Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akifuatana na Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Dk. Ad Koekkoek, alipofika Ikulu, Mjini Zanzibar, kumuaga Rais, baada kwa kumaliza muda wake wa kazi nchini leo asubuhi.
Na Said Ameir, Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameishukuru Serikali na wananchi wa Uholanzi kwa misaada yake ambayo imekuwa ikiitoa kwa Zanzibar.
Dk. Shein ametoa shukrani hizo leo, wakati alipokuwa akizungumza na Balozi wa Uholanzi nchini Bwana Ad Koekkokek ambaye alikwenda Ikulu kumuaga baada ya kipindi chake cha kuitumikia nchi yake nchini Tanzania kumalizika.
Dk. Shein ametaja miongoni mwa misaada hiyo ni wa kuimarishaji Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja ili kuifanya kuwa ya Rufaa ambapo itaiwezesha kutoa huduma zote zinazotakiwa kwa wagonjwa wanaopewa rufaa katika hospitali hiyo.
Mapema mwaka huu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Uholanzi zilitiliana saini mkataba wa awamu ya pili ya msaada wa kuimarisha hospitali hiyo ambao utagharimu jumla ya Euro milioni 9.6.
Chini ya mkataba wa msaada huo Serikali ya Uholanzi itatoa asilimia 50 ya gharama wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itachagia asilimia 50 iliyobaki. Fedha hizo pamoja na mambo mengine zitatumika katika kuimarisha miundombinu ya hospitali hiyo pamoja na kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto. Kabla ya hapo Serikali ya Uholanzi iligharimia awamu ya kwanza ya utayarishaji mradi huo.
Dk. Shein ameuelezea uhusiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Uholanzi kuwa wa manufaa kwa nchi hizo na kueleza kuwa misaada ambayo nchi hiyo imekuwa ikizipatia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikiwasaidia watanzania kupambana na changamoto za kimaendeleo.
“Uholanzi imekuwa ikizisaidia serikali zetu kuendeleza na kuimarisha sekta mbalimbali za maendeleo ikiwemo ya nishati, miundombinu, afya na elimu” Dk. Shein alimueleza Balozi huyo.
Dk. Shein alimueleza Balozi Ak Koekkoek kuwa Serikali na wananchi wa Zanzibar wameridhishwa na ushirikiano mzuri kati ya nchi yao na Uholanzi wakati wote Balozi huyo alipokuwepo nchini na ameeleza matumaini yake kuwa ushirikiano huo utaimarika zaidi kwa kuangalia maeneo mengine zaidi ya ushirikiano.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumtakia Balozi Ak Koekkoek kila la heri katika katika nafasi yake mpya ya kuitumikia nchi yake na kumueleza kuwa milango iko wazi kuitembelea Zanzibar na Tanzania kadri atakapopata nafasi.
Kwa upande wake Balozi Ak Koekkoek alimueleza Rais wa Zanzibar kuwa anaamini kuwa aliweza kutimiza majukumu yake ipasavyo wakati wote alipokuwa akiitumikia nchi yake nchini Tanzania.
“wajibu wangu ilikuwa ni kujenga mazingira mazuri ya kuziwezesha nchi zetu ziwe na mahusiano mazuri na ya karibu wakati wote. Nadhani hili nimeweza kulifanya na naamini uhusiano wa nchi zetu umezidi kuimarika”alieleza Balozi Ak Koekkoek.
Aliongeza kuwa anaondoka Tanzania akiwa na kumbukumbu nzuri ya ushirikiano aliopata kutoka kwa Serikali na watu wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla wakati wote wa utumishi wake humu nchini.
Balozi huyo alimkabidhi nakala mbili za kitabu cha kumbukumbu ya historia ya Zanzibar kiitwacho Kasri ya Mtoni, Sultani na Binti Sultani wa Zanzibar kilichochapishwa kwa msaada wa Wizara ya Misaada ya Kimataifa ya Nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment