Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa
I.
UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa
Spika, naomba kutoa hoja
kwamba Bunge lako Tukufu lijadili na kupitisha makadirio ya mapato na matumizi
ya Serikali kwa mwaka 2013/14. Pamoja na hotuba hii, vimeandaliwa vitabu vinne
vya Bajeti vinavyoelezea takwimu mbalimbali za Bajeti. Kitabu cha Kwanza kinahusu makisio ya mapato;
Kitabu cha Pili kinaelezea makisio
ya matumizi ya kawaida kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala wa
Serikali; Kitabu cha Tatu kinahusu
makisio ya matumizi ya kawaida kwa Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa; na
Kitabu cha Nne kinaainisha makadirio
ya matumizi ya maendeleo kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala
za Serikali, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa
mwaka 2013 ambao ni sehemu ya bajeti hii.
2.
Mheshimiwa
Spika, awali ya yote
ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kushiriki
mkutano wa nane wa Bunge la Kumi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha
namshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete kwa uongozi wake thabiti. Vilevile, napenda kutumia fursa hii
kukushukuru wewe Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Wenyeviti wa vikao vya Bunge
kwa kuongoza majadiliano vizuri bungeni.
3.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mapendekezo
ya Bunge ya mzunguko mpya wa bajeti, Serikali imeridhia mapendekezo hayo ambayo
yanatoa fursa ya kushirikisha wadau wengi zaidi na kuwezesha utekelezaji wa
bajeti kuanza tarehe 1 Julai kila mwaka. Serikali imetekeleza mapendekezo hayo
kwa kurekebisha muda na utaratibu wa hatua za uandaaji wa bajeti ambazo zimezingatiwa
wakati wa maandalizi ya bajeti ya mwaka 2013/14.
4.
Mheshimiwa Spika, kutokana na mabadiliko hayo, Serikali itakuwa
inatayarisha Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti mwezi Agosti hadi Oktoba kila
mwaka; kuidhinisha na kusambaza Mwongozo mwezi Novemba; kuandaa rasimu za
mipango na bajeti za mafungu mwezi Novemba hadi Januari; kufanya uchambuzi wa
rasimu za Bajeti na kuingiza takwimu kwenye mfumo wa IFMS Mwezi Februari; kuwasilisha
rasimu za Bajeti pamoja na randama kwenye Kamati za Bunge za Kisekta mwezi
Machi; kuchapisha na kuwasilisha Bungeni vitabu vya bajeti mwezi Aprili;
kuchambua na kuidhinisha bajeti Bungeni mwezi Aprili hadi Juni; na kufanya
ufuatiliaji na tathmini ya shughuli zilizoidhinishwa muda wote wa utekelezaji
wa bajeti.
5.
Mheshimiwa
Spika, kufuatia
mabadiliko hayo, Wizara zote zinatakiwa kuwasilisha makadirio ya mapato na
matumizi ya fedha na kuhitimishwa na hotuba hii ya bajeti ya Serikali.
6.
Mheshimiwa
Spika, Ninazishukuru
Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala za Serikali, Mikoa na Mamlaka
za Serikali za Mitaa na wadau mbalimbali walioshiriki kufanikisha matayarisho ya
bajeti hii. Kwa namna ya pekee, ninaishukuru Kamati ya Bunge ya Bajeti
ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Andrew John Chenge, Mbunge wa Bariadi
Magharibi kwa kuchambua kwa kina bajeti za mafungu yote na kutoa mapendekezo. Aidha,
naishukuru Kamati Maalum ya Mheshimiwa Spika kuhusu mapendekezo ya mapato ya
Serikali; Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara inayoongozwa na
Mhe. Mahmoud Hassan Mgimwa (Mb) na Waheshimiwa Wajumbe wengine wa Kamati hiyo pamoja
na Wenyeviti wa Kamati nyingine za kisekta kwa ushauri, mapendekezo na
maelekezo wakati wakichambua Bajeti hii. Vilevile, ninawashukuru Waheshimiwa
Wabunge wote kwa ushauri na mapendekezo yao ambayo yamesaidia kuboresha Bajeti
hii.
7.
Mheshimiwa
Spika, ninampongeza kwa
dhati Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb), kwa hotuba yake
ambayo imefanya majumuisho ya mapitio ya utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2012/13
na kutoa mwelekeo wa shughuli za Serikali kwa mwaka 2013/14. Aidha, ninamshukuru
Mhe. Stephen Masatu Wasira (Mb), Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu
kwa kuwasilisha Taarifa ya Hali ya Uchumi ya mwaka 2012 na Mpango wa Maendeleo
wa mwaka 2013/14. Vilevile, ninawapongeza Mawaziri wenzangu kwa kuwasilisha hotuba
za bajeti za wizara zao ambazo zimejumuishwa katika Bajeti hii.
8.
Mheshimiwa
Spika, ninawashukuru
Naibu Mawaziri wa Fedha, Mhe. Janet Zebedayo Mbene (Mb) na Mhe. Saada Mkuya
Salum (Mb), Katibu Mkuu; Naibu Makatibu Wakuu; Gavana wa Benki Kuu; Kamishna
Mkuu wa Mamlaka ya Mapato; Mkurugenzi
Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu; Viongozi wakuu wa taasisi zilizo chini ya
Wizara; wakuu wa idara na vitengo pamoja na watumishi wa Wizara ya Fedha na
taasisi zake kwa michango yao katika maandalizi ya Bajeti hii. Ninamshukuru pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali
kwa kutayarisha kwa wakati Muswada wa Fedha wa mwaka 2013 na nyaraka mbalimbali
za sheria ambazo ni sehemu ya Bajeti hii. Aidha, ninamshukuru Mpiga Chapa Mkuu
wa Serikali kwa kuchapisha nyaraka zote za Bajeti kwa wakati.
9.
Mheshimiwa
Spika, Bajeti ya mwaka
2013/14 ni ya tatu katika utekelezaji wa Mpango wa kwanza wa Maendeleo wa Miaka
Mitano; Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2010; na Awamu ya Pili ya
Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUKUTA II). Aidha, Bajeti hii
inaendelea kutekeleza Malengo ya Maendeleo ya Milenia 2015. Madhumuni ya mipango na mikakati hii ni kufikia
malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. Vilevile, Bajeti hii inalenga
kufungua fursa za kiuchumi na kijamii kwa ajili ya maendeleo endelevu kupitia
mfumo mpya wa utekelezaji wa miradi ya kipaumbele ambayo italeta matokeo
makubwa kwa haraka.
10.
Mheshimiwa
Spika, kama ilivyoelezwa
katika hotuba iliyowasilishwa na Mhe. Stephen Masatu Wasira (Mb), kuhusu utaratibu
mpya wa uibuaji wa vipaumbele vya Taifa ambavyo vitaleta matokeo makubwa na ya
haraka (Big Results Now –BRN), Bajeti
ya mwaka 2013/14, imedhamiria kutekeleza maeneo makuu sita yaliyobainishwa kama
vipaumbele vya kitaifa. Maeneo hayo ni maji, nishati, uchukuzi, kilimo, elimu
na kuongeza mapato.
11.
Mheshimiwa
Spika, baada ya maelezo
hayo ya awali, naomba sasa kutoa taarifa kuhusu mapitio ya utekelezaji wa
bajeti ya mwaka 2012/13, na mwelekeo wa makadirio ya mapato na matumizi kwa
kipindi cha mwaka 2013/14.
II.
MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA SERA ZA BAJETI YA MWAKA 2012/13
12.
Mheshimiwa
Spika, shabaha na malengo
ya Bajeti ya mwaka 2012/13 yalijikita katika kukuza Pato halisi la Taifa kwa
asilimia 6.8 mwaka 2012; kuongeza mapato ya ndani kufikia uwiano na Pato la
Taifa wa asilimia 18.0; kudhibiti mfumuko wa bei na hatimaye kuurudisha kwenye kiwango
cha tarakimu moja; kuimarisha kiwango cha ubadilishaji wa fedha kitakachotokana
na mwenendo wa soko la fedha pamoja na kuongeza mikopo kwa sekta binafsi kwa
asilimia 20 ya Pato la Taifa.
13.
Mheshimiwa
Spika, maeneo mengine yaliyozingatiwa
katika misingi na shabaha ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2012/13 yalikuwa:
kuwepo kwa nishati ya umeme wa uhakika na kuhamasisha matumizi ya gesi asilia;
kuimarika kwa utekelezaji wa Sera za Fedha na Bajeti; kuimarika kwa mahusiano
na Washirika wa Maendeleo; kutekeleza maboresho katika sekta ya umma ikiwa ni
pamoja na kuendelea kuimarika kwa usimamizi wa fedha za umma; kuboresha
mazingira ya biashara pamoja na kuongezeka kwa tija na fursa za uwekezaji;
kulinda na kudumisha mafanikio yaliyopatikana katika Sekta za huduma za jamii;
kuimarisha utawala bora na uwajibikaji; na kuimarisha utaratibu wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP).
Sera za Mapato
14.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka
2012/13, Sera za mapato zilizotekelezwa na Serikali zililenga kuongeza mapato
ya ndani yatokanayo na kodi na yasiyo ya kodi ili kuimarisha uwezo wa Serikali
wa kutoa huduma kwa umma na kupunguza utegemezi wa bajeti. Sera zilizotekelezwa
zililenga katika kuimarisha taratibu za kukadiria na kukusanya mapato;
kuboresha sheria za kodi; kuongeza matumizi ya kielektroniki katika kukusanya
kodi; kupunguza misamaha ya kodi; na kuwianisha viwango vya kodi na tozo.
15.
Mheshimiwa
Spika, itakumbukwa
kwamba katika mwaka wa fedha 2012/13, Bunge lilipitisha sera mbalimbali za kodi
ambazo zimetekelezwa na Serikali. Azma ya sera hizo ilikuwa ni kuimarisha
ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kupanua wigo wa kodi, kuimarisha taratibu za
kukusanya mapato pamoja na kupunguza misamaha ya kodi ili kuweza kugharamia kwa
kiwango kikubwa matumizi ya Serikali kwa kutumia mapato ya ndani. Kwa
kuzingatia azma hiyo, Serikali imechukua hatua zifuatazo katika eneo la mapato:-
(i)
Kuboresha
mifumo ya ukusanyaji na usimamizi wa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi kwa
kupitia upya mfumo wa ukadiriaji kodi, utoaji wa stakabadhi na leseni, pamoja
na kuboresha viwango vya kubakiza maduhuli kwa Wizara, Idara na Taasisi za
Serikali;
(ii)
Kupanua
wigo wa kodi kwa kuendelea kurasimisha sekta isiyo rasmi ili iingie kwenye
mfumo wa kodi;
(iii)
Kufanya
mapitio ya sheria za Wakala/Taasisi za Umma zinazokusanya maduhuli ili ziweze
kuchangia zaidi kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali;
(iv)
Kufanya
mapitio ya sheria mbalimbali zinazotoa misamaha ya kodi kwa lengo la kudhibiti
na kupunguza misamaha hiyo;
(v)
Kupitia
upya mfumo wa ukusanyaji wa kodi ya majengo katika majiji, manispaa, miji,
wilaya na miji midogo ili kuuboresha zaidi;
(vi)
Kufanya
mapitio ya vyanzo vya mapato na mfumo wa ukusanyaji katika Mamlaka za Serikali za
Mitaa ili kuongeza mapato; na
(vii)
Kujenga
uwezo wa Wizara ya Fedha, Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Maendeleo la
Petroli Tanzania, Mamlaka ya Mapato Tanzania, na Wakala wa Ukaguzi wa Madini
ili kuweza kusimamia ukusanyaji wa mapato katika maeneo ya madini, gesi na
petroli.
Mwenendo wa Ukusanyaji Mapato
ya Ndani
16.
Mheshimiwa
Spika, hadi
kufikia mwezi Aprili 2013, jumla ya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi yalifikia
kiasi cha shilingi bilioni 6,717.2, sawa na asilimia 93.2 ya makadirio ya
kukusanya shilingi bilioni 7,209.2 katika kipindi hicho na asilimia 77.1 ya
makadirio ya mwaka ya shilingi bilioni 8,714.7. Kati ya makusanyo hayo, mapato ya kodi
yalikuwa shilingi bilioni 6,371.3 ambayo ni sawa na asilimia 96 ya makadirio ya
kipindi hicho na asilimia 79.0 ya lengo la mwaka la shilingi bilioni 8,070.1 na
mapato yasiyotokana na kodi yalikuwa shilingi bilioni 357.8 ikiwa ni asilimia 55.5
ya lengo la mwaka la shilingi bilioni 644.6.
17.
Mheshimiwa
Spika, tathmini
ya makusanyo ya mapato ya kodi inaonesha mwenendo wa kuridhisha ambapo hadi
kufikia mwezi Aprili 2013, makusanyo ya ushuru wa forodha yalifikia shilingi
bilioni 487.8, sawa na asilimia 84.6 ya kukusanya shilingi bilioni 576.7;
mapato kutokana na kodi ya ongezeko la thamani yalifikia shilingi bilioni
1,965.5, sawa na asilimia 90.3 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 2,176.4.
Kwa upande wa ushuru wa bidhaa, hadi kufikia mwezi Aprili 2013 jumla ya
shilingi bilioni 1,050.7 zimekusanywa ambazo ni sawa na asilimia 90.3 ya
kukusanya shilingi bilioni 1,163.1. Kwa upande wa kodi ya mapato kwa makampuni,
makusanyo yalifikia shilingi bilioni 2,381.9 hadi mwezi Aprili 2013, ambayo ni
sawa na asilimia 105.4 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 2,260.7
18.
Mheshimiwa
Spika, kuongezeka kwa
makusanyo ya kodi kulitokana, pamoja na sababu nyingine, na: kuongezeka kwa
makusanyo ya kodi ya mapato ya makampuni; kuongezeka kwa kodi ya zuio
inayotokana na malipo ya gawio katika makampuni ya madini; na ukusanyaji wa
malimbikizo ya kodi. Hatua zingine za kiutawala zilizosababisha kuongezeka kwa
mapato zinajumuisha: kuhakikisha mashine za kielektroniki zinatumika ipasavyo;
kuendelea kuimarisha mfumo wa kusimamia vitalu vya kodi; kuboresha mfumo wa
uthamanishaji bidhaa; kuimarisha ukaguzi wa hesabu za walipa kodi; mapato
kutokana na mauzo ya hisa za kampuni ya M/S BP Tanzania; kuongezeka kwa ushuru
wa bidhaa wa muda wa maongezi wa simu; na utozaji wa ushuru wa bidhaa katika
bidhaa zote zisizo za petroli zinazostahili kutozwa kodi hiyo.
19.
Mheshimiwa
Spika, licha ya mafanikio
hayo, baadhi ya kodi zimeonesha mwenendo usioridhisha tofauti na ilivyotarajiwa,
hasa kwenye kodi ya ongezeko la thamani, ushuru wa bidhaa kwenye bidhaa zisizo
za petroli na kodi ya mapato inayotokana na ajira. Aidha, uzalishaji katika
baadhi ya viwanda ulipungua na hivyo kusababisha makusanyo ya ushuru wa bidhaa
na kodi ya ongezeko la thamani kuwa chini ya matarajio. Vilevile, kumekuwa na
ongezeko la uingizaji bidhaa kupitia njia zisizo rasmi bila kulipia ushuru na
kodi.
20.
Mheshimiwa
Spika,
makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi yamekuwa hayaridhishi kutokana na: uwezo
mdogo wa ukusanyaji na kukosa utaalam, vifaa duni na mifumo dhaifu ya
ukusanyaji wa mapato ambayo inachangia katika upotevu wa mapato. Baadhi ya wakala
na Mashirika bado hayachangii ipasavyo kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Aidha,
baadhi ya Idara ambazo zilikuwa vyanzo muhimu zimegeuzwa kuwa Wakala
zilizoundwa chini ya Wizara mbalimbali hivyo kupunguza michango yake kwenye
mapato ya Mfuko Mkuu wa Serikali.
21.
Mheshimiwa
Spika, hadi mwezi Aprili 2013, mapato yanayokusanywa na Mamlaka
za Serikali za Mitaa yalifikia shilingi bilioni 177.4, sawa na asilimia 49 ya
lengo la mwaka la kukusanya shilingi bilioni 362.2.
Misaada na Mikopo ya Nje yenye Masharti Nafuu
22.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka
2012/13, Serikali ilikadiria kupata shilingi bilioni 842.5 kama misaada na
mikopo ya kibajeti. Hadi kufikia Aprili, 2013 Serikali ilipata misaada na
mikopo ya kibajeti ya shilingi bilioni 645.4 ambazo ni sawa na asilimia 77 ya
makadirio ya mwaka. Kwa upande mwingine, shilingi bilioni 443.4 zilipokelewa
kupitia mifuko ya kisekta, ikiwa ni sawa na asilimia 107 ya makadirio ya
shilingi bilioni 415.1 kwa mwaka.
23.
Mheshimiwa
Spika, misaada na mikopo
nafuu iliyopokelewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa kipindi kilichoishia
Aprili, 2013 ilifikia shilingi bilioni 1,235.7 ambayo ni asilimia 65 ya ahadi
ya shilingi bilioni 1,899.1 kwa mwaka. Kumekuwepo na changamoto inayotokana na Washirika
wa Maendeleo kuchelewa kutoa taarifa wanapotuma fedha moja kwa moja kwenye miradi
husika; kasi ndogo ya utekelezaji wa baadhi ya miradi; ucheleweshwaji wa
taarifa za utekelezaji wa miradi kutoka Wizara, Idara, Taasisi, Mikoa na
Serikali za mitaa; pamoja na mchakato mrefu wa ununuzi, hususan inapohusisha
kupata idhini ya mfadhili (no objection).
Mikopo ya Ndani
24.
Mheshimiwa
Spika, katika kipindi
cha Julai hadi Aprili 2013, Serikali ilikopa shilingi bilioni 1,364.7 kutoka
soko la ndani la mitaji kwa ajili ya kulipia dhamana za Serikali zilizoiva pamoja
na shilingi bilioni 809.1 kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya
maendeleo.
Mikopo
ya Nje yenye Masharti ya Kibiashara
25.
Mheshimiwa
Spika, mwaka
2012/13 Serikali ilikadiria kupata mikopo yenye masharti ya kibiashara shilingi
bilioni 1,254.1, sawa na Dola za Kimarekani milioni 800 kwa ajili ya kugharamia
miradi mbalimbali ya maendeleo katika bajeti ya mwaka 2012/13 iliyopitishwa na
Bunge lako tukufu. Hadi kufikia Mei 2013, Serikali ilipokea shilingi bilioni 947,
sawa na dola milioni 600 kutoka benki ya Stanbic, na shilingi bilioni 59.2,
sawa na dola milioni 37 kutoka benk ya Credit Suisse.
Sera
za Matumizi
26.
Mheshimiwa
Spika, Serikali
ilitekeleza sera za matumizi kwa kuzingatia vipaumbele vilivyoainishwa kwenye
Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2012/13, ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na
kupunguza umaskini. Aidha, sera za matumizi zililenga kupunguza nakisi ya
bajeti kwa kuwianisha mapato na matumizi; kuzingatia Sheria ya Fedha za Umma na
Sheria ya Ununuzi wa Umma; kusimamia ulipaji wa mishahara; na kuendelea kuhakiki
na kulipa madai ya wakandarasi, wazabuni, watoa huduma na watumishi, pamoja na
kufuatilia utekelezaji wa bajeti.
27.
Mheshimiwa
Spika, Serikali ilikadiria kutumia shilingi
bilioni 15,191.9 katika mwaka 2012/13. Mgawanyo wa matumizi ya Serikali katika
kipindi hiki ulikuwa kama ifuatavyo: shilingi bilioni 10,597.1 zilitengwa kwa
matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 4,594.8 zilikadiriwa kutumika kwa ajili
ya matumizi ya maendeleo.
Mwenendo wa Matumizi
28.
Mheshimiwa
Spika, hadi kufikia Aprili 2013, matumizi
ya kawaida bila kujumuisha malipo ya hatifungani zilizoiva (rollover) yalifikia shilingi bilioni 7,582.6,
sawa na asilimia 82 ya makadirio ya mwaka. Kati ya kiasi hicho, malipo ya
mishahara ya watumishi wa Serikali, katika wizara, Idara zinazojitegemea, Sekretarieti
za Mikoa, Mamlaka ya Serikali za Mitaa na Taasisi za Umma yalikuwa shilingi
bilioni 3,209.2 sawa na asilimia 85 ya makadirio ya mwaka ya shilingi bilioni
3,781.1.
29.
Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka
2012/13 Serikali iliendelea na udhibiti wa ulipaji wa mishahara ya watumishi wa
umma. Kwa mwaka 2012/13 Serikali imekamilisha uhakiki wa watumishi na malipo ya
mishahara kwenye Wizara pamoja na Sekretarieti za Mikoa. Kazi hii ilianza mwaka
2011/12 kwa kufanya uhakiki wa watumishi wa Serikali kwenye Mamlaka za Serikali
za Mitaa na Taasisi zote. Matokeo ya uhakiki wa watumishi yalisambazwa kwa
waajiri kwa ajili ya kuchukua hatua zinazostahili. Aidha, Serikali imechukua
hatua ya kusambaza mfumo wa malipo kwa waajiri wote ili marekebisho ya
mishahara, waajiriwa wapya, kuondoa watumishi wanaomaliza utumishi wao
(wanaostaafu, wanaofukuzwa, wanaofariki, wanaocha kazi) yaweze kufanyika mara
moja baada ya tukio hilo kutokea kwenye kituo cha kazi. Katika mwaka 2013/14
Serikali itaendelea na hatua za kudhibiti mishahara ya watumishi, ikiwa ni
pamoja na Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali kuendelea kukagua eneo hilo.
30.
Mheshimiwa
Spika, Serikali
iliendelea kutoa kipaumbele katika kulipa Deni la Taifa. Katika kipindi hicho, malipo ya riba kwa mikopo ya ndani na
nje yalikuwa shilingi bilioni 438.8, sawa na asilimia 79 ya makadirio ya shilingi bilioni 555.2 kwa mwaka. Malipo ya deni halisi la mikopo
ya nje yalikuwa shilingi bilioni 79.0, sawa na asilimia 34 ya makadirio ya
mwaka. Aidha, Serikali ilitumia shilingi bilioni 1,364 kwa ajili ya kulipia
dhamana za Serikali za muda mfupi na Hatifungani za Serikali zilizoiva. Vilevile,
matumizi mengineyo katika Wizara, Idara, Taasisi za Serikali, Mikoa na
Halmashauri yalifikia shilingi bilioni 3,000.8 ikiwa ni asilimia 74 ya
makadirio ya shilingi bilioni 4,070.9 kwa mwaka.
31.
Mheshimiwa
Spika, hadi Aprili 2013,
jumla ya shilingi bilioni 3,956.3 zilitolewa katika miradi ya maendeleo
ikilinganishwa na makadirio ya mwaka ya kutumia shilingi bilioni 4,594.8. Kati
ya hizo, fedha za ndani zilikuwa shilingi bilioni 2,277.2 ikilinganishwa na
makadirio ya mwaka ya shilingi bilioni 2,280.6, sawa na asilimia 99.9. Aidha, fedha
za nje zilikuwa shilingi bilioni 1,679.1 ikilinganishwa na makadirio ya
shilingi bilioni 2,314.2 sawa na asilimia 73 ya makadirio ya mwaka.
Usimamizi
wa Fedha za Umma
32.
Mheshimiwa
Spika, mwaka 2012/13,
Serikali ilianza kutekeleza mpangokazi wa miaka mitano wa kuiwezesha Serikali
Kuu kuandaa hesabu kwa viwango vipya vya uhasibu vya Kimataifa (IPSAS Accrual
Basis). Kwa mara ya kwanza hesabu za
Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea na Sekretarieti za Mikoa kwa mwaka wa
fedha unaoishia tarehe 30 Juni, 2013 zitaandaliwa kwa kutumia viwango hivyo.
Wizara imeandaa miongozo mbalimbali na kufanya mikutano elekezi ili kuwajengea
uwezo wa uelewa wahasibu na wadau mbalimbali.
33.
Mheshimiwa
Spika, katika kudhibiti
mapato na matumizi, Serikali imeandaa na kutoa miongozo ya usimamizi wa
vihatarishi katika sekta ya umma pamoja na mwongozo wa uhakiki wa ubora wa
ukaguzi wa ndani. Serikali pia imetayarisha mwongozo wa ukaguzi wa ndani kwa
kuzingatia viwango vya kimataifa ambao unategemea kuanza kutumika rasmi Julai,
2013. Miongozo hiyo ina lengo la kuboresha utendaji kazi wa ukaguzi wa ndani.
Maslahi ya Watumishi
34.
Mheshimiwa Spika, Mwaka 2012/13, Serikali iliendelea kuboresha maslahi
ya watumishi wa umma kulingana na uwezo wa mapato yake kwa lengo la kuwawezesha
kumudu gharama za maisha. Maeneo ambayo yalitiliwa mkazo ni pamoja na ongezeko
la mshahara hasa kima cha chini, kupunguza kiwango cha kodi ya mapato kwenye
mishahara, malipo ya mshahara kwa wakati na kuhakikisha watumishi wanalipwa
mafao yao mara baada ya kustaafu.
Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA II)
35.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa MKUKUTA II umeonesha mafanikio katika
maeneo mengi ingawa bado kuna changamoto. Mafanikio hayo ni pamoja na kuendelea
kukua kwa pato la Taifa, kuongezeka kwa mapato ya kodi, kukua kwa sekta ya
fedha na mikopo kwa sekta binafsi, kuimarika kwa usimamizi wa matumizi ya
Serikali na kuimarika kwa utoaji na upatikanaji wa huduma za jamii.
36.
Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kutathmini hali ya umaskini hapa nchini, Serikali
imefanikiwa kukamilisha zoezi la ukusanyaji wa takwimu za Utafiti wa Hali ya
Mapato na Matumizi katika kaya binafsi ya mwaka 2012. Uchambuzi wa takwimu hizo
unaendelea na unatarajia kukamilika kabla ya Desemba 2013. Aidha, takwimu za
Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika 2012, na Utafiti wa Hali ya Ajira na
Kipato wa mwaka 2012 vitafanyiwa uchambuzi wa kina ili kutuwezesha kupata
takwimu zitakazoonesha hali ya umaskini katika ngazi mbalimbali. Tafiti hizi
zitatoa matokeo ya utekelezaji wa MKUKUTA katika nguzo ya kwanza ya Kupunguza
Umaskini na Ukuaji wa Uchumi.
37.
Mheshimiwa
Spika, kwa upande wa nguzo ya pili ya MKUKUTA ya kuboresha
hali ya maisha na ustawi wa jamii, viashiria vingi vilionesha mabadiliko
chanya. Viwango vya uandikishaji katika ngazi za elimu ya msingi na sekondari
vimeimarika. Aidha, uandikishaji katika ngazi ya vyuo vya ufundi na elimu ya
juu uko katika kiwango cha kuridhisha. Matokeo haya yanatokana na utekelezaji
wa juhudi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya shule, vyuo,
waalimu, upanuzi wa miundombinu ya ufundishaji na kuongezeka kwa mikopo ya
elimu ya juu. Changamoto iliyopo ni kuboresha mazingira ya kufundishia na
kujifunza katika ngazi zote. Katika mwaka 2012/13, Serikali
iliendelea pia kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha huduma za afya, lishe,
upatikanaji wa maji safi na salama na utoaji elimu kwa umma kuhusu kinga ya
malaria na athari za ugonjwa wa UKIMWI.
38.
Mheshimiwa Spika, ili kuimarisha utawala bora na uwajibikaji,
Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuimarisha mfumo wa usimamizi wa
mali za umma, kuimarisha mfumo wa sheria na haki za binadamu, hususan katika
ngazi za chini kwa kuongeza idadi ya mahakimu.
Hatua hii imeboresha kasi ya utoaji maamuzi ya mashauri katika mahakama
zetu. Aidha, programu ya maboresho ya sekta ya sheria nayo iliendelea
kutekelezwa, lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa haki za raia zinaboreshwa na
kulindwa, hususan wale walio katika mazingira hatarishi.
Sensa ya Watu na Makazi
39.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/13,
Serikali ilifanya Sensa ya Watu na Makazi kama ilivyopangwa ambapo jumla ya
shilingi bilioni 127.3 zilitumika. Matokeo ya sensa hiyo, yalibainisha kuwa
Tanzania ina jumla ya watu milioni 44.9 sawa na ongezeko la asilimia 2.6 kwa
mwaka ikilinganishwa na matokeo ya Sensa ya mwaka 2002 ambapo ongezeko lilikuwa
asilimia 2.9.
40.
Mheshimiwa Spika, kasi ya ongezeko la idadi ya
watu ni kubwa kwa mikoa ya Dar es Salaam na Mjini Magharibi ambapo kasi ya
ongezeko la idadi ya watu kwa mkoa wa Dar es Salaam ni asilimia 5.6 kwa
mwaka, wakati Mjini Magharibi kasi hiyo ni asilimia
4.2. Aidha, mkoa wa Dar es salaam una idadi
kubwa ya watu ikilinganishwa na mikoa mingine ukiwa na asilimia 10 ya idadi ya
wakazi wote wa Tanzania Bara. Vilevile, wastani wa idadi ya watu kwa kaya kwa
mwaka 2012 umebakia karibu sawa na ule wa mwaka 2002. Wastani ulikuwa watu 4.9
kwa kaya mwaka 2012 ikilinganishwa na watu 4.8 mwaka 2002. Napenda niwajulishe waheshimiwa
wabunge kwamba Serikali inatumia takwimu za sensa hii katika kuandaa sera,
mikakati, mipango na kufanya tathmini ya utekelezaji wa mikakati na mipango
yake. Nashauri wadau wengine wafanye hivyo pia wakati wa kuandaa mipango ya
maendeleo kwa ajili ya ujenzi wa Taifa letu.
41.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na
uchambuzi wa kina wa matokeo ya Sensa ambayo yatahusisha viashiria vya kiuchumi
na kijamii. Napenda nitumie nafasi hii kuwajulisha kuwa toleo linalofuata ni la
mgawanyo wa watu kwa umri na jinsia katika ngazi ya Taifa, Mkoa na Wilaya
ambalo litatolewa mwezi Julai, 2013. Matokeo yanayofuata ambayo yanahusu
viashiria vya kiuchumi na kijamii yataendelea kutolewa kama yalivyoanishwa
kwenye ratiba ya usambazaji na pia katika tovuti ya Serikali.
Sekta ya Fedha
42.
Mheshimiwa Spika, Serikali iliendelea
kutekeleza progamu ya maboresho ya sekta ya fedha ili kuhakikisha kwamba sekta
hii inachangia kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kukuza Pato la Taifa. Katika
mwaka 2012, huduma ya sekta ya fedha ilichangia asilimia 1.8 ya pato la Taifa ikilinganishwa
na asilimia 1.7 mwaka 2011. Aidha, katika kipindi hicho, sekta ya fedha ilikua
kwa asilimia 13.2 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 10.7 mwaka 2011. Ongezeko
hilo lilitokana na mafanikio ya utekelezaji wa maboresho ya sekta ya fedha
ambayo yaliwezesha kuongezeka kwa idadi ya benki kutoka 49 Februari 2012 hadi 51
Februari 2013; kampuni za bima kutoka 26 mwaka 2011 hadi 28 mwaka 2012; na idadi
ya SACCOS kutoka 5,424 Machi 2012 hadi 5,559 Machi 2013.
43.
Mheshimiwa Spika, Serikali iliendelea kutekeleza sera ya fedha yenye lengo la kupunguza
ukwasi nchini ambapo Benki Kuu iliongeza mauzo ya fedha za kigeni katika soko
la fedha za kigeni pamoja na mauzo ya dhamana za Serikali. Aidha, Benki Kuu
ilipandisha kiwango cha chini cha fedha zinazotakiwa kuhifadhiwa Benki Kuu kwa
ajili ya akiba ya amana za serikali katika mabenki kutoka asilimia 30 hadi
asilimia 40, pamoja na kupunguza kiwango cha kuhodhi fedha za kigeni kulingana
na mitaji yao kwa mabenki kutoka asilimia 10 hadi asilimia 7.5 kuanzia Desemba,
2012. Hatua hizo zilisaidia katika kupunguza kiwango cha mfumuko wa bei usiojumuisha
chakula na nishati (core inflation) kutoka asilimia 8.7 Mei, 2012 hadi asilimia
7.1 Mei, 2013. Vilevile, hatua hizi zilisaidia kuimarika kwa kiwango cha
ubadilishanaji wa shilingi dhidi ya Dola ya Kimarekani.
44.
Mheshimiwa
Spika, Serikali
ilifanya utafiti wa huduma ndogo ndogo za bima kwa lengo la kuboresha
upatikanaji wa huduma za bima kwa wananchi walio wengi. Utafiti umebaini kwamba
kiwango cha matumizi ya huduma za bima bado ni kidogo, ambapo ni asilimia 19 tu
ya watu wazima wanatumia huduma hizo (hii inajumuisha huduma za bima ya afya
zinazotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya). Utafiti umebaini pia kwamba
uhitaji wa huduma ndogo ndogo za bima ni mkubwa na upatikanaji wa huduma hizo
utasaidia katika juhudi za Serikali za kukuza uchumi na kuondoa umaskini.
Serikali iliendelea kuwahamasisha wananchi ili waone umuhimu wa kujiunga na
huduma za bima.
45.
Mheshimiwa
Spika, Serikali
ilianzisha kampuni ya Tanzania Mortgage Refinancing Company (TMRC) ili kuwezesha
benki kutoa mikopo ya nyumba. Ili benki ziweze kupata mikopo hiyo, zinapaswa ziwe
na hisa kwenye kampuni hiyo. Hadi kufikia Desemba 2012, benki 12 zimenunua
hisa. Serikali kupitia Kampuni ya TMRC ilitoa mikopo yenye thamani ya shilingi
bilioni 4.2 kwa benki 12 wanachama, ambazo zilitoa mikopo 1,799 yenye thamani
ya shilingi bilioni 106.2.
46.
Mheshimiwa
Spika, katika kutimiza
azma ya Serikali ya kuimarisha usimamizi na maendeleo ya Sekta ya Fedha, Serikali
inaendelea kuweka mazingira mazuri kwa kuanzisha Idara ya Maendeleo ya Sekta ya
Fedha ambayo ndani yake kutakuwa na kitengo cha kusimamia sekta ya huduma ndogo
ndogo za fedha na kitengo cha sera za sekta ya fedha. Muundo huu mpya kwa sasa
uko katika hatua ya kuridhiwa. Miongoni mwa majukumu ya idara hii ni kuandaa
sera ya sekta ya huduma ndogo ndogo za fedha.
47.
Mheshimiwa
Spika, katika kuhamasisha
uanzishwaji wa benki za wananchi, Benki kuu imekuwa ikitoa masharti nafuu
yanayohusu mtaji wakati zinapoanza. Kwa mfano, wakati benki za biashara
zinatakiwa kuwa na mtaji wa shilingi bilioni 15, benki za wananchi zinatakiwa
kuwa na shilingi bilioni 2. Kwa upande mwingine, Serikali imekuwa ikihimiza
uanzishwaji wa SACCOS, VICOBA na benki za wananchi ili kuwawezesha wananchi
kupata mitaji kwa ajili ya biashara na uzalishaji.
Ununuzi wa Umma
48.
Mheshimiwa
Spika, Bunge lako tukufu
limetunga Sheria mpya ya Ununuzi wa Umma Na. 7 ya mwaka 2011 baada ya kubaini
upungufu uliokuwepo katika Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 21 ya mwaka 2004.
Aidha, Bunge lako pia limetunga Sheria ya Ubia Na. 19 ya mwaka 2010 ambayo
utekelezaji wake katika hatua ya kumpata Mbia unatumia Sheria ya Ununuzi wa
Umma. Hivyo kuna haja ya kufanya marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 7
ya mwaka 2011 ili kuzingatia maboresho na mabadiliko yanayohitajika. Mbali na
kuleta uwiano wa Sheria ya Ununuzi na Sheria ya Ubia, maboresho yanalenga
kuweka misingi imara ya taratibu za kusimamia ununuzi wa umma; kufafanua
majukumu ya Mamlaka za usimamizi wa ununuzi wa umma; na kuongezea madaraka ya
kiutendaji Taasisi za ununuzi na zile zinazosimamia ununuzi wa umma. Aidha,
maboresho yanalenga kupunguza muda wa kushughulikia malalamiko ya wazabuni, na
kupunguza muda wa mchakato wa ununuzi. Serikali inakusudia kufuta Sheria ya
Ununuzi wa Umma na. 21 ya 2004 mara baada ya mabadiliko ya Sheria Na. 7
kukamilika na Kanuni mpya kutangazwa katika gazeti la Serikali.
Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi
49.
Mheshimiwa
Spika, Serikali imeendelea
kusimamamia sera yake ya kushirikisha sekta binafsi ili iweze kuongeza Pato la
Taifa. Katika mwaka 2012/13, Serikali ilifanya uchambuzi wa awali wa baadhi ya
miradi ya PPP katika sekta za ujenzi wa barabara na bandari. Miradi hiyo ni
pamoja na ujenzi wa barabara ya Dar es Salaam – Chalinze, bandari ya Katanga,
bandari ya Mwambani, na bandari ya Mtwara.
50.
Mheshimiwa
Spika, katika kutekeleza
Sheria ya Ubia ya mwaka 2010, changamoto iliyojitokeza ni kuwepo kwa vitengo na
ofisi nyingi zinazoshughulikia masuala ya PPP. Kwa kutambua hili, Serikali katika
mwaka 2013/14 itaunganisha vitengo vya PPP na kufanya mapitio ya sheria na
kanuni za ubia kwa nia ya kufanya maboresho. Aidha, katika mwaka 2013/14,
Serikali imepanga kuanzisha mfuko maalumu utakaotumika kugharamia upembuzi
yakinifu ili kuendeleza miradi ya ubia hapa nchini.
Deni la Taifa
51.
Mheshimiwa Spika, hadi mwishoni mwa Machi 2013, Deni la Taifa (likijumuisha deni la umma
na sekta binafsi) lilikuwa shilingi bilioni 23,673.53 ikilinganishwa na deni la
shilingi bilioni 20,276.6 Machi 2012 likiwa ni ongezeko la asilimia 17. Kati ya
kiasi hicho, shilingi bilioni 18,282.02 ni deni la nje na shilingi bilioni
5,397.50 ni deni la ndani. Deni la nje, linajumuisha deni la umma la shilingi
bilioni 15,203.34 na deni la sekta binafsi ni shilingi bilioni 3,078.69. Kiasi
hicho cha deni la nje kinajumuisha deni halisi shilingi bilioni 16,087.43 na
malimbikizo ya riba ya shilingi bilioni 2,194.59. Deni la ndani linajumuisha
hati fungani za muda mrefu kiasi cha shilingi bilioni 4,261.03 na dhamana za
Serikali za muda mfupi kiasi cha shilingi bilioni 1,136.48. Mikopo hiyo
iligharamia miradi ya maendeleo hususan miundombinu kwa kuzingatia vipaumbele
vilivyopitishwa na Bunge lako tukufu.
Uhimilivu wa Deni la Taifa
52.
Mheshimiwa
Spika, Serikali inasimamia
deni la taifa kwa kuzingatia Mkakati wa Taifa wa Kusimamia Deni la Taifa pamoja
na Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada ya mwaka 1974 kama ilivyorekebishwa
mwaka 2004. Kwa kuzingatia Sheria hiyo, mwaka 2012 Serikali ilifanya tathmini ya
kuangalia uhimilivu wa deni la Taifa. Napenda kulijulisha bunge lako tukufu
kwamba, viashiria vyote vya kupima uhimilivu wa deni vilivyokubalika kimataifa
vinaonesha kuwa, deni la Taifa ni himilivu katika muda mfupi na muda wa kati.
Mathalani, uwiano wa thamani ya sasa ya deni la Taifa kwa Pato la Taifa ni
asilimia 18.9, ikilinganishwa na ukomo wake wa asilimia 50 na kiashiria cha
uwiano wa thamani ya sasa ya deni la Taifa kwa mapato yanayotokana na mauzo ya
bidhaa na huduma nje ya nchi ilikuwa asilimia 53.6 ikilinganishwa na ukomo wa
asilimia 200.
Tathmini ya Uwezo wa Kukopa na Kulipa Madeni
53.
Mheshimiwa Spika, Serikali
imepiga hatua kubwa katika kufanikisha zoezi la nchi kufanyiwa tathmini ya
uwezo wa kukopa na kulipa madeni na ipo kwenye hatua ya kupata kampuni za
kufanya tathmini. Kazi hii imepangwa kukamilika mwaka 2013/14 ambapo itawezesha
nchi kukopa kwa gharama nafuu katika masoko ya fedha ya kimataifa kwa ajili ya
kugharamia miradi mikubwa ya miundombinu. Aidha, kampuni za Tanzania nazo zitaweza
kupata mitaji kwa urahisi zaidi kutoka kwenye masoko ya mitaji ya kimataifa.
Ushirikiano
wa Kiuchumi wa Kikanda
54.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha ushiriki katika Jumuiya
ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Africa
(SADC). Ushiriki wetu katika jumuiya hizi ni mojawapo ya mkakati wa kuhakikisha
tunaitumia jiografia ya nchi yetu kwa kukuza uchumi.
55.
Mheshimiwa Spika, mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umefikia
hatua ya kuanzisha Umoja wa Fedha na majadiliano ya Itifaki hiyo yanaendelea na
yanatarajiwa kukamilika mwezi Novemba 2013. Aidha, hatua zinachukuliwa za
kutekeleza Itifaki ya Soko la Pamoja ambapo yameainishwa maeneo katika sheria
zetu yanayotakiwa kufanyiwa marekebisho ili kuwezesha ushiriki wa nchi katika
soko hili. Baadhi ya sheria zitakazo rekebishwa ni zile zinazohusika na taratibu za kuwezesha
watanzania kuwekeza mitaji yao katika nchi za Jumuiya; lengo likiwa kurahisisha
biashara ya mitaji na huduma ili kuchochea uwekezaji.
56.
Mheshimiwa Spika, mwaka
2012/13, Serikali iliendelea
na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Maendeleo wa SADC, ambapo taratibu za
kuridhia Itifaki ya Fedha na Uwekezaji ya SADC zimekamilika. Itifaki hii
itarahisisha taratibu za uwekezaji katika nchi za SADC, kuwezesha nchi za SADC
kuwianisha sera za kodi hasa eneo la vivutio vya uwekezaji. Kupitia Itifaki
hii, nchi za SADC zitaweza kubuni na kutekeleza sera za kuimarisha uchumi na
fedha kwa pamoja kwa lengo la kuwa na utulivu wa uchumi katika ukanda huu na
hivyo kuvutia uwekezaji. Ili kuhakikisha
azma hii inatekelezwa kwa vitendo, nchi za SADC zinakamilisha utaratibu wa
kuanzisha Mfuko wa Maendeleo.
III.
MAFANIKIO NA CHANGAMOTO KATIKA UTEKELEZAJI WA BAJETI
YA MWAKA 2012/13
57.
Mheshimiwa Spika, mafanikio na changamoto za utekelezaji wa bajeti kwa
mwaka 2012/13 kwa kila sekta yameelezwa kwa kina katika hotuba za bajeti za wizara
husika ambazo bunge lako tukufu limepata fursa ya kuzijadili na kuzipitisha. Kwa
kuzingatia hilo, nitaeleza kwa kifupi baadhi ya mafaniko na changamoto hizo.
Ukusanyaji wa Mapato
58.
Mheshimiwa Spika, bajeti ya mwaka 2012/13 ilitekelezwa kwa mafanikio,
hususan katika ujenzi wa miundombinu ya kiuchumi; utoaji wa huduma za jamii;
kuimarisha ulinzi na usalama, pamoja na utengamano wa kikanda na kimataifa.
Aidha, Serikali imefanikiwa kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani, hususan
mapato ya kodi kutoka wastani wa shilingi bilioni 540 kwa mwezi kwa mwaka
2011/12 hadi shilingi bilioni 640 kwa mwezi kwa mwaka 2012/13. Pamoja na
wastani huo wa mwezi, kiwango cha juu cha makusanyo kilifikiwa mwezi Desemba
2012, ambapo makusanyo ya kodi na yasiyo ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 890.
Ukuaji wa
Uchumi
59.
Mheshimiwa Spika, Pato la
Taifa limeendelea kuimarika mwaka 2012 ambapo ukuaji halisi ulikuwa asilimia
6.9 ikilinganishwa na asilimia 6.4 mwaka 2011. Ongezeko hili la ukuaji
lilitokana na kuboreshwa kwa miundombinu ya usafirishaji na mawasiliano, pamoja
na kuimarika kwa uzalishaji viwandani kutokana na jitihada za serikali za
kuhakisha upatikanaji wa umeme wa uhakika sambamba na matumizi ya nishati
mbadala katika uzalishaji viwandani.
60.
Mheshimiwa Spika, sekta ya
mawasiliano ndiyo ilikuwa na kiwango kikubwa cha ukuaji wa asilimia 20.6 mwaka
2012. Pamoja na kuwa na kiwango kikubwa cha ukuaji, sekta ya mawasiliano
ilichangia asilimia 2.3 tu katika Pato la Taifa ikilinganishwa na sekta ya
kilimo ambayo pamoja na kukua kwa kiwango kidogo ilichangia asilimia 24.7
katika Pato la Taifa mwaka 2012. Zaidi ya asilimia 70 ya watanzania wamejikita
katika shughuli za kilimo, hivyo hii ni sekta ambayo serikali inaitilia mkazo
ili kuhakikisha kuwa inaleta mafanikio yanayotarajiwa na wengi, ikiwemo
kupunguza umaskini. Serikali imefanya jitihada kubwa za kuboresha sekta hii
lakini bado imeendelea kukua kwa kiwango kisichozidi asilimia 5 kwa kipindi cha
miaka mitano iliyopita.
61.
Mheshimiwa Spika, Serikali
inaendelea na jitihada za kuimarisha sekta ya kilimo ili ikue kwa kasi zaidi na
kuongeza kipato na hivyo kupunguza umaskini kwa wananchi walio wengi. Juhudi
hizo zinahusisha kuendeleza miundombinu ya umwagiliaji ili kuondokana na kilimo
cha kutegemea mvua; kutoa ruzuku za pembejeo za kilimo kwa wakati zikiwemo
mbolea, madawa na mbegu bora; kuondoa kodi katika zana mbalimbali za sekta ya
kilimo ili kuongeza tija; kuimarisha masoko ya mazao, kuongeza thamani ya mazao
ya kilimo, mifugo na uvuvi na uhifadhi; na kuimarisha barabara vijijini. Aidha,
Serikali itaendeleza juhudi za upatikanaji wa umeme na maji vijijini. Vilevile,
Serikali itaimarisha sekta nyingine za kiuchumi zenye kutoa ajira kama vile
sekta za ujenzi na uzalishaji viwandani, pamoja na kupanua wigo wa kinga ya
jamii ili kuongeza ushiriki wao kwenye shughuli za uchumi na hivyo kuinua Pato la wananchi na kuongeza kasi ya kupunguza umaskini wa kipato.
Mwenendo wa Bei
62.
Mheshimiwa Spika, wastani wa
mfumuko wa bei kwa mwaka 2012 uliongezeka kwa asilimia 16.0 ikilinganishwa na
asilimia 12.7 mwaka 2011. Upandaji huu wa bei ulitokana hasa na kupanda kwa bei
ya mafuta ya petroli katika soko la dunia na kupanda kwa bei za chakula
kulikotokana na mahitaji makubwa ya chakula katika baadhi ya nchi jirani. Ikumbukwe kwamba chakula peke yake huchangia
asilimia 47.8 ya bidhaa na huduma zinazotumika katika ukokotoaji wa fahirisi ya
bei kwenye kapu la bidhaa za walaji, ikifuatiwa na usafiri (asilimia 9.5) na
nishati (asilimia 9.2). Makundi haya ni muhimu sana katika kuchochea mwelekeo
wa bei za bidhaa na huduma mbalimbali. Katika kukabiliana na kasi ya kupanda
kwa bei za bidhaa na huduma, Serikali ilichukua hatua kadhaa zikiwemo:
(i)
Kuhakikisha kuwa
kunakuwa na ugavi mzuri wa chakula unaoendana na mahitaji nchini;
(ii)
Kupanua kilimo cha
mazao ya chakula na kuongeza upatikanaji wa pembejeo za kilimo zikiwemo mbolea,
madawa na mbegu bora;
(iii)
Kuimarisha
miundombinu ya usafirishaji;
(iv)
Kuimarisha
upatikanaji wa umeme; na
(v)
Kupandisha kiwango
cha riba ya Benki Kuu inayotozwa kwa mikopo iendayo kwa taasisi za fedha nchini
kutoka asilimia 7.58 hadi asilimia 12.58.
63.
Mheshimiwa Spika, hatua hizi ziliwezesha kupunguza kiwango cha mfumuko
wa bei kutoka asilimia 18.2 mwezi Mei 2012
hadi asilimia 8.3 mwezi Mei 2013.
Mafanikio Katika Sekta Mbalimbali
64.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilitoa jumla ya shilingi bilioni 826.1 kwa
ajili ya kuwezesha upatikanaji wa umeme na kutekeleza miradi mbalimbali ya
kimkakati. Baadhi ya miradi iliyotekelezwa ni pamoja na: kuanza ujenzi wa bomba
la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam ikijumuisha ujenzi wa kituo cha
kupokelea gesi Kinyerezi; kukamilisha ujenzi na kuanza kuzalisha umeme kwa
kutumia mafuta mazito katika vituo vya Ubungo - Dar es Salaam (MW 105) na
Nyakato - Mwanza (MW 60); kuendeleza miradi ya umeme vijijini katika mikoa 16;
na kuendeleza upembuzi yakinifu katika miradi ya Makaa ya Mawe – Mchuchuma na Liganga.
Aidha, hadi kufikia mwezi Desemba 2012, kiasi cha umeme kilichoingizwa kwenye
Grid ya Taifa kilikuwa MWh 5,759,756 ikilinganishwa na MWh 5,153,400 mwaka 2011,
sawa na ongezeko la asilimia 11.8.
65.
Mheshimiwa Spika, sekta ya maji iliendelea kupewa kipaumbele katika
mwaka 2012/13 kwa kuendeleza ujenzi wa miradi ya maji katika vijiji 682 kupitia
mpango wa vijiji kumi kwa kila Halmashauri; uboreshaji wa mamlaka za maji
mijini; na ujenzi wa miundombinu ya maji, ikiwemo bomba la maji la Ruvu Chini
hadi Dar es Salaam. Ili kutekeleza miradi ya maji, Serikali ilitoa jumla ya
shilingi bilioni 106.6 katika ngazi ya Wizara na shilingi bilioni 98.4 katika
ngazi ya Halmashauri.
66.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/13, Serikali ilitoa jumla ya
shilingi bilioni 537.40 kwa ajili ya kuboresha huduma za afya tiba, kinga na
ustawi wa jamii. Fedha hizo pia zilitumika katika kuendeleza ujenzi na
ukarabati wa miundombinu ya afya; kuimarisha stadi na kujenga uwezo wa
rasilimali watu; na kuanza ujenzi wa Chuo Kikuu cha Afya, Mlonganzila - Dar es
Salaam.
67.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilitoa jumla ya shilingi bilioni 2,421.5
katika sekta ya elimu kwa ajili ya kugharamia shughuli mbalimbali katika shule
za msingi, sekondari, elimu ya watu wazima, vyuo vya ufundi stadi, na vyuo vya
elimu ya juu. Baadhi ya shughuli zilizotekelezwa ni pamoja na: ulipaji wa
mishahara kwa wakati; kuajiri walimu wapya 27,773 (walimu 13,633 wa shule ya
msingi, 14,060 wa sekondari na 80 wa vyuo vya ualimu) na kuwalipa stahili zao;
kugharamia uendeshaji mashuleni (Capitation); kutoa mikopo kiasi cha shilingi
bilioni 326.1 kwa wanafunzi 96,350 wa elimu ya juu; kuanza ujenzi wa maabara
katika shule mbili kwa kila Halmashauri 132 ambapo kiasi cha shilingi bilioni
102.3 kimetolewa; ununuzi wa vitabu vya kiada na ziada 27,159,106 kwa ajili ya shule za msingi; na kuendelea
kuboresha miundombinu ya kutolea elimu katika ngazi zote nchini.
68.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilitoa jumla ya shilingi
bilioni 1,044.2 kwa ajili ya kujenga na kukarabati barabara za lami; kufanya
matengenezo maalumu na ya kawaida kwenye barabara za changarawe; kuboresha
barabara za wilaya pamoja na kujenga na kukarabati madaraja. Aidha, fedha hizo
zilitumika kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vivuko vitatu na maegesho; kukarabati
vivuko vitano; na kufanya upembuzi yakinifu wa kujenga barabara na vivuko
katika maeneo mengine nchini. Vilevile, Serikali iliendelea na ujenzi na
ukarabati wa barabara za Dar es Salaam na miji mingine mikuu ili kupunguza
msongamano wa magari.
69.
Mheshimiwa Spika, sekta ya uchukuzi ilipewa jumla ya shilingi bilioni 181.8 kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwemo: kuanzisha usafiri wa treni
ya abiria jijini Dar es Salaam kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari na
adha ya usafiri jijini Dar es Salaam; kuboresha na kurejesha huduma za treni za
abiria na mizigo katika reli ya kati na TAZARA; na kuendeleza miradi ya ujenzi
wa viwanja vya ndege vya Songwe, Katavi, Mwanza, Kigoma na Tabora.
70.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kuimarisha utawala bora, Serikali ilitoa jumla ya
shilingi bilioni 27.0 kwa ajili ya mchakato wa marekebisho ya Katiba ikiwa ni
pamoja na kukusanya kura za maoni katika mikoa yote 30 ya Tanzania Bara na
Zanzibar na shilingi bilioni 40 kutekeleza mradi wa vitambulisho vya Taifa. Aidha,
shughuli zingine muhimu zilizotekelezwa ni kukamilisha rasimu ya awali ya
katiba mpya, kuchapisha nakala za rasimu ya katiba mpya na kuzisambaza kwa
wadau mbalimbali nchini pamoja na kuendesha mikutano ya Mabaraza ya Katiba.
71.
Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na upungufu wa chakula kwenye
baadhi ya maeneo nchini, Serikali ilitoa jumla ya shilingi bilioni 42.87 mwaka
2012/13 zilizotumika kununua tani 53,269.70 za nafaka kwa ajili ya kuongeza chakula
cha hifadhi ya Taifa. Aidha, Serikali ilisambaza chakula cha msaada kwa
wananchi wenye mahitaji katika Halmashauri 47 na kuuza jumla ya tani 16,653 kwa
wasagishaji wa nafaka ili kurahisisha usambazaji wa unga wa sembe na hatimaye kupunguza mfumuko wa bei nchini. Vilevile,
uzalishaji wa chakula katika msimu wa mwaka 2012/13 ulifikia tani milioni 13.34
ikilinganishwa na mahitaji ya chakula ya tani milioni 11.97.
72.
Mheshimiwa
Spika, pamoja na
mafanikio hayo, changamoto bado ni nyingi, ambazo ni pamoja na kuimarisha
ukusanyaji wa mapato kutoka vyanzo vya ndani na upatikanaji wa mikopo ya nje
yenye masharti ya kibiashara kwa wakati na hivyo kuchelewa kupeleka fedha
kwenye sekta husika. Changamoto nyingine ni: madai ya wakandarasi, wazabuni,
watumishi na watoa huduma wa ndani na nje; kuimarisha miundombinu; kupata
thamani ya fedha katika ununuzi wa umma; kuongeza ubora na tija katika
uzalishaji; kutumia fursa za kijiografia katika ukuzaji wa uchumi; upatikanaji
wa nishati ya umeme wa uhakika; riba za mikopo; kusimamia deni la Taifa;
kudhibiti mfumuko wa bei na mabadiliko ya tabianchi.
73.
Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine ni: huduma za jamii hususan elimu, afya, na maji bado hazijafikia
viwango vinavyotarajiwa; kuongeza fursa za ajira; kukuza ushirikiano kati ya
Serikali na sekta binafsi (PPP); na upatikanaji wa huduma za mikopo ya kilimo. Changamoto
hizo zitaendelea kutafutiwa ufumbuzi hatua kwa hatua katika kipindi cha muda wa
kati na muda mrefu. Aidha, Serikali imejipanga kukabiliana na baadhi ya
changamoto hizi katika mwaka 2013/14.
IV.
BAJETI YA MWAKA 2013/14
74.
Mheshimiwa
Spika, bajeti ya mwaka
2013/14 itazingatia vipaumbele vilivyoainishwa kwenye: Mpango wa Maendeleo wa
mwaka 2013/14 na mfumo mpya wa utekelezaji wa vipaumbele vyenye matokeo makubwa
na ya haraka (Big Results Now – BRN);
Awamu ya Pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUKUTA II);
Malengo ya Maendeleo ya Milenia 2015; Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010; na
programu za maboresho katika sekta ya umma. Lengo likiwa ni kufikia Dira ya
Taifa ya Maendeleo 2025.
Shabaha na Malengo ya Bajeti kwa Mwaka
2013/14
75.
Mheshimiwa
Spika, bajeti ya mwaka
2013/14, imejielekeza katika kufikia shabaha na malengo ya uchumi jumla yafuatayo:
(i)
Pato halisi la Taifa
linatarajiwa kukua kwa asilimia 7.0 mwaka 2013, na asilimia 7.2 mwaka 2014;
(ii)
Kuendelea kudhibiti
kasi ya upandaji bei ili ibaki kwenye viwango vya tarakimu moja, ambapo mfumuko
wa bei unatarajiwa kushuka zaidi kufikia asilimia 6.0 Juni 2014;
(iii)
Kuongezeka kwa mapato ya
ndani yatakayofikia uwiano na Pato la Taifa wa asilimia 20.2 mwaka 2013/14 ikilinganishwa na
matarajio ya asilimia 17.7 kwa mwaka 2012/13;
(iv)
Kuwa na nakisi ya bajeti
(ikijumuisha misaada) isiyozidi asilimia 5.0 ya Pato la Taifa mwaka 2013/14;
(v)
Kudhibiti ongezeko la ujazi
wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) katika wigo wa asilimia 15.0 Juni 2014 utakaowiana na malengo ya ukuaji wa uchumi na
kasi ya upandaji bei;
(vi)
Kuwa na akiba ya fedha za
kigeni itakayoweza kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje
kwa kipindi kisichopungua miezi minne mwaka 2013/14;
(vii)
Kupunguza tofauti ya
viwango vya riba vya kuweka na kukopa; na
(viii)
Kuimarisha thamani ya
Shilingi na kuwa na kiwango imara cha ubadilishanaji wa fedha kitakachotokana
na mwenendo wa soko la fedha.
Misingi
ya Bajeti ya Serikali kwa kipindi cha mwaka 2013/14
76.
Mheshimiwa Spika, ili kufikia malengo
yaliyoainishwa hapo juu, misingi ya bajeti ya Serikali kwa kipindi cha mwaka
2013/14 ni hii ifuatayo:-
(i)
Kuendelea kuimarisha na
kudumisha amani, usalama, utulivu na utengamano;
(ii)
Kuendelea kuboresha
viashiria vya uchumi jumla na maendeleo ya jamii vikiwemo Pato la Taifa,
biashara ya nje, fedha, mapato na matumizi na viashiria vya huduma za jamii;
(iii)
Kuongeza mapato ya ndani
kwa kuimarisha vyanzo vilivyopo na kubuni vyanzo vipya vya mapato;
(iv)
Kuboresha usimamizi wa
fedha za umma;
(v)
Kuimarisha mfumo wa IFMS na
kuhakikisha unatumika kuweka mihadi ya huduma na bidhaa kabla ya malipo;
(vi)
Kuzingatia vipaumbele vilivyopo
katika Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano hasa vipaumbele vyenye matokeo makubwa na ya haraka pamoja na MKUKUTA II;
(vii)
Kuboresha mfumo wa
utekelezaji wa vipaumbele na uwajibikaji;
(viii)
Kuendelea kuimarisha sera
za fedha ili ziendane na sera za bajeti zitakazosaidia kupunguza mfumuko wa bei
na tofauti ya riba za amana na za mikopo; na
(ix)
Kuendelea kuboresha
mazingira ya biashara na uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuvutia ushiriki wa sekta
binafsi katika uchumi.
Sera za Mapato
77.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka
2013/14, Serikali inakusudia kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha mapato ya
ndani yanayotokana na kodi na yasiyo ya kodi. Sera za mapato zinajumuisha
kupanua wigo wa kodi kwa kubainisha vyanzo vipya na kuimarisha usimamizi wa
ukusanyaji wa mapato kutoka vyanzo vilivyopo. Aidha, hatua zaidi zitachukuliwa
kudhibiti na kupunguza misamaha ya kodi. Kwa ujumla, sera na hatua
zitakazotekelezwa katika mwaka wa fedha 2013/14 zinalenga kuimarisha uwezo wa
Serikali kukusanya mapato ya ndani ili kupunguza utegemezi kutoka nje, na
kupunguza kutegemea kodi zinazotokana na biashara za kimataifa ambazo zimeanza
kushuka kutokana na kuongezeka kwa biashara za ushirikiano wa kikanda katika
nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa
Afrika.
78.
Mheshimiwa
Spika, kwa upande wa
mikakati ya pamoja ya kuongeza mapato ya Serikali, napenda kuchukua fursa hii
kukushukuru wewe binafsi kwa hatua uliyochukua ya kuunda Kamati ya Spika ili kuishauri
Serikali kuhusu vyanzo vya mapato ambapo baadhi ya mapendekezo yake yamezingatiwa
katika Sera za Mapato kwenye Bajeti ya mwaka 2013/14.
79.
Mheshimiwa
Spika, Serikali
itatekeleza baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa na Labs ya kubuni vyanzo vya mapato. Baadhi ya mapendekezo hayo ni
kuanza kuuza vitalu vya misitu na uwindaji kwa njia ya mnada na kufanya
tathmini ya mali na ardhi ili kuimarisha makusanyo ya tozo ya mali na kodi ya
ardhi. Hatua nyingine za kumairisha makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi tayari
zimeshatangazwa kupitia bajeti za Wizara husika.
80.
Mheshimiwa
Spika, Serikali katika
mwaka wa fedha wa 2013/14 itatekeleza mikakati mbalimbali ya kuimarisha
ukusanyaji wa mapato ili kupunguza utegemezi. Moja ya hatua muhimu
itakayotekelezwa katika mwaka 2013/14 ni kuangalia upya misamaha ya kodi kwa
lengo la kuipunguza. Hatua nyingine zitakazochukuliwa ni pamoja na:
(i)
Kupunguza misamaha ya kodi kwa kufuta msamaha wa kodi
ya ongezeko la thamani kwenye huduma za utalii. Aidha, Sheria ya Uwekezaji itafanyiwa
marekebisho ili kupunguza misamaha ya kodi na kubakiza misamaha yenye tija na
yenye kuchochea uwekezaji mkubwa katika sekta za uchumi za kimkakati;
(ii)
Kuendelea kuunga mkono jitihada za kuanzisha kituo kimoja cha kutoa huduma bandarini (one stop centre) katika bandari. Aidha,
Serikali itaendelea kutekeleza mpango wa kuanzisha One Stop Border Posts katika mipaka kwenye vituo vya Holili, Mutukula,
Sirari, Horohoro, Kabanga, Tunduma, Rusumo na Namanga;
(iii)
Kuendelea kuwajengea uwezo watumishi wa Serikali
wakiwemo wa Mamlaka ya Mapato ili kupata ujuzi wa kuthibiti mbinu za kukwepa
kodi zinazotumiwa na makampuni makubwa hasa katika sekta za mawasiliano, madini
na gesi ukiwemo ujuzi wa kukagua uhamishaji wa gharama yaani “transfer
pricing” hivyo kudhibiti mianya ya kupotea kwa mapato;
(iv)
Mamlaka ya Mapato Tanzania inaendela kuimarisha
matumizi ya mashine za kieletroniki za kutoa risiti (Electronic Fiscal Devices-EFDs) ambazo zimeunganishwa moja kwa
moja na Mamlaka kwa mtandao wa kompyuta ili kuhakikisha kuwa Serikali inapata
mapato yake stahiki. Aidha, Mashine hizi
zinasimamiwa kupitia mtandao wa kielektroniki ambapo hupeleka moja kwa moja
taarifa kwenye hifadhi kuu ya Mamlaka kila siku.
(v)
Kuwajengea uwezo watumishi kwa kutoa mafunzo ya muda
mfupi na mrefu ndani na nje ya nchi, hususan katika sekta ya gesi, mafuta na
madini ili kusimamia ipasavyo mapato yatokanayo na rasimali hizo; na
(vi)
Serikali
kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania itaanzisha mfumo mpya ujulikanao kama Revenue Gateway ambao utaanza kutumika
rasmi kuanzia tarehe 1 Julai 2013. Mfumo huo unalenga kuboresha mifumo iliyopo
ya ulipaji kodi na upatikanaji wa taarifa za malipo ya kodi kwa njia ya
mtandao. Aidha, mfumo huo utarahisisha uhamishaji wa fedha kutoka kwenye benki
za biashara hadi Mfuko Mkuu wa Serikali. Vilevile, mlipakodi atalazimika kujisajili kwa
ajili ya kufanya malipo kupitia tovuti ya Mamlaka ya Mapato Tanzania kabla ya
kulipa kupitia mfumo wa Tanzania
Interbank Settlement System (TISS). Mtumiaji
wa mfumo huu atanufaika kwa kupata
taarifa kwa njia ya barua pepe kuhusu malipo yake ya kodi aliyofanya.
81.
Mheshimiwa
Spika, Sera za mapato
katika mwaka 2013/14, zinalenga kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ya
shilingi bilioni 11,154.1 sawa na asilimia 20.2 ya Pato la Taifa. Kati ya kiasi
hicho, mapato ya kodi ni shilingi bilioni 10,412.9, na mapato yasiyo ya kodi ni
shilingi bilioni 741.1. Mapato yanayotokana na vyanzo vya Halmashauri ni
shilingi bilioni 383.5 sawa na asilimia 0.7 ya Pato la Taifa.
Mikopo ya Ndani
82.
Mheshimiwa Spika, Serikali bado ina changamoto ya kugharamia miradi ya
maendeleo kwa kutegemea mapato ya ndani. Ili kukabiliana na changamoto hiyo,
Serikali itakopa kutoka soko la ndani shilingi bilioni 552.3, sawa na asilimia
moja ya Pato la Taifa kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Aidha, katika
mwaka 2013/14, Serikali itakopa shilingi bilioni 1,147.6 kwa ajili ya kulipia
hatifungani na dhamana za Serikali za muda mfupi zinazoiva.
Misaada na Mikopo ya Masharti
Nafuu
83.
Mheshimiwa
Spika, Washirika wa
Maendeleo wamekuwa wakichangia katika bajeti ya matumizi ya maendeleo. Katika
mwaka 2013/14, Serikali inatarajia kupata misaada na mikopo yenye masharti
nafuu kiasi cha shilingi bilioni 3,855.2 kutoka kwa Washirika wa Maendeleo.
Kati ya fedha hizo, misaada na mikopo ya kibajeti ni shilingi bilioni 1,163.1; misaada
na mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo ni shilingi bilioni 2,191.6; na
mifuko ya kisekta ni shilingi bilioni 500. Aidha, Serikali itaendelea kusimamia matumizi
ya fedha za Washirika wa Maendeleo na kuhakikisha zinaleta ufanisi na tija.
84.
Mheshimiwa
Spika, kutokana
na juhudi zao za kuchangia maendeleo yetu, naomba kuwatambua na kuwashukuru
Washirika wa Maendeleo yetu kama ifuatavyo: Nchi za Canada,
China, Denmark, Finland, Hispania, India, Ireland, Italia, Japani, Korea ya
Kusini, Marekani, Norway, Sweden, Ubelgiji, Ufaransa, Uholanzi, Uingereza,
Ujerumani, na Uswisi, pia taasisi mbalimbali za Kimataifa ikiwemo Benki ya
Maendeleo ya Afrika, Benki ya Dunia, BADEA, Global Funds, OPEC Fund, Saudi
Fund, Umoja wa Ulaya, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Mashirika ya Umoja
wa Mataifa. Tunawashukuru sana na tunathamini michango yao.
Mikopo
ya nje yenye Masharti ya Kibiashara
85.
Mheshimiwa
Spika, kwa kuzingatia
mahitaji makubwa ya kuendeleza miradi ya maendeleo kwa mwaka 2013/14 na
changamoto za upatikanaji wa mapato ya ndani, Serikali itakopa kutoka nje
mikopo yenye masharti nafuu ya kibiashara shilingi bilioni 1,156.4, sawa na
Dola za Marekani milioni 700. Mikopo hiyo itatumika kugharamia miradi ya
maendeleo kama ilivyoainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2013/14.
Uamuzi wa kuendelea kukopa kwa masharti nafuu ya kibiashara unazingatia
uhimilivu wa Deni la Taifa uliopo.
Sera za Matumizi
86.
Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2013/14, Serikali itatekeleza sera za matumizi zifuatazo:-
(i)
Kuwianisha matumizi na
mapato yanayotarajiwa;
(ii)
Nakisi ya bajeti
(ikijumuisha misaada) haitazidi asilimia 5.0 ya Pato la Taifa;
(iii)
Mafungu yatazingatia
viwango vya matumizi vitakavyoidhinishwa na Bunge;
(iv)
Kutenga fedha za kutosha
katika kutekeleza miradi ya vipaumbele vilivyoainishwa katika Mpango wa
Maendeleo; na
(v)
Kuzingatia Sheria ya Fedha za
Umma na Sheria ya Ununuzi wa Umma.
87.
Mheshimiwa Spika, matumizi ya
kawaida kwa mwaka 2013/14 yanalenga
katika kufanikisha maeneo yafuatayo: kugharamia
nyongeza ya mishahara pamoja na kulipa mishahara kwa wakati; kuboresha huduma
za kiuchumi na maendeleo ya jamii; kukamilisha mchakato wa upatikanaji wa
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; kuendelea na utoaji wa vitambulisho vya
Taifa; kukamilisha uchambuzi wa takwimu za sensa ya watu na makazi; maandalizi
ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015; na kuendelea kulipa madeni ya ndani na nje
yaliyoiva pamoja na madai mbalimbali ya watumishi na wazabuni yaliyohakikiwa.
88.
Mheshimiwa spika, katika
bajeti ya mwaka 2012/13, Serikali ililenga kupunguza matumizi yasiyo ya lazima
katika maeneo mbalimbali kama vile semina, usafiri wa ndani na nje, ununuzi wa
samani, maonesho mbalimbali na katika magari. Matokeo ya hatua hizi yameleta
mafanikio kadhaa ikiwemo yafuatayo: semina na warsha zimepunguzwa; manunuzi ya magari
mapya yamepunguzwa na yananunuliwa kwa kibali cha Waziri Mkuu tu na ukubwa wa
injini umepunguzwa na kubaki zenye ukubwa uliokubalika (cc 3,000 au chini ya
hapo); maonyesho pia yamepunguzwa mfano maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma
hayakufanyika mwaka 2012/13; ununuzi wa samani kutoka nje umepungua.
89.
Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2013/14, Serikali itaendelea kudhibiti matumizi yake katika maeneo
mbalimbali ikiwemo kutumia malipo ya simu kabla ya huduma; kutumia utaratibu wa
ununuzi wa magari wa pamoja ambao utapunguza gharama za ununuzi; kupunguza
matumizi ya magari ya Serikali kwa kuanzisha utaratibu wa kuwakopesha magari
watumishi wa Serikali wanaostahili; kuoanisha kanuni za ununuzi wa umma za
Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kwa lengo la kuimarisha ununuzi katika
Mamlaka za Serikali za Mitaa; na kuhimiza matumizi ya samani zinazotengenezwa
nchini.
90.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa
matumizi ya maendeleo, bajeti itazingatia kutekeleza vipaumbele vya Mpango wa Kwanza
wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao mwaka 2013/14 unaingia mwaka wa tatu wa
utekelezaji kama ifuatavyo:
(i)
Miundombinu: -
miundombinu ya nishati; usafirishaji (barabara, reli, viwanja vya ndege,
usafiri wa majini ); TEHAMA; maji safi na maji taka na umwagiliaji;
(ii)
Kilimo: – ikijumuisha mazao ya
chakula na biashara, malighafi ya viwandani, ufugaji, uvuvi na misitu;
(iii)
Viwanda: – vinavyotumia malighafi
hususan za ndani, na kuongeza thamani, viwanda vikubwa vya mbolea na saruji,
viwanda vya kanda maalum za kiuchumi, kielektroniki na TEHAMA;
(iv)
Maendeleo
ya rasilimali watu na Ujuzi kwa kutilia mkazo sayansi, teknolojia na ubunifu;
(v)
Uendelezaji
wa huduma za utalii, biashara na fedha; na
(vi)
Huduma za jamii:
kuimarisha upatikanaji na ubora wa huduma za jamii.
91.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka
2013/14, Serikali itaendelea kuboresha mfumo wa ugawaji wa fedha kwenye Mamlaka
za Serikali za Mitaa kwa kuzingatia sera ya ugatuaji wa madaraka na rasilimali.
Aidha, Serikali itaimarisha mifumo ya ndani ya mapato na matumizi kwa kutoa
miongozo mahsusi ya ukaguzi wa ndani, kuimarisha utendaji wa kamati za ukaguzi,
kutoa mafunzo ya usimamizi na uimarishaji mifumo ya udhibiti wa ndani kwa
Wakurugenzi wa Halmashauri. Vile vile, Mamlaka za Serikali za Mitaa
zitawezeshwa kuainisha uwezo wa pato la kila Halmashauri na fursa zilizopo
katika ukusanyaji wa mapato ya ndani; na kujenga uwezo wa Halmashauri katika
matumizi ya mfumo wa IFMS; kuhuisha baadhi ya vyanzo vya mapato ya ndani ili
kuongeza mapato; kuboresha mfumo wa uthamini wa majengo kwa kutumia kanuni za
jumla; kuhamasisha Halmashauri kutumia teknolojia rahisi ya mitandao ya simu za
mkononi katika kufanya malipo.
92.
Mheshimiwa
Spika,
ili kuwezesha Wizara, Idara zinazojitegemea, Mikoa na Mamlaka ya Serikali za
Mitaa kutekeleza majukumu yao, Serikali itahakikisha kwamba mafungu yanapata
fedha kama ilivyoidhinishwa na Bunge lako tukufu.
93.
Mheshimiwa
Spika, kutokana na
mashauriano ya Kamati ya Bunge ya Bajeti na Serikali, pamoja na mahitaji
mengine ya Serikali jumla ya shilingi bilioni 538.6 zimeongezwa katika Bajeti
hii kama mchanganuo unavyoonesha.
MCHANGANUO WA FEDHA AMBAZO ZIMETOLEWA NA SERIKALI
KUPITIA
MASHAURIANO NA KAMATI YA BUNGE YA BAJETI KWA MWAKA WA
FEDHA 13/14
FUNGU
|
MAELEZO
YA FUNGU
|
BAJETI
KABLA YA NYONGEZA YA MWAKA 2013/14
|
FEDHA
ZILIZOTOLEWA NA SERIKALI
|
JUMLA
BAJETI YA FUNGU IKIJUMUISHA NYONGEZA
|
MAELEZO
|
15
|
Tume
ya Usuluhishi na Uamuzi
|
1,924,748,000
|
350,000,000
|
2,274,748,000
|
Fedha
kwa ajili ya shughuli za usuluhishi wa migogoro ya wafanyakazi
|
21
|
Hazina
|
1,416,332,728,000
|
5,600,000,000
|
1,421,932,728,000
|
Fedha
kwa ajili ya kugharamia uchambuzi wa mapato ya ziada
|
35
|
Idara ya Kurugenzi ya
Mashtaka
|
13,011,796,000
|
10,000,000,000
|
23,011,796,000
|
Fedha
kwa ajili ya matumizi ya kawaida
|
40
|
Mfuko
wa Mahakama
|
141,696,825,000
|
20,000,000,000
|
161,696,825,000
|
Fedha
za maendeleo
|
43
|
Wizara
ya Kilimo, Chakula na Ushirika
|
328,134,608,000
|
21,150,000,000
|
349,284,608,000
|
Fedha
za ruzuku ya mbolea
|
44
|
Wizara
ya Viwanda na Biashara
|
78,492,632,000
|
30,000,000,000
|
108,492,632,000
|
Fedha
za maendeleo kwa ajili ya Kurasini Logistic Hub-EPZ Development
|
49
|
Wizara
ya Maji
|
398,395,874,000
|
184,500,000,000
|
582,895,874,000
|
Fedha
za matumizi ya kawaida na maendeleo kwa ajili ya miradi ya maji vijijini
|
53
|
Wizara
ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto
|
21,870,448,700
|
2,000,000,000
|
23,870,448,700
|
Fedha
za maendeleo kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo wa Wanawake
|
70-95
|
HALMASHAURI
MBALIMBALI
|
1,247,049,476,000
|
10,800,000,000
|
1,257,849,476,000
|
Matumizi
ya kawaida Kutokana na ongezeko la makusanyo ya mapato kwa Halmashauri
|
58
|
Wizara
ya Nishati na Madini (REA)
|
1,102,429,129,000
|
186,900,000,000
|
1,289,329,129,000
|
Fedha
za maendeleo kwa ajili ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA)
|
62
|
Wizara
ya Uchukuzi
|
491,105,994,000
|
38,300,000,000.0
|
529,405,994,000
|
Fedha
za maendeleo kwa ajili ya miundombinu ya Reli na Mtaji kwa TAZARA
|
96
|
Wizara
ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
|
21,328,045,000
|
9,000,000,000
|
30,328,045,000
|
Fedha
za maendeleo kwa ajili ya kuongeza usikivu TBC shilingi bilioni 6 na Mfuko wa
Maendeleo wa Vijana shilingi bilioni 3
|
99
|
Wizara
ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi
|
47,180,225,000
|
20,000,000,000
|
67,180,225,000
|
Fedha
za maendeleo kwa ajili ya maendeleo ya mifugo na uvuvi
|
JUMLA
|
5,308,952,528,700
|
538,600,000,000
|
5,847,552,528,700
|
94.
Mheshimiwa
Spika, kwa hali hiyo,
Serikali itaongeza juhudi za kukusanya mapato ya ndani, kuharakisha majadiliano
na Washirika wa Maendeleo na wakopeshaji mbalimbali katika kutafuta mikopo na
misaada kwa wakati. Ninatoa wito kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Mikoa na
Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha kwamba wanatimiza masharti na taratibu
za kupata fedha zilizoidhinishwa na Bunge.
Mfumo Mpya wa Uandaaji na Utekelezaji wa Vipaumbele vya Miradi ya
Maendeleo
95.
Mheshimiwa
spika, kama
ilivyoelezwa hapo awali kwenye hotuba ya Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais –
Mahusiano na Uratibu, Mh. Stephen Masatu Wassira (Mb), Serikali imeainisha
maeneo ya kimkakati ambayo yatafungua fursa ya mapinduzi ya kiuchumi na kuleta
matokeo makubwa kiuchumi na kijamii kwa muda mfupi. Maeneo hayo ni utafutaji wa
mapato, kilimo, maji, elimu, nishati na miundombinu ya uchukuzi. Serikali imedhamiria kutekeleza miradi kwenye maeneo
hayo katika kipindi cha muda wa kati. Utekelezaji madhubuti wa vipaumbele
hivi utafanikisha kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ya
Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati.
96.
Mheshimiwa
spika, ili kuongeza ufanisi
katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Serikali imeweka mikakati ya
kuongeza nidhamu ya kupanga na kutekeleza miradi ya mendeleo ili kupata matokeo
yanayowiana na thamani halisi ya fedha. Kwa kuzingatia hilo, Serikali
imeainisha maeneo makuu sita kama nilivyoeleza hapo awali ambayo yatazingatiwa
katika kipindi cha miaka mitatu ijayo. Aidha, kama mnavyofahamu, Serikali
imeunda chombo (Presidential Delivery Bureau) kitakachoratibu, kufuatilia na
kutathmini utekelezaji wa miradi katika sekta zilizobainishwa.
97.
Mheshimiwa
spika, katika
mwaka 2013/14, Serikali imeweka kipaumbele katika kutatua kero ya maji kwa
wananchi ambapo shilingi bilioni 747.6 zimetengwa kwa ajili ya kuimarisha
miundombinu ya maji mijini na vijijini. Katika kipindi cha muda wa kati, Serikali
itaendelea na juhudi za kuimarisha upatikanaji wa maji safi na salama.
98.
Mheshimiwa
Spika, katika kuimarisha miundombinu
ya uchukuzi ambayo inajumuisha barabara, reli, madaraja, bandari na viwanja vya
ndege, Serikali imetenga shilingi bilioni 2,169.0 katika mwaka 2013/14
ikilinganishwa na shilingi bilioni 1,940.0 mwaka 2012/13. Kati ya fedha hizo
zilizotengwa mwaka 2013/14, shilingi bilioni 196.8 ni kwa ajili ya kuimarisha
miundombinu ya reli ikilinganishwa na shilingi bilioni 134.2 zilizotengwa mwaka
2012/13, sawa na ongezeko la asilimia 46.6.
Aidha, Serikali imedhamiria kuongeza bajeti na kuchukua hatua za
kuishirikisha sekta binafsi katika kuimarisha miuondombinu ya reli.
99.
Mheshimiwa
Spika, katika
kuendeleza sekta ya nishati na madini, juhudi zitaelekezwa katika kuongeza
uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme ambapo jumla ya shilingi
bilioni 1,426.9 zimetengwa kwa ajili hiyo ikilinganishwa na shilingi bilioni
731.8 mwaka 2012/13.
Sekta ya Fedha
100.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Serikali itachukua hatua zifuatazo
katika kuboresha sekta ya fedha:-
(i) Kutunga sheria ya Mfumo wa Malipo nchini kwa
ajili ya kuwa na utaratibu wa usimamizi wa mifumo ya malipo nchini ili
kuboresha matumizi ya kielektroniki katika kufanya malipo, hususan kwa kutumia
simu za mikononi, huduma za benki kwa njia ya mtandao, vituo vya mauzo na
mashine za kutolea fedha (ATM);
(ii) Kuandaa Sera ya Bima ya Taifa; na
(iii) Kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Taasisi
ndogo za Fedha, 2002.
101.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa
fedha 2013/14 Serikali itaendelea na hatua za kuboresha sekta ya hifadhi ya
jamii kwa kutekeleza kazi zifuatazo:-
(i) Kuandaa kanuni na miongozo ambayo itajikita
katika kuboresha sekta ya hifadhi ya jamii na kuifanya kuwa endelevu na yenye
mchango katika maendeleo ya wanachama wa mifuko na nchi kwa ujumla;
(ii) Kusajili mifuko, mameneja uwekezaji (Fund Managers) na watunza mali (Custodians) kwa ajili ya kutenganisha
majukumu kwenye uendeshaji wa Mifuko ili kuleta ufanisi zaidi; na
(iii) Kutoa elimu kwa umma kuhusu sekta ya hifadhi ya
jamii.
Mikakati ya Kukabiliana na Changamoto
102.
Mheshimiwa
Spika, kutokana na
changamoto nilizozieleza awali, serikali imeandaa mikakati ya kukabiliana nazo
katika mwaka 2013/14 kama ifuatavyo: kuhusu suala la tija katika kilimo, Serikali
itaboresha mfumo wa kilimo, mifugo na uvuvi uwe wa kibiashara badala ya ule wa
kujikimu; kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji; kuongeza upatikanaji na
utumiaji wa pembejeo za kilimo; kuimarisha huduma za ugani; upatikanaji wa
mikopo kwa wakulima, kusimamia upatikanaji wa masoko; na kuboresha mazingira ya
uwekezaji katika sekta ya kilimo.
103.
Mheshimiwa
Spika, kuhusu matumizi ya
fedha za umma, Serikali itaendelea kuwajengea uwezo watumishi wa kada za
uhasibu, ununuzi, uhakiki mali na ukaguzi wa ndani. Aidha, Serikali
itaimarisha, usimamizi wa mali za Serikali na kufanya uhakiki wa mali za
Serikali katika Wizara, Mikoa na Halmashauri ili kuboresha daftari la mali za
Serikali na kubaini mali zisizokuwa na tija kwa ajili ya kuzifuta.
104.
Mheshimiwa
Spika, katika hatua za
kudhibiti matumizi, Serikali itapunguza matumizi kwenye maeneo mbayo
hayataathiri utoaji wa huduma za msingi. Aidha, Serikali itapitia kanuni za
ununuzi ili kuhakikisha kuwa huduma na vifaa vinavyonunuliwa vinaendana na
thamani ya fedha. Serikali itaendelea kuhamasisha matumizi ya TEHAMA katika
kupunguza gharama za uendeshaji.
105.
Mheshimiwa
Spika, katika kutekeleza
Sheria ya ununuzi wa umma, kumekuwepo na kanuni za ununuzi tofauti kati ya
zinazotumika katika Serikali Kuu na zile zinazotumika katika Serikali za Mitaa.
Uzoefu uliopo unaonesha kuwa kanuni hizo zimekuwa na changamoto nyingi za
kiutekelezaji. Ili kutatua tatizo hilo, Serikali imepanga kuoanisha kanuni za
ununuzi wa umma zinazotumika katika Serikali Kuu na zile zinazotumika katika
Serikali za Mitaa. Hatua hii itaboresha usimamizi na udhibiti wa ununuzi wa
umma. Ili kuhakikisha ununuzi wa umma unatekelezwa kulingana na Sera na Sheria
husika, Wizara ya Fedha itasimamia shughuli hiyo.
106.
Mheshimiwa
Spika, katika kuimarisha
usimamizi wa Deni la Taifa, Serikali inakamilisha taratibu za kuanzisha Idara
ya Usimamizi wa Deni la Taifa ndani ya Wizara ya Fedha ambayo itaanza kazi
mwaka 2013/14. Aidha, Serikali inapitia upya Mkakati wa Kusimamia Deni laTaifa
wa mwaka 2002 pamoja na kuifanyia marekebisho Sheria ya Mikopo, Dhamana na
Misaada ya mwaka 1974 iliyorekebishwa mwaka 2004, ili kutambua uanzishwaji wa
Idara ya Kusimamia Deni la Taifa kwa mujibu wa Sheria na kuiboresha ili kwenda
na wakati.
107.
Mheshimiwa
Spika, katika
kuhakikisha kwamba Bajeti ya Serikali inatekelezwa kama ilivyokusudiwa,
Serikali itawajengea uwezo watumiaji wa Mfumo wa Malipo (IFMS) kuhusu maeneo
yaliyoboreshwa katika toleo la Epicor 9.02; kuhakikisha mihadi na malipo yote
yanafanyika kwa kutumia mfumo wa IFMS; na kufanya ukaguzi wa ununuzi kwenye
Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na wakala wa Serikali, Mikoa na Mamlaka
za Serikali za Mitaa. Aidha, Serikali itaweka utaratibu wa kuibua miradi,
kuifanyia upembuzi yakinifu na kuichambua kabla haijatengewa fedha katika bajeti
ya mwaka husika ili kuhakikisha kuwa miradi inatekelezwa kwa wakati na Serikali
inapata thamani halisi ya fedha.
108.
Mheshimiwa
Spika, kuhusu kutumia
fursa za kijiografia katika ukuzaji wa uchumi, Serikali itaendelea kuboresha
miundombinu ya usafirishaji hususan barabara, reli, bandari, na viwanja vya
ndege; kuongeza upatikanaji wa nishati ya umeme; kuboresha huduma za utalii; kupunguza
gharama za kufanya biashara nchini ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje; na
kuimarisha ulinzi na usalama katika ngazi zote.
109.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka
2013/14, Serikali itaendelea kudhibiti mfumuko wa bei kwa kuhamasisha
uzalishaji na usambazaji sawia wa mahitaji muhimu kama vile chakula, mafuta ya
nishati, sukari, vifaa vya ujenzi na huduma za usafiri. Aidha, Serikali itatumia
hifadhi ya taifa ya chakula kusambaza chakula katika masoko kwa ajili ya
kudhibiti bei.
110.
Mheshimiwa
Spika, katika
kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi, Serikali itaimarisha
kamati za kisekta za kuratibu mifumo ya kuhimili na kukabili athari za
mabadiliko ya tabianchi. Aidha, Serikali itaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa
wa Mabadiliko ya Tabianchi; kuhimiza wananchi kutumia nishati mbadala;
kuhamasisha wananchi kupanda mazao yanayostahimili ukame; kutumia chakula
kilichopo kwa tija na uangalifu ili kukidhi mahitaji ya msingi; kuchukua
tahadhari ya upatikanaji wa umeme wa uhakika; na kuelimisha wananchi wachukue
tahadhari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuepuka uhaba wa chakula.
V.
MABORESHO YA MFUMO WA KODI, ADA, TOZO NA
HATUA NYINGINE ZA MAPATO
111.
Mheshimiwa
Spika, Serikali itaendelea kuchukua
hatua za makusudi ili kuongeza mapato na kupanua wigo wa kodi hususan kubuni
vyanzo vipya vya mapato. Aidha, itaendelea pia kupunguza misamaha ya kodi
katika muda wa kati kutoka asilimia 4.3 ya Pato la Taifa katika mwaka 2011 hadi
kufikia walau asilimia 1. Hivi karibuni uchambuzi wa misamaha ya kodi umeonesha
kwamba, misamaha mingi ya kodi imetokana na kuongezeka kwa uwekezaji kwenye
maeneo ya kimkakati kupitia Kituo cha Uwekezaji. Aidha, Serikali ilisamehe kodi
na ushuru kwenye mafuta ya kuendeshea mitambo ya umeme wa dharura na pia
kusamehe kodi na ushuru kwenye uagizaji wa sukari na mchele ili kuziba pengo la
upungufu wa bidhaa hizo hapa nchini. Vile vile misamaha pia imekuwa ikitolewa
kwa wawekezaji katika Maeneo Maalum ambao wanazalisha bidhaa zinazouzwa nje
(EPZ na SEZ), ujenzi wa miundombinu na baadhi ya miradi inayofadhiliwa na
wahisani ili kuwezesha utekelezaji wa miradi hiyo yenye gharama kubwa kwa
ukamilifu.
112.
Mheshimiwa
Spika, juhudi za kupunguza misamaha zitaelekezwa zaidi katika kupunguza misamaha isiyo na tija na yenye
uwezekano wa kutumika vibaya. Kwa sasa Serikali inakamilisha mapitio ya Sheria
ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ili kupunguza misamaha. Aidha, Serikali
inakamilisha kazi ya utafiti wa kuchambua misamaha yote ya kodi ili kuleta
mapendekezo ya kupunguza misamaha isiyo na tija.
113.
Mheshimiwa
Spika, kufuatia kuendelea
kufanya vibaya katika ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi, Serikali iko katika
hatua nzuri ya kukamilisha utafiti wa kuangalia vyanzo vya mapato na kuwianisha
mifumo inayotumika katika ukusanyaji wa mapato hayo. Mapendekezo ya utafiti huo
yatazingatiwa kwenye kipindi cha mwaka 2014/15.
114.
Mheshimiwa
Spika, ili kufikia malengo ya
kiuchumi na mapato katika mwaka
2013/14, ninapendekeza kufanya maboresho ya sheria mbalimbali za kodi kama
ifuatavyo:
a. Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148;
b. Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332;
c. Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147;
d. Sheria ya Ushuru wa Mafuta, SURA, 220;
e. Sheria
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, SURA 82
f. Sheria ya Usalama Barabarani, SURA, 168;
g. Sheria ya Petroli (Petroleum Act) SURA, 392;
h. Sheria
ya Uwekezaji Tanzania, SURA, 38;
i. Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ya
mwaka 2004;
j. Marekebisho mengine madogo madogo katika baadhi ya sheria
za kodi na Sheria nyingine mbalimbali; na
k. Marekebisho ya Ada na Tozo Mbalimbali za Wizara, Mikoa na
Idara zinazojitegemea.
(a)
Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148
115.
Mheshimiwa
Spika, napendekeza kufanya
marekebisho yafuatayo katika Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148
kama ifuatavyo: -
(i)
Kufuta msamaha wa
VAT unaotolewa kwenye huduma za utalii chini ya Jedwali la Pili la Sheria ya
Kodi ya Ongezeko la Thamani, Kipengele cha 14. Aidha, hatua hii itahusisha
huduma zifuatazo: (i) Tourist Guiding
(ii) Game driving (iii) Water Safaris (iv) Animal or bed watching (v) Park fees
(vi) Tourist Charter Services (vii) Ground Transport. Hatua hii inalenga
katika kutekeleza azma ya Serikali ya kupunguza misamaha ya kodi. Hata hivyo,
msamaha wa ushuru wa forodha utaendelea kutolewa kwenye vifaa mbalimbali
vinavyotumika katika kutoa huduma za utalii;
(ii)
Kutoa
msamaha wa VAT kwa wazalishaji wa nguo nchini zinazozalishwa kwa pamba ya ndani
kwa bidhaa na huduma zitakazotumika tu kwenye uzalishaji wa nguo hizo kupitia
jedwali la tatu la Sheria ya kodi ya Ongezeko la Thamani badala ya utaratibu wa
sasa wa kutoza VAT kwa wazalishaji kwa kiwango cha asilimia sifuri chini ya
Jedwali la kwanza la Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani “VAT”. Kwa hatua hii
mzalishaji wa nguo zinazotumia pamba ya hapa nchini hatalipa VAT kwenye
manunuzi ya pamba, umemr na malighafi za uzalishaji wa nguo hizo;
Hatua hizi katika Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa pamoja
zitaongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 48,977.60
(b)
Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332
116.
Mheshimiwa
Spika, napendekeza kufanya
marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332 kama ifuatavyo: -
(i)
Kupunguza
kiwango cha chini cha kutoza kodi ya mapato ya ajira kutoka asilimia 14 hadi
asilimia 13. Hatua hii inalenga katika kutoa nafuu ya kodi kwa mfanyakazi;
Viwango vya sasa na vile vinavyopendekezwa ni kama
ifuatavyo: -
Viwango
vya sasa
Jumla
ya Mapato
|
Kiwango
cha Kodi
|
Mapato
ya jumla yasiyozidi Shilingi 2,040,000/=
|
Asilimia
sifuri (0%)
|
Mapato
ya jumla yanayozidi Shilingi 2,040,000 lakini hayazidi shilingi 4,320,000/=
|
14%
ya kiasi kinachozidi Shilingi 2,040,000/=
|
Mapato
ya jumla yanayozidi Shilingi 4,320,000/= lakini hayazidi shilingi 6,480,000/=
|
Shilingi
319,200/= + 20% ya kiasi kinachozidi Shilingi 4,320,000/=
|
Mapato
ya jumla yanayozidi Shilingi 6,480,000/= lakini hayazidi shilingi 8,640,000/=
|
Shilingi
751,200/= + 25% ya kiasi kinachozidi Shilingi 6,480,000/=
|
Mapato
ya jumla yanayozidi Shilingi 8,640,000/=
|
Shilingi
1,291,200/= + 30% ya kiasi kinachozidi Shilingi 8,640,000/=
|
Viwango vinavyopendekezwa
Jumla ya Mapato
|
Kiwango cha Kodi
|
Mapato ya jumla yasiyozidi Shilingi 2,040,000/=
|
Asilimia sifuri (0%)
|
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 2,040,000 lakini
hayazidi shilingi 4,320,000/=
|
13% ya kiasi
kinachozidi Shilingi 2,040,000/=
|
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 4,320,000/= lakini
hayazidi shilingi 6,480,000/=
|
Shilingi 296,400/= + 20% ya kiasi kinachozidi Shilingi
4,320,000/=
|
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 6,480,000/= lakini
hayazidi shilingi 8,640,000/=
|
Shilingi 728,400/= + 25% ya kiasi kinachozidi Shilingi
6,480,000/=
|
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 8,640,000/=
|
Shilingi 1,268,400/= + 30% ya kiasi kinachozidi
Shilingi 8,640,000/=
|
(i)
Kuanzisha kodi ya zuio ya asilimia 10 ya
kamisheni (commission) ya usafirishaji wa fedha kwa njia ya simu za mkononi.
Kodi hiyo itakusanywa na kampuni za simu kutoka kwa wakala wanaotoa huduma za
kusafirisha fedha kupitia simu za mkononi;
(ii)
Kutoza kodi ya zuio kwa kiwango cha asilimia
5 kwenye malipo yatokanayo na huduma mbali mbali kama vile huduma za ushauri wa
kitaalamu na nyinginezo (Consultancy services and other services). Kodi hii
itatozwa bila kujali kama kuna Namba ya Utambulisho wa Mlipa kodi (TIN) au la.
Lengo la hatua hii ni kudhibiti na kulinda mapato ya Serikali;
(ii)
Kutoza kodi ya zuio kwenye bidhaa
zinazonunuliwa na Serikali na Taasisi zake kwa kiwango cha asilimia 2 bila
kujali kama kuna Namba ya Utambulisho wa Mlipa kodi (TIN) au la. Lengo la hatua
hii ni kudhibiti na kulinda mapato ya Serikali;
(iii)
Kufuta msamaha wa kodi ya zuio kwenye
ukodishaji wa ndege kwa walipa kodi wasio wakazi (non-resident). Hatua hii
inalenga katika kupunguza misamaha ya kodi na kuhuisha mapato ya Serikali;
Hatua hizi za Kodi ya Mapato kwa pamoja zitaongeza mapato
ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni
131,686.
(c)
Sheria
ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147
117.
Mheshimiwa
Spika, napendekeza kufanya marekebisho katika
Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147 kama ifuatavyo:-
(i)
Kuongeza kiwango cha Ushuru wa Bidhaa kwenye
magari yasiyo ya uzalishaji (Non-Utility Motor Vehicles) ya umri wa zaidi ya
miaka 10 kutoka asilimia 20 hadi asilimia 25. Hatua hii inalenga katika
kupunguza uagizaji wa magari chakavu, kulinda mazingira na kupunguza ajali;
(ii)
Kuanzisha kiwango kipya cha Ushuru wa Bidhaa
cha asilimia 5 kwenye magari ya uzalishaji (Utility Motor Vehicles) yenye umri
wa zaidi ya miaka 10 yanayotambuliwa katika HS Code 87.01, 87.02 na 87.04.
Hatua hii haitahusisha magari chini ya HS Code
8701.10.00; na HS Code 8701.90.00 ambayo kimsingi ni matrekta
yaliyounganishwa; na magari yasiyounganishwa chini ya HS Code 8702.10.11;
8702.10.21, 8702.10.91; 9702.90.11, 8702.90.21; 8702.90.91; HS Code 87.04;
8704.10.10; 8704.21.10; 8704.22.10; 8704.23.10; 8704.31.10, na 8704.32.10,
8704.90.10. Lengo la kuanzisha kiwango kipya cha ushuru ni kupunguza uagizaji
wa magari chakavu, kulinda mazingira na kupunguza ajali. Aidha, matrekta na
magari yasiyounganishwa hayatatozwa ushuru huu kwa nia ya kuhamasisha uwekezaji
kwenye sekta ya uunganishaji wa magari na hivyo kuongeza ajira na mapato ya
serikali;
(iii)
Kurekebisha viwango vya Ushuru wa bidhaa
kwenye mafuta ya Petroli kama ifuatavyo: -
a. Mafuta
ya Dizeli kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 215 kwa lita hadi shilingi 217
kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 2 tu;
b. mafuta
ya Petroli kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 339 kwa lita hadi shilingi 400
kwa lita; na,
c. mafuta
ya Taa kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 400.30 kwa lita kwa mafuta ya taa
hakitabadilika;
(iv)
Kutoza ushuru wa bidhaa wa asilimia kati ya
10 hadi asilimia 25 kwenye bidhaa mbalimbali zinazozalishwa au kuingizwa
nchini kama vile; Mazulia, vipodozi,
mafuta ya kujipaka, bidhaa na mifuko ya ngozi, bunduki na risasi, boti za
kifahari, ndege na helikopta;
(v)
Kuanzisha kiwango cha Ushuru wa bidhaa wa
asilimia 15 kwenye samani zinazoagizwa kutoka nje ya nchi, zinazotambulika
katika HS Code 94.03. Hatua hii inalenga katika kulinda na kuhamasisha
uzalishaji wa samani kwa kutumia mbao zinazozalishwa hapa nchini. Aidha hatua
hii itachochea ukuaji wa ajira na kuongeza mapato ya Serikali;
(vi)
Kutoza Ushuru wa bidhaa wa asilimia 14.5
kwenye huduma zote (all mobile phone
services) za simu za kiganjani/mkononi badala ya muda wa maongezi tu (airtime
alone). Katika ushuru huu asilimia 2.5 zitatumika kugharamia elimu hapa nchini.
(vii)
Kuongeza wigo wa kutoza Ushuru wa bidhaa
kwenye huduma za simu za mezani (zinazojulikana
kama simu za TTCL) na zisizokuwa na waya;
(viii)
Kurekebisha viwango maalum (specific rates)
vya Ushuru wa bidhaa zisizokuwa za mafuta kama vile vinywaji baridi, mvinyo, pombe, vinywaji vikali, sigara
n.k. kwa
asilimia 10 kama ifuatavyo:-
(a) Vinywaji baridi, kutoka shilingi 83 kwa lita hadi
shilingi 91 kwa lita; Hilo ni ongezeko la shilingi 8 tu kwa lita;
(b) Ushuru wa bidhaa kwenye maji ya matunda (Juisi)
iliyotengenezwa kwa matunda yanayozalishwa hapa nchini kutoka shilingi 8 kwa
lita hadi shilingi 9 kwa lita, sawa na ongezeko la shilingi 1 tu kwa lita;
(c) Ushuru wa bidhaa kwenye Juisi iliyotengenezwa kwa
matunda ambayo hayazalishwi hapa nchini kutoka shilingi 100 kwa lita hadi
shilingi 110 kwa lita, sawa na ongezeko la shilingi 10 kwa lita;
(d) Bia inayotengenezwa kwa nafaka ya hapa nchini na
ambayo haijaoteshwa, kutoka shilingi 310 kwa lita hadi shilingi 341 kwa lita,
sawa na ongezeko la shilingi 31 kwa lita;
(e) Bia
nyingine zote, kutoka shilingi 525 kwa lita hadi shilingi 578 kwa lita; yaani
ongezeko la shillingi 51 kwa lita;
(f) Mvinyo
uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa ndani ya nchi kwa kiwango kinachozidi
asilimia 75, kutoka shilingi 145 kwa lita hadi shilingi 160 kwa lita, sawa na ongezeko la shilingi 15 kwa
lita moja;
(g) Mvinyo
uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi
asilimia 25, kutoka shilingi 1,614 kwa lita hadi shilingi 1,775 kwa lita. sawa na ongezeko la shilingi 161
kwa lita;
(h) Vinywaji
vikali, kutoka shilingi 2,392 kwa lita hadi shilingi 2,631 kwa lita; sawa na
ongezeko la shilingi 239 kwa lita moja;
(i) Ushuru wa bidhaa kwenye maji yanayozalishwa viwandani
hautaongezeka;
(ix)
Kurekebisha viwango vya ushuru wa bidhaa
kwenye sigara kama ifuatavyo:-
(a)
Sigara zisizo na kichungi na
zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha
angalau asilimia 75, kutoka shilingi 8,210 hadi shilingi 9,031 kwa sigara elfu
moja; sawa na ongezeko la senti 82 tu kwa sigara 1;
(b)
Sigara zenye kichungi na zinazotengenezwa
kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia
75, kutoka shilingi 19,410 hadi shilingi 21,351 kwa sigara elfu moja; ikiiwa ni
ongezeko la shilingi 1 na senti 94 kwa sigara moja;
(c)
Sigara nyingine zenye sifa tofauti na (a) na
(b) kutoka shilingi 35,117 hadi shilingi 38,628 kwa sigara elfu moja; ikiwa ni
ongezeko la shilingi 3 na senti 50 tu kwa sigara moja;
(d)
Tumbaku ambayo iko tayari kutengeneza sigara
(“cut filler’) kutoka shilingi 17,736 hadi shilingi 19,510 kwa kilo; na
(e)
Ushuru wa Bidhaa kwa “Cigar” unabaki kuwa
asilimia 30.
Hatua
hizi katika Ushuru wa Bidhaa kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya
Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 510,017.50.
(d)
Sheria ya Ushuru wa Mafuta, SURA, 220;
118.
Mheshimiwa
Spika, ili kuongeza uwezo wa
Serikali katika kugharamia ukarabati wa miundo mbinu ya barabara ambayo ni
muhimu katika kuleta maendeleo na kujenga uchumi hapa nchini, napendekeza
kufanya marekebisho katika Sheria
ya Ushuru wa Mafuta ya Petroli, SURA, 220 kama ifuatavyo: -
(i)
Kuongeza kiwango cha Ushuru wa mafuta (fuel
levy) kutoka shilingi 200 kwa lita hadi shilingi 263 kwa lita, sawa na ongezeko
la shilingi 63 kwa lita.
Hatua
hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 155,893.50
(e)
Sheria
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, SURA 82
119.
Mheshimiwa
Spika, napendekeza kufanya marekebisho katika
Sheria ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, SURA 82 kama ifuatavyo:-
(iv)
Kupunguza tozo ya kuendeleza mafunzo ya
ufundi stadi (Skills Development Levy
“SDL”) kutoka kwenye kiwango cha sasa cha
asilimia 6 hadi kiwango cha asilimia 5. Aidha, sambamba na kupunguza kiwango
cha sasa cha SDL, Taasisi za Serikali zisizotegemea bajeti ya Serikali kwa
kiwango kikubwa katika kujiendesha pia zitalipa tozo hii.
Hatua
hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 28,213.90
(f)
Sheria ya Usalama Barabarani, SURA, 168;
120.
Mheshimiwa
Spika, napendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Usalama Barabarani, SURA, 168
ili kuongeza viwango vya Ada ya mwaka ya leseni za Magari (Annual Motor vehicle Licence Fee) kama
ifuatavyo: -
(i) Gari lenye ujazo wa Injini 501.cc – 1500.cc kutoka
kiwango cha sasa cha shilingi 100,000
hadi shilingi 150,000;
(ii) Gari lenye ujazo wa Injini 1501.cc – 2500.cc kutoka
kiwango cha sasa cha shilingi 150,000
hadi shilingi 200,000;
(iii) Gari lenye ujazo wa Injini zaidi ya 2501.cc kutoka
kiwango cha sasa cha shilingi 200,000
hadi shilingi 250,000.
(iv) Magari yenye ujazo wa Injini chini ya 501cc hayatatozwa Ada ya leseni za magari.
Hatua
hii itatekelezwa kupitia tangazo litakalochapishwa kwenye Gazeti la Serikali.
Hatua
hizi kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 19,710.90
(g)
Sheria ya Petroli (Petroleum Act), SURA, 392;
(ii)
Ili kutekeleza dhamira ya Serikali ya
kusambaza umeme vijijini, napendekeza kuanzisha Tozo ya mafuta ya petroli
(petroleum levy) ya shilingi 50 kwa lita ambayo itakusanywa na Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA). Mapato yatakayokusanywa kutoka kwenye tozo hiyo
yatatumika kugharamia mahitaji ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA) katika
kusambaza umeme vijijini. Hatua hii itatekelezwa kupitia tangazo
litakalochapishwa kwenye Gazeti la Serikali.
Hatua
hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 123,725.
(h)
Sheria
ya Uwekezaji Tanzania, SURA, 38
Kutoza asilimia 25
ya ushuru wa forodha unaopaswa kutozwa kwenye bidhaa zinazotambulika kama “Deemed Capital Goods” (yaani kutoa
msamaha wa kodi wa asilimia 75 kwenye bidhaa hizo badala ya asilimia 90 za
sasa), na kuziondoa baadhi ya bidhaa kwenye orodha ya kupata msamaha. Bidhaa
hizo ni zile ambazo hazina uasilia wa kuwa bidhaa za mtaji (capital goods) kama
vile vifaa vya ofisi, samani, sukari, vinywaji (viburudisho), bidhaa za mafuta
ya petroli, magari madogo (Non Utility Motor Vehicles), viyoyozi, majokofu, na
vifaa vya kielektroniki, mashuka, vijiko, vikombe nk.
(i)
Sheria
ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ya mwaka 2004
121.
Mheshimiwa Spika, Mawaziri wa Fedha kutoka
katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walifanya
Kikao cha mashauriano kuhusu
masuala ya Bajeti (Pre-Budget Consultations of EAC Ministers
for Finance) tarehe 07 Juni 2013 mjini Arusha. Kikao hicho kilipendekeza
marekebisho ya viwango vya Ushuru wa Pamoja wa Forodha (EAC-Common External
Tariff “CET”) na Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC-Customs Management Act, 2004) kwa
mwaka wa fedha wa 2013/14.
122.
Mheshimiwa Spika, maeneo yaliyopendekezwa kufanyiwa marekebisho kwenye viwango vya Ushuru
wa Pamoja wa Forodha ni:-
(i) Kutoza
Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 10 badala ya asilimia 35 kwenye
ngano inayotambuliwa katika HS Code 1001.99.20 na HS Code 1001.99.90. Lengo la
hatua hii ni kutoa unafuu kwa viwanda na wazalishaji wa bidhaa na vyakula
vinavyotumia ngano hiyo;
(ii) Kutoza ushuru wa asilimia 25 kwenye bidhaa za mchele
na sukari wakati bidhaa hizo zinapoingizwa nchini kwa msamaha maalumu wa
Serikali baada ya kupata ridhaa ya Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika
Mashariki. Bidhaa hizo kwa sasa zinatozwa Ushuru wa pamoja wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki wa asilimia 100 kwa sukari na asilimia 75 kwa mchele.
123.
Mheshimiwa Spika, Mawaziri wa Fedha wa
Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walifanya marekebisho kwenye
Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC-Customs Management Act, 2004) kama ifuatavyo:-
(i)
Kurekebisha Jedwali la Tano la Sheria ya
Forodha ya Jumuiya ili kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha kwa mashine na vipuli
vya reli vinavyoagizwa na Shirika la Reli Tanzania. Hatua hii inalenga katika kutoa unafuu kwenye gharama za kuboresha reli
na kuimarisha usafirishaji wa reli;
(ii)
Kufuta utaratibu
wa kutokukagua mizigo inayoingizwa na wafanyabishara ujulikanao kama “Compliant Trader Scheme” ambao uzoefu
umeonesha kwamba unatumiwa vibaya na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu
kukwepa kulipa kodi sahihi na hivyo kuipotezea Serikali mapato yake halali;
(iii)
Kuimarisha mfumo
wa uthamini (valuation) wa bidhaa kutoka nje ya nchi ili kuondoa tatizo la
upotevu wa mapato kutokana na uthamini usio sahihi. Hatua zitakazochukuliwa ni
pamoja na kuboresha mfumo wa Import
Export Commodity Database (IECDB);
(iv)
Kuendelea kutoa
msamaha wa Ushuru wa Forodha (duty remission) kwa malighafi ya kutengeneza
sabuni inayojulikana kama LABSA inayotambuliwa katika HS Code 3402.11.00; HS
Code 3402.12.00 na HS Code 3402.19.00 kwa kipindi kingine cha mwaka mmoja.
Hatua hii inalenga katika kuimarisha uzalishaji na kukuza viwanda vidogo na vya
kati vya sabuni hapa nchini;
(v)
Kutoa msamaha wa ushuru wa forodha kwenye
mifuko ya plastiki inayotumika katika uzalishaji wa nishati ya gesi (plastic bag biogas digesters). Lengo la
hatua hii ni kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala na kutunza mazingira;
(vi) Kuongeza ushuru wa forodha kwenye mawe
yanayotumika katika mashine za kusaga bidhaa mbalimbali kutoka asilimia sifuri
hadi asilimia 25. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vya ndani vya Jumuiya
ya Afrika Mashariki;
(vii) Kutoa
msamaha wa ushuru wa forodha kwenye mitambo ya kusafisha uchafu katika maji
(Water treatment effluent plant) unaotoka viwandani kutoka asilimia 10 hadi
asilimia sifuri. Lengo la hatua hii ni kuhamasisha viwanda vya ndani kutumia
mitambo hii ili kupunguza uchafuzi wa mazingira na kupunguza gharama za
uzalishaji viwandani;
(viii) Kuendelea
kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye migahawa ya Majeshi ya Ulinzi kwa
kipindi cha mwaka mmoja;
(ix) Kufanya
marekebisho kwenye Jedwali la Tano la Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki ili kutoa msamaha kwa Idara ya Usalama wa Taifa.
Hatua
hizi kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 135,526.90
(j)
Marekebisho
mengine madogo madogo katika baadhi ya Sheria za Kodi na sheria nyingine
mbalimbali.
124.
Mheshimiwa Spika, napendekeza
kufanya marekebisho mengine madogo madogo yasiyo ya kisera katika Sheria
mbalimbali za kodi ili ziwe sanjari na azma ya kurahisisha utekelezaji wake.
(i)
Kwa kutambua kwamba Sekta binafsi ndiyo yenye
msukumo mkubwa katika maendeleo ya uchumi duniani kote, napendekeza kufanya
marekebisho katika sheria ya Public Procurement Act, 2011 na Public Private
Partnership Act 2010 ili kuwezesha “unsolicited
PPP Proposals” kutohusika na utaratibu wa ushindani ikiwa ni njia mojawapo
ya kuvutia wawekezaji katika miradi ya maendeleo kwa manufaa ya kiuchumi ya
nchi yetu;
(ii)
Kurekebisha Sheria ya Fedha Za Umma SURA 348, Sheria
ya Msajili wa Hazina SURA 418, na Sheria ya Wakala za Serikali, SURA 245, ili
kuweka sharti kwa wakala na taasisi za serikali kuwasilisha kiasi cha asilimia
10 ya mapato ghafi (badala ya mapato ya ziada) ya taasisi na wakala hizo kwenda
kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.
(k)
Marekebisho ya Ada na Tozo Mbalimbali za Wizara, Mikoa na
Idara zinazojitegemea
125.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho ya viwango vya ada na
tozo mbali mbali zinazotozwa na Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea ili
kuvihuisha kulingana na hali halisi ya ukuaji wa uchumi.
(l)
Tarehe ya Kuanza Kutekeleza Hatua Mpya za Kodi
126.
Mheshimiwa Spika, hatua hizi za kodi zinazopendekezwa zitaanza kutekelezwa
tarehe 1 Julai, 2013, isipokuwa pale ilipoelezwa vinginevyo.
VI.
SURA YA BAJETI KWA MWAKA 2013/14
127.
Mheshimiwa
Spika, kwa kuzingatia
sera za uchumi jumla pamoja na misingi na shabaha ya bajeti, sura ya bajeti
itakuwa kama ifuatavyo; Serikali imepanga kukusanya jumla ya shilingi bilioni 18,249
kutoka kwenye vyanzo vya ndani na nje. Mapato
ya kodi na mapato yasiyo ya kodi yanatarajiwa kufikia shilingi bilioni 11,154.1
sawa na asilimia 20.2 ya Pato la Taifa. Aidha, mapato kutokana na vyanzo vya
Halmashauri yanatarajiwa kufikia shilingi bilioni 383.5 sawa na asilimia 0.7 ya
Pato la Taifa.
128.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka
2013/14 Washirika wa Maendeleo wanatarajiwa kuendelea kutupatia misaada na
mikopo ya jumla ya shilingi bilioni 3,855.2. Kati ya fedha hizo, shilingi
bilioni 1,163.1 ni misaada na mikopo ya kibajeti na shilingi bilioni 2,692.1 ni
mikopo na misaada kwa ajili ya miradi ya maendeleo, na Mifuko ya Pamoja ya
Kisekta shilingi bilioni 500.4.
129.
Mheshimiwa
Spika, ili kuziba
nakisi ya bajeti, Serikali inatarajia kukopa kutoka katika vyanzo vya ndani na
nje shilingi bilioni 2,856.3. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 1,147.6 ni
kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva na mkopo wa
ndani shilingi bilioni 552.3 ambao ni asilimia moja ya Pato la Taifa na
shilingi bilioni 1,156.4 ambazo ni mikopo yenye masharti ya kibiashara
zitatumika kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
130.
Mheshimiwa
Spika, kuhusu
matumizi, jumla ya shilingi bilioni 18,249 zimekadiriwa kutumika katika mwaka
2013/14, kwa ajili ya matumizi ya kawaida na ya maendeleo. Kati ya hizo matumizi
ya kawaida ni shilingi bilioni 12,574.9 ambayo
yanajumuisha shilingi bilioni 4,763 kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa
Serikali, Taasisi na Wakala za Serikali; Mfuko Mkuu wa Serikali shilingi
bilioni 3,319.2, na Matumizi Mengineyo shilingi bilioni 4,492.6.
131.
Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka
2013/14 jumla ya shilingi bilioni 5,674 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya
maendeleo, ambapo kiasi cha shilingi bilioni 2,982 kitagharamiwa kwa fedha za
ndani. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 552.3 zinatokana na mkopo kutoka
vyanzo vya ndani, shilingi bilioni 1,156.4 ni mikopo ya masharti ya kibiashara,
shilingi bilioni 386.2 ni mikopo ya kibajeti, na shilingi bilioni 887.1
zitatokana na asilimia 8 ya mapato ya kawaida. Kiasi cha shilingi bilioni 2,692.6
kitagharamiwa kwa fedha za nje, misaada na mikopo ya miradi ya maendeleo ikijumuisha
Mifuko ya Pamoja ya Kisekta.
132.
Mheshimiwa
Spika, kwa kuzingatia
mfumo wa bajeti kama ulivyoelezwa hapo juu, mfumo wa bajeti kwa mwaka 2013/14
unakuwa kama ifuatavyo:
Mapato
|
Shilingi Milioni
|
||
A.
|
Mapato ya
Ndani
|
11,154,071
|
|
(i) Mapato ya Kodi (TRA)
|
10,412,937
|
||
(ii) Mapato yasiyo ya Kodi
|
741,134
|
||
B.
|
Mapato ya Halmashauri
|
383,452
|
|
C.
|
Mikopo na
Misaada ya Kibajeti
|
1,163,131
|
|
D.
|
Mikopo na
Misaada ya Miradi ya Maendeleo ikijumuisha MCA (T)
|
2,692,069
|
|
E.
|
Mikopo ya
Ndani
|
1,699,860
|
|
F.
|
Mikopo
yenye Masharti ya Kibiashara
|
1,156,400
|
|
JUMLA YA
MAPATO YOTE
|
18,248,983
|
||
Matumizi
|
|||
G.
|
Matumizi
ya Kawaida
|
2,574,949
|
|
(i) Deni la Taifa
|
3,319,156
|
||
(ii) Mishahara
|
4,763,196
|
||
(iii) Matumizi Mengineyo
|
4,492,566
|
||
Wizara
3,738,316
|
|||
Mikoa 49,701
|
|||
Halmashauri 04,549
|
|||
H.
|
Matumizi
ya Maendeleo
|
5,674,034
|
|
(i) Fedha za Ndani
|
2,981,965
|
||
(ii) Fedha za Nje
|
2,692,069
|
||
JUMLA YA MATUMIZI
YOTE
|
18,248,983
|
VII.
HITIMISHO
133.
Mheshimiwa
Spika, kama
nilivyoeleza hapo awali, bajeti ya mwaka 2013/14 imelenga kutekeleza Mpango wa
Kwanza wa Maendeleo wa miaka mitano; Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010;
Awamu ya Pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA II); Malengo
ya Maendeleo ya Milenia 2015; na kuanza kutekeleza maeneo ya vipaumbele
yaliyoainishwa katika Labs. Madhumuni
ya mipango na mikakati hii ni kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo
2025.
134.
Mheshimiwa Spika, suala ambalo ningependa kulisisitiza ni sote kwa pamoja
kuongeza ushirikiano katika kusimamia majukumu na matumizi ya fedha na
rasilimali zetu vizuri ili kuongeza ufanisi. Masuala yote tuliyoyajadili katika
bunge hili ni ya msingi sana, hivyo kama yakifanyiwa kazi kwa ufanisi tutafikia
matarajio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ambayo yanalenga kuitoa Tanzania
katika kundi la nchi maskini na kuingia katika kundi la nchi zenye viwango vya
kati vya mapato na hali bora ya maisha.
135.
Mhesimiwa
Spika, bajeti
hii imelenga pia kuongeza makusanyo ya mapato, hasa ya ndani kwa kuanzisha
vyanzo vipya na kuboresha vilivyopo. Lengo likiwa ni kujitosheleza kwa mapato
yatakayowezesha kutekelezwa kwa miradi mbalimbali ya maendeleo na kuboresha
huduma kwa wananchi. Katika kikao hiki cha Bunge la bajeti, waheshimiwa wabunge
walipendekeza kuongeza fedha kwa baadhi ya mafungu ili kuyawezesha kutekeleza
majukumu yao kikamilifu. Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa Serikali
sikivu ya Chama cha Mapinduzi imezingatia kwa kiasi kikubwa mapendekezo hayo. Ili
kutekeleza mapendekezo hayo, imelazimu kufanya maboresho zaidi katika kodi na
tozo mbalimbali kwani isingewezekana kugharamia mapendekezo hayo bila kuathiri
upande wa kodi. Hivyo, waheshimiwa wabunge naomba mnielewe katika hili na
kuniunga mkono ili mafungu yaweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu na kufikia
malengo tuliojiwekea.
136.
Mhesimiwa
Spika, Serikali
kwa upande wake inaendelea kuboresha miundombinu ya kiuchumi, kifedha na
kijamii ili kuongeza fursa za ushiriki wa wananchi katika uzalishaji na kuboresha
hali zao za maisha. Bajeti, inalenga pia kuongeza upatikanaji wa nishati ya
umeme wa uhakika, kuendeleza ardhi na kuunganisha nchi yetu kwa njia ya miuondombinu
ya barabara, reli na viwanja vya ndege na mawasiliano. Hii itasaidia pia
kutumia vyema fursa za kijiografia zinazotokana na kupakana na nchi zisizokuwa
na bahari. Aidha, bajeti hii inalenga kufungua fursa za kuchumi na kijamii kwa
ajili ya maendeleo endelevu kupitia mfumo mpya wa utekelezaji wa miradi ya
kipaumbele ambapo italeta matokeo makubwa kwa haraka.
137.
Mheshimiwa Spika, bajeti ya Serikali kwa mwaka 2013/14 imezingatia mapendekezo
ya Kamati ya Bajeti na Kamati za Kisekta za Bunge kadiri hali ya fedha
ilivyoruhusu. Ushauri uliotolewa na Kamati hizo na hoja mbalimbali zilizotolewa
na waheshimiwa wabunge zilifanyiwa kazi kadiri ilivyowezekana. Aidha, kwa
utaratibu huu mpya wa mzunguko wa bajeti ambao ulipitisha bajeti za mafungu
mbalimbali, maelelezo yangu haya ni kuhitimisha mjadala wa bajeti ya Serikali
kwa mwaka 2013/14.
138.
Mheshimiwa
Spika, yote niliyoyasema
yanawezekana iwapo kila mmoja wetu na wananchi kwa ujumla tutatimiza wajibu wetu,
kila mmoja kwa nafasi yake, kwa kushiriki na kuwajibika kikamilifu katika
kutekeleza sera na mipango tuliyojiwekea.
139.
Mheshimiwa
Spika, naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment