TANGAZO


Saturday, April 27, 2013

Mwingine azikwa akiwa hai Mbeya

Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Kamishna Msaidizi, Diwani Athuman 

-Alipigwa sururu kichwani akipokea maiti ya kijana wakati ikishushwa kaburini
-Atuhumiwa kumuua kishirikina kijana mgonjwa aliyefia kwa mganga wa jadi.

Na Moses Ng’wat,Mbeya.

KWA mara nyingine Mkoa wa Mbeya umegubikwa na tukio lisilo la kawaida, baada ya mtu mmoja, Flovian Mwamosi Mwachuki (70), mkazi wa mtaa wa Maweni, katika Mji mdogo wa  Mkwajuni, wilayani Chunya, amefariki dunia baada ya kufukiwa katika kaburi moja na marehemu anayedaiwa kumuua kishirikina.

Tukio hilo ambalo ni miongoni mwa matukio kadhaa ya aina hiyo, yaliyoibuka hivi karibuni mkoani hapa, lilitokea jana, Aprili 26, mwaka huu, majira ya saa tisa mchana, muda mfupi kabla ya kuzikwa kwa marehemu anayedaiwa kulogwa na Mwachuki, Peter Robert (28).

Taarifa za uhakika na kina kutoka eneo la tukio zinadai kuwa tukio hilo la  marehemu Mwachuki kuzikwa hai lilisababishwa na hisia kuwa alihusika kwa njia ushirikina kumuua marehemu Robert aliyefariki siku moja kabla.

Inadaiwa kuwa marehemu  Robert  alifia kwa mganga wa kienyeji alikokuwa akipatiwa matibabu kutokana na kuugua maradhi ambayo hata hivyo hayakutajwaanaye, ilielezwa kuwa baada ya kifo hicho kuliibuka hisia kuwa aliuawa kishirikina.

Habari zaidi zinadai kuwa hali iliyochochea baadhi ya vijana kuamini kuwa kifo hicho cha mwenzao  kilitekelezwa na marehemu Mwachui ambapo walianza kumwinda hadi walipofanikiwa kulipiza kisasi baada ya kumuomba ashuke kaburini kupokea maiti ya kijana mwenzao huyo.

Inadaiwa kuwa wakiwa eneo la makaburini huku wakijua nia yao ovu ya kutaka kulipiza kisasi, vijana hao waliomba watu wenye umri mkubwa washuke kaburini ili kupokea mwili wa marehemu ndipo marehemu Mwachui na wenzake walishuka na kujikuta akianza kupokea kipigo huku watu wengine wakiondolewa kwa kuvutwa.

“Ni tukio ambalo huwezi kuamini kwani wakati mzee huyo akijaribu kujinasua kutoka ndani ya kaburi hilo, huku akiendelea kupata kipigo kikali cha mawe na udongo waliorushia kwa chepeo, kijana mmoja alimpiga sururu ya kichwa iliyomnyong’onyesha na kisha kuanguka chini na baadae vijana hao waliingiza mwili wa mwenzao na kufukia kaburi hilo” alisema mmoja wa mashuhuda ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.

Baada ya kutekeleza unyama huo vijana hao waliamua kutawanyika mmoja moja kusikojulikana, huku wakiwatrisha badfhi ya wananchi wengine waliokuwa makaburini hapo kuthubutu kutoa taarifa kwa vyombo vya dola.

Hata hivyo inadaiwa kuwa polisi walikuja kupata taarifa za tukio hilo baada ya saa mbili, ambapo majira ya saa 11 jioni ndipo walifukua kaburi hilo na kukuta miili ya marehemu wotw wawili wakiwa wamezikwa ndani yake.

Inadaiwa waliitoa miili ya marehemu hao na kwenda kuhifadhi katika Hospitali ya misheni ya Mwambaji katika mji huo, ambapo hadi jana majira ya saa nane bado miili hiyo ilikuwa imehifadhiwa katika hospitali hiyo.

Jeshi la polisi mkoani Mbeya limethibitisha kutokea kwa tukio hilo la kikatili dhidi ya binadamu na kudai kuwa bado linaendelea kuwasaka wote waliohusika na ukatili huo ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria kwa kuwa kulikuwa hakuna aliyekamatwa.

Katika taarifa yake iliyoitumwa kwa njia ya mtandao kwenye vyombo habari mkoani hapa na kusainiwa na kamanda wa polisi, Diwani Athuman, zinaeleza kuwa tukio hilo lilitokea majira ya saa tisa Aprili 26 mwaka huu huku Mkwajunu, wilayani Chunya.

Hata hivyo katika taarifa hiyo, kamanda wa polisi anatoa wito kwa wakazi wa eneo la tukio na mkoa wa Mbeya, kujitokeza katika jeshi hilo kutoa ushirikano wa kuwataja wahusika ili wakamatwe.

“Msako mkali unaendelea kuwasaka waliohusikana katika tukio hilo na natoa wito na kuwaasa  wananchi/jamii kuacha tabia ya kuamini mambo ya ushirikina/uchawi kwani hauna faida kwao bali huchochea migogoro katika jamii zao, aidha nawaomba wenye taarifa za walipo waliohusika na mauaji hayo kuzifikisha polisi haraka ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.” Ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Matukio mengine yaliyotokea mkoani hapa kwa watu kuzikwa hai ni lile la Aprili 29 mwaka 2011 la  mkazi wa kijiji cha Itezi, Jijini Mbeya, Kombwee Nyerere, pamoja na wakazi wengineEnest Morela na Minazara Mililo wote wakazi wa kijiji cha Ivuna, wilaya ya Momba nao walizikwa wakiwa hai wakikutuhumiwa kumuua mwanakijiji mwenzao kwa ushirikina.

No comments:

Post a Comment