TANGAZO


Tuesday, April 2, 2013

Maafisa wa EU kutoa mafunzo Mali


Maafisa wa kijeshi wa Muungano wa Ulaya watakaotoa mafunzo kwa wanajeshi wa Mali kama sehemu ya juhudi za kusaidia nchi hiyo ya Afrika Magharibi kukabiliana na wapiganaji wa kiisilamu, wanatarajiwa kuanza kazi yao hivi karibuni.
Moja ya vikosi vinne vya wanajeshi wa Mali, watafunzwa na maafisa wa Ulaya katika kambi ya jeshi ya Koulikoro umbali wa kilomita sitini kutoka mji wa Bamako.
Harakati hizo zinazoendeshwa na jeshi la Ufaransa zilianza mwezi Januari,katika miji mikubwa ya Mali, dhidi ya wapiganaji wa kiisilamu.
Hata hivyo, mapigano yangali yanaendelea Kaskazini mwa nchi.
Kuna takriban maafisa 150 wa mafunzo ya jeshi kati ya wanajeshi 550 kutoka nchi 22 barani Ulaya walioko Mali kukabiliana na wapiganaji wa kiisilamu.
Ufaransa ndio nchi kubwa zaidi kutoa wanajeshi wengi, 207 ikifuatiwa na Ujerumani yenye wanajeshi 71 , Uhispania ikiwa na 54, Uingereza 40,Jaumuhuri ya Czech 34, Ubelgiji 25 na Poland 20.
Mafunzo yanatolewa chini ya usimamizi wa Generali Brigedia Francois Lecointre na yanatarajiwa kuendelea kwa zaidi ya miezi 15.
Kikosi cha kwanza kitakachopokea mafunzo kamilifu kuendesha harakati hizo kinatarajiwa kuanza kazi mwezi Julai.
Makundi ya wapiganaji wa kiisilamu yalianza kuendesha harakati zao pindi mapinduzi ya kijeshi yalipofanyika mwezi Machi mwaka jana Kaskazini mwa Mali ikiwemo Gao, Kidal na Timbuktu.
Yalianza kutumia sheria za kiisilamu kutawala miji hiyo.
Ufaransa iliingilia mgogoro huo baada ya kusema kuwa wapiganaji hao wenye uhusiano na al-Qaeda walitishia kuvamia mji mkuu Bamako.
Ufaransa sasa inajiandaa kuondoa wanajeshi wake 4,000 wanaoshika doria nchini Mali.Wanajeshi wengine kutoka nchi za Afrika Magharibi watachukua mahala pao.

No comments:

Post a Comment