa Tiba kwa wakati uliopangwa.
Isaya Mzoro
Kny: Kaimu Mkurugenzi Mkuu - MSD


No comments:

Post a Comment