TANGAZO


Thursday, May 9, 2013

Dk. Charles Kimei achaguliwa kuwania tuzo ya Kiongozi bora wa Mabenki Afrika mwaka 2013



Mkurugenzi Mtendaji wa 

Benki ya CRDB, Dk. 

Charles Kimei (pichani), 
amechaguliwa kwenye 
mchakato wa kumtafuta “kinara wa Benki wa Afrika”  kwa mwaka 2013, unaoendeshwa na African Banker Awards, chini ya African  Development Bank Group.

 Kinara wa Benki wa mwaka ni tuzo inayotolewa kwa Viongozi (CEO`s) wa sekta ya benki na fedha barani Afrika ambao wamepata mafanikio makubwa kwenye mashirika yao hivyo kuleta maendeleo katika sekta fedha na uchumi katika nchi zao na Afrika nzima kwa ujumla.
African Banker Awards imechagua  vinara watano wa sekta ya fedha Afrika  kuingia katika mchakato huo ambapo mmoja wao ndiyo atakayejitwalia tuzo hiyo. Zaidi ya Dk. Charles Kimei, wengine waliongia kwenye mchakato huo na nchi wanazotoka kwenye mabano ni  Segun Agbaje-GTB Bank(Nigeria), Aigboje Aig-Imoukhede-Access Bank(Nigeria), Andrew Allly-Africa Finance Corporation(Nigeria) na Jao Figuerdo- Unico Bank.

Dk. Kimei ni mtanzania wa kwanza kuingizwa kwenye mchakato huu tangu kuanzishwa kwa tuzo hiyo zaidi ya miaka kumi iliyopita, na ni mtanzania pekee kwenye kinyang`anyiro hicho ambacho kimekuwa kikitawaliwa na mabenki kutoka nchini Nigeria na Afrika ya Kusini. Hii ni fahari kubwa kwa taifa letu kwani Dk. Charles Kimei ni mtanzania anayeongoza benki kubwa ya Tanzania inayoendeshwa na watanzania wenyewe.

Dk. Kimei, ambaye ni mchumi mwenye stashahada ya uzamivu, amefanya kazi katika sekta ya fedha kwa zaidi ya miaka 30 akitokea Benki Kuu ya Tanzania alikokuwa Mkurugenzi wa Sera na Utafiti  kabla ya kujiunga na Benki ya CRDB mwaka 1998 kama Mkurugenzi Mtendaji. Akiwa Benki ya CRDB ameingoza kutoka Benki iliyokuwa ikijiendesha kwa  hasara hadi kuwa Benki inayoongoza nchini.

Chini ya uongozi wa Dk. Kimei, Benki ya CRDB imeweza kupata mafanikio makubwa  ikiwemo kutoka kutengeneza faida ya Shilingi billion 2 mwaka 1998 mpaka kufikia Shilingi billion 108 mwaka huu, kuongeza mtandao wake wa matawi kutoka matawi 16 hadi matawi 97 mwaka huu. Katika kipindi hiki  pia Benki ya CRDB imekuwa kinara wa kuleta bidhaa bunifu kwenye soko ikiwemo kadi zenye nembo za kimataifa za MasterCard na Visa, ATMs za kutolea na kuweka fedha, mashine maalum za kulipa kwa kutumia kadi (POS), Mikopo maalum ya Microfinance na Wajasiriamali pamoja na kushinda tuzo za kimataifa za Chapa Bora yaani SuperBrands kwa miaka minne mfululizo (2010-2013) na  tuzo ya benki bora itolewayo na  Euro-Money mwaka 2004.

Chini ya uongozi wa Dk. Kimei, Benki ya CRDB imekuwa benki ya kwanza ya kizalendo  kuvuka mipaka na kufungua kampuni tanzu katika nchi jirani ya Burundi hivyo kufungua milango ya ukuaji wa mahusiano ya biashara kati ya nchi hizo mbili na ukanda mzima wa Afrika Mashariki kwa ujumla.

Kuingia kwa Dk.Kimei kwenye mchakato huu wa kupata kiongozi bora  wa Benki wa Afrika kunakuja muda mfupi tu baada ya kuteuliwa kwake bila kupingwa kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mabenki nchini Tanzania (TBA). Mwenyekiti wa Chama Cha Mabenki huchaguliwa na benki zote wanachama wa TBA.

Tunamtakia kila kheri Dk.Charles Kimei na Benki ya CRDB katika kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania katika tuzo hiyo.

No comments:

Post a Comment