TANGAZO


Wednesday, May 29, 2013

Balozi wa Ujerumani nchini, aimwagia sifa Tanzania katika utoaji huduma za maji safi

Balozi Klaus – Peter Brandes


Na FrankShija, Eliphace Marwa-MAELEZO

TANZANIA ni miongoni mwa nchi za Bara la Afrika zinazojitahidi katika utoaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wake.

Hayo, yamebainishwa na Balozi wa Ujerumani   nchini Tanzania, Balozi Klaus – Peter Brandes  leo, wakati akifungua kongamano la Kikanda kuhusu ushirikishwaji wa sekta mbalimbali katika  rasilimali za maji linaloendelea jijini Dar es Salaam.

Balozi Brandes amesema kuwa Tanzania imepata sifa kwa kuweka kipaumbele katika sekta ya maji  kuwa miongoni wa sekta sita muhimu zilizo katika mpango wa ufuatiliaji utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia mpango wake unaojulikana kama Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now).

“Tanzania ni miongoni mwa nchi za bara la Afrika zinazoshughulikia maendeleo ya sekta ya maji,naipongeza Serikali ya Tanzania hasa kwa kuona umuhimu na kuweka kipaumbele sekta hii   katika mpango wake wa Matokeo Makubwa Sasa”,alisema Balozi Brandes.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Christopher Simon Sayi amesema kuwa Serikali itatekeleza miradi ya usambazaji maji vijijini ambapo vijiji kumi vitanufaika katika kila wilaya  na kusema kuwa zaidi ya watu milioni 15 watakuwa wamepata maji ifikapo 2015/2016.

Aidha  Mhandisi Sayi aliongeza kuwa ili kuleta ufanisi katika sekta ya maji  wadau wa maji lazima  washirikishwe  kwa kuwa Serikali peke yake haiwezi kuwa na suluhisho  kuhusu upatikanaji wa maji.

 Mhandisi Sayi amesema kuwa Serikali kwa kutambua umuhimu wa maji, mwaka 2002 ilipitisha sera ya maji ambayo  inatoa fursa kwa wananchi kuunda jumuiya za  matumizi ya  maji ambapo watabuni na kusimamia miradi ya maji inayotekelezwa katika maeneo yao.

No comments:

Post a Comment