Mkurugenzi Bi. Lutgard Kagaruki |
Na Genofeva Matemu – MAELEZO
CHAMA cha Kudhibiti Matumizi ya Tumbaku Tanzania kimeiomba serikali kutunga sheria ya kudhibiti matumizi ya tumbaku inayoendana na matakwa ya Mkataba wa Kimataifa wa Kudhibiti Matumizi ya Tumbaku ili kuzuia madhara yanayoendelea kutokea kwa wananchi wasiotumia na wanaotumia tumbaku.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Kudhibiti Tumbaku Tanzania Bi. Lutgard Kokulinda Kagaruki wakati akitangaza maadhimisho ya siku ya kutokumia Tumbaku Tanzania yatakayofanyika Mei 31 mwaka huuna kuongozwa na kauli mbiu isemayo Piga Marufuku Matangazo, Promosheni na Ufadhili wa Tumbaku.
“Baada ya kutambua kuwa madhara ya tumbaku ni janga la dunia, Shirika la Afya Dunia lilipendekeza Mei 31 ya kila mwaka iwe Siku ya Kutotumia Tumbaku Duniani na kuielimisha jamii juu ya madhara ya afya yanayosababishwa na matumizi ya tumbaku” amesema Bi. Kagaruki.
Akizungumzia tafiti zilizofanywa na taasisi mbalimbali kuhusiana athari za matumizi ya tumbaku Bi. Kagaruki amesema kuwa utafiti uliofanywa na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road mwaka 2010 ulionyesha kuwa zaidi ya asilimia 32 ya saratani zote zilihusishwa moja kwa moja na matumizi ya tumbaku na kuigharimu serikali zaidi ya dola za kimarekani milioni arobaini kuhudumia wagonjwa wa saratani.
Magonjwa mengine yanayohusishwa na matumizi ya tumbaku ni pamoja na magonjwa ya moyo, kisukari, upungufu wa nguvu za kiume, vidonda vya tumbo pamoja na magonjwa sugu ya kifua.
Aidha Bi. Kagaruki amesema kuwa muendelezo wa matangazo, promosheni na ufadhili wa bidhaa za tumbaku Tanzania umesababisha ongezeko kubwa la matumizi ya tumbaku miongoni mwa vijana ambapo utafiti uliyofanywa mwaka 2008 na Global Youth Tobacco Survey unaonyesha kuwa asilimia 10.6 ya wanafunzi wanatumia bidhaa zinzotokana na tumbaku.
Naye mkulima wa Tumbaku kutoka Tabora Bw. Salum Rajabu Matongo amesema kuwa tumbaku ni zao linalomwezesha kupata fedha kwa ajili ya kuhudumia familia yake lakini ni zao lenye athari nyingi zikiwemo kudhoofisha mwili wa mtumiaji, kusababisha madhara mengi kama uharibifu wa mazingira kutokana na kukata miti wa ajili ya kukausha tumbaku na kuathiri macho kutokana na moshi.
No comments:
Post a Comment