TANGAZO


Monday, June 24, 2013

Mahakama ya Wilaya Igunga yawaachia washitakiwa wa tindikali, Polisi wawakamata tena

Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana, kuhusu kuwapeleka mawakili watatu, watakaoongozwa na Profesa Abdalla Safari (katikati), kuisimamia kesi iliyofunguliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), wilayani Igunga, ikiwatuhumu baadhi ya wanachama wao kumwagia tindi kali mwanachama wa CCM, Mussa Tesha, wakati wa kampeni za uchaguzi jimboni humo. (Picha na Kassim Mbarouk)

Na Abdallah Amiri, Igunga.
MAHAKAMA ya Wilaya ya Igunga Mkoani Tabora, leo imewaachia watuhumiwa wanne wa Tindikali baada ya upande wa mashitaka kuondoa shitaka lililokuwa likiwakabili mahakamani hapa.

Mwendesha mashitaka wa Polisi, Cosmas Mboya aliondoa shitaka hilo kwa kutumia kifungu cha 98 (A) cha sheria ya makosa ya jinai cha mwaka 1985 kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2002 kinacho mruhusu mwendesha mashitaka kufanya hivyo.

Baada ya mwendesha mashitaka kuondoa shitaka hilo, Hakimu wa mahakama hiyo, Ajali Milanzi alikubaliana na upande wa mashitaka na kusema kuwa, washitakiwa mko huru.

Hata hivyo baada ya kufutiwa shitaka hilo watuhumiwa walianza kutoka nje ya mahakama na ndipo askari zaidi ya 48 waliwazingira huku wakiwa na mabomu, bunduki na pingu na kuwakamata tena.

Baada ya kuwafunga pingu, polisi hao waliwapakia watuhumiwa hao ndani ya magari mawili ya polisi na kuondoka nao huku wananchi waliokuwa wamefurika mahakamani hapo wakibakia wameshikwa butwaa huku wakilia bila kujua watuhumiwa walikopelekwa.

Waandishi wa habari tulifanya juhudi za kufuatilia kituo cha polisi ili kujua walikopelekwa watuhumiwa. Hata hivyo tuliambiwa na Mkuu wa polisi Bw. Abeid Maige  kuwa washitakiwa wamepelekwa Tabora kwa ajili ya kwenda kufunguliwa mashitaka mengine.

Washitakiwa hao ambao ni Evodius  Justian (30) mkazi wa Bukoba, Osca Kaijage (36) mkazi wa Ndala mkoani Shinyanga , Rajabu Daniel (24) mkazi wa Singida na Seif  Magesa (37) mkazi wa Nyasaka mkoani Mwanza walifikishwa katika mahakama ya wilaya ya Igunga April 12 mwaka huu kwa kosa la kummwagia Tindikali Bw. Mussa Tesha (26) mkazi wa Igunga Mjini wakati wa Kampeni za Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga uliofanyika Octoba mwaka 2011.

No comments:

Post a Comment