Ndugu
Wananchi;
Naomba nianze kwa kumshukuru
Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na kunipa fursa ya kuzungumza nanyi kwa
kupitia utaratibu wetu huu mzuri wa kila mwisho wa mwezi. Leo ninayo mambo matatu ninayopenda kuzungumza nanyi.
Ziara ya Rais wa
China Nchini Tanzania
Ndugu wananchi;
Jambo
la kwanza ni ziara ya Mheshimiwa Xi Jinping, Rais wa Jamhuri ya Watu wa China
aliyoifanya nchini kwetu kati ya tarehe 24 na 25 Machi, 2013. Lengo la ziara yake ilikuwa kuimarisha
uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya China na Tanzania. Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru
wakazi wa Dar es Salaam kwa kumpokea vizuri mgeni wetu na ujumbe wake. Wameondoka wakiwa na kumbukumbu nzuri ya nchi
yetu na watu wake.
Kwa niaba yenu, nimepokea salamu
za shukrani kutoka kwa Rais Xi Jinping akielezea kufurahishwa na mapokezi
mazuri tuliyowapatia. Naomba tuendelee kuonesha moyo wa upendo na ukarimu kwa
wageni wetu wengine mashuhuri watakaotutembelea siku za usoni.
Ndugu wananchi;
Nami pia, nimemshukuru sana
Mheshimiwa Xi Jinping kwa kukubali mwaliko wangu na kufanya ziara ya kihistoria
na yenye mafanikio makubwa kwa nchi yetu.
Ameifanyia nchi yetu jambo la heshima kubwa na kumbukumbu isiyosahaulika. Tanzania imekuwa nchi ya kwanza Barani Afrika
kuitembelea, tena siku kumi tu baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa nchi
yake. Na, kubwa zaidi ni kutumia fursa
ya ziara yake hapa nchini kutangazia dunia Sera ya China kwa Afrika katika
kipindi cha uongozi wake.
Tumefarijika sana kusikia kuwa
uhusiano na Afrika bado unapewa kipaumbele cha juu na viongozi wapya wa
China. Pia, kuwa China itaendelea kukuza
biashara na uwekezaji na kuongeza misaada ya maendeleo kwa Afrika ikiwemo kutoa
nafasi 18,000 za mafunzo kwa vijana wa Kiafrika. Kama mtakumbuka nchi zetu mbili zilitiliana
saini mikataka 16 ya ushirikiano katika nyanja mbalimbali. Misaada ya maendekeo kwa maeneo yetu ya
kipaumbele nayo imejumuishwa.
Ndugu Wananchi;
Rais Xi Jinping alielezea na
kusisitiza dhamira yake na ya Serikali na Chama cha Kikomunisti cha China ya
kudumisha na kukuza uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na China. Kama
mjuavyo uhusiano huo ulianzishwa mwaka 1964 na waasisi wa nchi zetu, yaani Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere aliyekuwa Rais wa kwanza wa Tanzania na Mwenyekiti Mao
Zedong aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa China na Waziri Mkuu wake Chou En Lai.
Rais wa China aliahidi kuwa nchi
yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika medani ya kimataifa na
kuchangia katika jitihada zetu za kujiletea maendeleo kwa kuongeza misaada ya
maendeleo. Katika miaka 49 ya uhusiano
na ushirikiano na China nchi yetu imepata misaada mingi ya maendeleo ikiwemo
Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere ambao ulizinduliwa na Rais
Xi Jinping wakati wa ziara yake.
Ndugu wananchi;
Kuna miradi kadhaa mikubwa
inayoendelea kutekelezwa nchini, Bara na Zanzibar, kwa msaada wa Serikali ya
China. Wakati wa ziara yake, Rais Xi
Jinping iliahidi kuendelea kutusaidia miradi mingine ya maendeleo kama
tulivyoomba wakati wa mazungumzo yetu licha ya ile ambayo ilitiwa saini siku
ile.
Ajali ya
Kuporomoka Jengo la Ghorofa
Jijini Dar
es Salaam
Ndugu Wananchi;
Jambo
la pili ninalotaka kuzungumzia ni ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa 16 lililokuwa linajengwa katika jiji la
Dar es Salaam. Ajali hiyo iliyotokea
juzi tarehe 29 Machi, 2013 imeleta msiba na simanzi kubwa nchini. Mpaka sasa maiti za ndugu zetu 30 zimepatikana. Watu 17
waliweza kuokolewa, wanne kati yao bado
wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Wengine walitibiwa na kuruhusiwa. Kazi ya kufukua eneo la ajali inaendelea na
sasa inakaribia kufikia ukingoni.
Ndugu Wananchi;
Mimi na
viongozi wenzangu tulipata nafasi ya kwenda kuangalia eneo la ajali. Hali niliyoiona pale imenihuzunisha
sana. Lazima nikiri, hata hivyo, kwamba
nimeridhishwa sana na juhudi kubwa za uokoaji zilizokuwa zinafanywa na wanajeshi
wetu wakishirikiana na taasisi, mashirika binafsi na wananchi. Napenda kutumia nafasi kutoa shukrani maalum
kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ndugu Saidi Meck Sadick kwa uongozi wake
madhubuti. Pia nampongeza Mkuu wa Wilaya
ya Ilala, Ndugu Raymond Mushi, na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es
Salaam, Ndugu Suleiman Kova pamoja na Maafisa na askari wa JWTZ, na wale wote
walioshiriki na wanaoendelea kushiriki katika juhudi za uokoaji.
Nawapongeza
pia madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na hospitali
nyinginezo kwa jitihada zao za kuokoa maisha ya waliojeruhiwa. Nawapa pole wale wote waliofiwa na wapendwa,
ndugu na jamaa zao katika ajali hii.
Nawaomba wawe na moyo wa subira huku sote tukiungana nao kuwaombea
marehemu wetu wapate mapumziko mema peponi.
Kwa waliojeruhiwa, tunawaombea wapone upesi.
Ndugu Wananchi;
Maneno
mengi yanasemwa kuhusu chanzo cha ajali ile.
Alimradi kila mtu ana dhana yake.
Niliagiza vyombo na mamlaka husika wachukue hatua zipasazo kuchunguza sababu
za ghorofa hilo kuanguka na watakaothibitika kusababisha maafa hayo wachukuliwe hatua zipasazo. Wa kushtakiwa Mahakamani washitakiwe na wa
kufutiwa leseni za kufanya shughuli za ujenzi au taaluma zao wafutiwe bila
ajizi. Jambo la msingi la kusisitiza ni
kuwa mamlaka zinazohusika na usimamizi wa ujenzi lazima zitimize ipasavyo wajibu
wake. Naamini kama mamlaka hizo
zingetimiza ipasavyo wajibu wake ajali hii ingeepukika. Halmashauri za miji na wilaya zina wajibu
maalum kwenye ujenzi katika maeneo yao. Watimize
wajibu wao. Yaliyotokea Dar es Salaam
yawe fundisho kwa wote.
Ndugu Wananchi;
Ni
matumaini yangu kuwa Bodi ya Usajili wa Wakandarasi na Bodi ya Usajili wa
Wahandisi itakamilisha mapema uchunguzi wake ili ukweli ujulikane. Bodi ya Usajili wa Wasanifu Majengo na
Wakadiriaji Majenzi na Baraza la Taifa la Ujenzi nao washirikishwe kwa
ukamilifu ili ukweli upatikane na hatua stahiki zichukuliwe. Pia naomba washauri namna bora ya kukomesha
ajali za aina hiyo siku za usoni.
Uhusiano
wa Wakristo na Waislamu
Ndugu Wananchi;
Jambo la tatu ninalopenda kuzungumza nanyi leo ni uhusiano wa
Waislamu na Wakristo nchini. Jambo hili
nimeshalizungumzia mara kadhaa siku za nyuma, lakini nalazimika kulisemea tena
kutokana na hali ilivyo sasa. Tumefikia
mahali ambapo kama viongozi na waumini wa dini hizi kubwa mbili hawatakubali
kubadili muelekeo wa sasa, tunakoelekea ni kubaya. Nchi yetu nzuri tutaivuruga na sifa yake ya
miaka mingi ya Waislamu na Wakristo kuishi pamoja kidugu, kwa upendo,
ushirikiano na kuvumiliana itatoweka.
Tanzania itaacha kuwa kisiwa cha amani na kuingia katika orodha ya nchi
zenye migogoro na hata vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Ndugu Wananchi;
Nyaraka
na kauli kali kali zinazotolewa na viongozi wa dini za Kikristo na Kiislamu
zinanishawishi kuamini haya niyasemayo.
Nyaraka na kauli hizo zina mambo mawili makuu. Kwanza, kwamba kila upande unatuhumu,
kushutumu na kulaumu upande mwingine kwa kufanya vitendo viovu dhidi ya dini yake. Kauli na mihadhara ya kudhalilisha dini za
wengine, kunajisi vitabu vitakatifu, kuchoma moto nyumba za ibada, mzozo kuhusu
nani achinje na kuuawa kwa viongozi wa dini ni baadhi ya mambo yanayotolewa
mifano.
Na, pili kwamba kila upande unailamu Serikali
kwa kupendelea upande mwingine. Wakristo wanalaumu kwamba mihadhara ya
kudhalilisha Ukristo inaendeshwa na Serikali haichukui hatua. Aidha, Wakristo wanateswa na viongozi wao
kuuawa na Waislamu, lakini Serikali haichukui hatua. Kwa ajili hiyo wanadai kuwa Serikali
imeshindwa kulinda uhai wa raia wake.
Wanasema pia kwamba Serikali inapendelea upande wa Waislamu.
Ndugu Wananchi;
Waislamu
nao wanadai kuwa kitabu chao kitakatifu, yaani Quran Tukufu, kinadhalilishwa
kwa kuchanwa, kuchomwa moto na kukojolewa na Wakristo na Serikali haichukui
hatua yo yote ya maana. Waislamu wananyanyaswa katika nchi yao, wanakamatwa
ovyo, hawapewi fursa sawa na kwamba Serikali inawapendelea Wakristo. Wanasema nchi inaendeshwa kwa mfumo wa
Kikristo. Mimi binafsi wananishutumu kuwa napendelea kushiriki zaidi kwenye
shughuli za Wakristo kuliko za Waislamu kama vile harambee za kujenga Makanisa
na shule za Makanisa. Naambiwa kuwa
mwepesi kushiriki maziko ya Maaskofu kuliko Masheikh wanapofariki. Ipo Misikiti
mitatu hapa Dar es Salaam wamenisomea itikafu nife. Katika itikafu hiyo wamewajumuisha Inspekta
Jenerali wa Polisi, Said Mwema na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es
Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Ndugu Suleiman Kova.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuwahakikishia Watanzania wenzangu kuwa mimi na
Serikali ninayoiongoza, hatupendelei upande wo wote. Hatufurahishwi na kitendo cha mtu
kudhalilisha dini ya mwenzake ndiyo maana wapo wahadhiri wa dini ya Kiislamu na
wahubiri wa dini ya Kikristo wamekamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa nyakati
mbalimbali. Vyombo vya usalama
vinatambua wajibu wake huo na kama haifanyiki ni ulegevu wa mtu tu katika
kutimiza wajibu wao na siyo kwamba ni sera na maelekezo yangu au ya
Serikali. Mtakumbuka kuwa mara kadhaa
nimewakumbusha Wakuu wa Mikoa na Wilaya na wakuu wa vyombo vya usalama kuacha
ajizi katika kutimiza wajibu wao kwenye suala hili.
Ndugu Wananchi;
Mimi
binafsi sibagui, hushiriki shughuli za Waislamu na Wakristo kila ninapoalikwa
labda nikose nafasi kwa sababu nyinginezo.
Nimeshafanya shughuli nyingi za Waislamu kama vile Maulid ya Mtume
Muhamad S.A.W., safari za Hija, ujenzi wa misikiti na madrasa na mengineyo mengi. Nimeshashiriki mazishi ya Masheikh kama
nifanyavyo kwa Maaskofu na watu mbalimbali Waislamu na Wakristo. Pale ambapo sikushiriki mazishi ya Sheikh au
Askofu itakuwa ni kwa sababu ya kubanwa na shughuli nyingine ambazo lazima
nifanye mimi, au taarifa ilikuwa ya muda mfupi.
Kwa upande wa Waislamu desturi yetu ya kuzika mara mtu anapofariki huwa
kikwazo kwangu kushiriki hasa ikiwa ni nje ya Dar es Salaam kwa sababu ya
taratibu za kumsafirisha Rais kutoka mahali pamoja kwenda pengine siyo nyepesi. Wakristo hawana utaratibu huo, huwa wanaweza
kusubiri hivyo huniwia rahisi kushiriki.
Ndugu Wananchi;
Napenda
kuwahakikishia kuwa Serikali yetu haijashindwa kulinda usalama wa raia wake au
viongozi wa dini na nyumba za ibada.
Kama ingekuwa hivyo, tungeshuhudia mauaji ya raia, viongozi wa dini na
matukio ya kuchomwa nyumba za ibada yakiwa mengi hapa nchini. Lakini hivyo sivyo. Nawasihi sana ndugu zangu Wakristo na
Waislamu kuwa tusiyachakulie matukio ya kuuawa kwa Mchungaji Mathayo Kachila
kule Buseresere, Geita, na Padri Evaristus Mushi kule Zanzibar, au kumwagiwa
tindikali Sheikh Fadhili Soroga, Naibu Mufti wa Zanizbar, kupigwa risasi Padri
Ambrose Mkenda na kuchomwa moto kwa Makanisa Zanzibar na Mbagala, Dar es Salaam
kuwa ni kielelezo na ushahidi wa Serikali kushindwa kutimiza wajibu wake.
Kila
tukio lina mazingira yake, hakuna ushahidi wa vyombo vya Serikali
kuzembea. Hakuna ushahidi wa matukio
hayo kuunganika. Mpaka sasa hatujapata ushahidi
wa kuwepo kikundi cha Waislamu wanaopanga kuua viongozi wa Kikristo na kuchoma
moto Makanisa hapa nchini.
Ndugu Wananchi;
Kifo
cha Mchungaji Mathayo Kachila wa Buseresere ni matokeo ya vurugu
zilizosababishwa na mzozo kati ya Wakristo na Waislamu kuhusu kama nyama
iliyochinjwa na Wakristo Kanisani nayo iuzwe kwenye bucha iliyopo pale kijijini
ambayo kwa mazoea huuzwa nyama iliyochinjwa na Waislamu. Katika ugomvi na vurumai hizo ndipo watu kadhaa
wa pande zote walijeruhiwa na Mchungaji kupoteza maisha. Si tukio unaloweza kulihusisha na mengineyo
nchini. Ni la pale pale Buseresere na
limeanzishwa na kuhusisha Wakristo na Waislamu wa Buseresere kwa sababu
zao.
Hivi kama
kusingekuwepo na mzozo wa nyama ile kuuzwa katika bucha ile kuumizana kule na
mauaji yale yangetokea? Kabla ya mzozo ule Wakristo na Waislamu wa Buseresere
hawakuwa na ugomvi baina yao. Walikuwa
wanaishi kidugu na kushirikiana katika shughuli zao za kujitafutia riziki huku
kila mmoja akimuabudu Mungu kwa misingi ya dini yake. Hivyo kutumia tukio hilo kutoa wito kwa
Wakristo wote kuwa kuuawa kwa Mchungaji Kachila ni sawa na kuuawa kwa Wakristo
wote nchini kulikofanywa na Waislamu ni kulikuza tatizo isivyostahili. Busara ituongoze kutafuta njia ya
kuwapatanisha Wakristo na Waislamu wa Buseresere wazungumze, waelewane na
waendelee kuishi pamoja kama ilivyokuwa awali.
Hata mzozo wa kuchinja wanaweza kuumaliza. Mbona bucha za kitimoto zipo na watu
hawajapigana. Kutumia mzozo wa Buseresere kueneza chuki kati ya Wakristo na
Waislamu nchi nzima si sawa.
Hatuwatendei haki Watanzania.
Ndugu Wananchi;
Kuuawa
kwa Padri Evaristus Mushi wa Zanzibar ni tukio linalojitegemea halina uhusiano
kabisa na lile la Buseresere, Geita.
Hapakuwa na mzozo kuhusu nani achinje.
Bado uchunguzi wake unaendelea na tumehusisha vyombo vya upelelezi vya
nje vishirikiane na vyetu kufanya uchunguzi.
Tumefanya hivyo kwa sababu ya ugumu uliopatikana katika uchunguzi wa matukio
ya kabla yake. Yaani ile la kupigwa
risasi na kujeruhiwa kwa Padri Ambrose Mkenda na kumwagiwa tindikali kwa Naibu
Mufti wa Zanzibar Sheikh Fadhili Soroga.
Bado hakuna mafanikio ya kutia moyo.
Na bado tunajiuliza kama matukio hayo matatu yanahusiana. Je, Makanisa kuchomwa moto kule Zanzibar nako
kuna uhusiano wowote na matukio yale matatu?
Uchunguzi unaoendelea unaweza kufumbua fumbo hilo.
Kuna watu wanadhani yanahusiana na kwa sababu
nzuri. Lakini inabaki kuwa ni dhana ya
kibinadamu mpaka ukweli halisi utakapobainika.
Bado kazi ya uchunguzi inaendelea kufanywa na vyombo vya usalama vya
nchi yetu wakishirikiana na wenzao wa nje.
Katika mazingira hayo, ni mapema mno kumnyooshea kidole mtu ye yote na
kuilaumu Serikali ya Muungano au Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Serikali siyo mshirika katika mauaji hayo,
na haina sababu ya kufanya hivyo. Ndiyo
maana tunahangaika usiku na mchana kupata jawabu.
Ndugu Wananchi;
Hali kadhalika tukio la Makanisa ya Mbagala, Dar Es Salaam kuvamiwa,
kubomolewa, mali kuibiwa na kuchomwa moto tarehe 12 Oktoba, 2012 nalo lina
mazingira yake maalum. Chanzo chake ni
mzozo uliotokana na tukio la kusikitisha la kijana mmoja Mkristo kukojolea Kitabu
Kitakatifu cha Waislamu, yaani Quran Tukufu.
Pamoja na maelezo kuwa walikuwa na ubishi wa kitoto na kijana mwenzake,
lakini kitendo hicho kiliwakasirisha Waislamu.
Kijana huyo alifikishwa kituo cha Polisi. Baadhi ya Waislamu wenye msimamo mkali
walifika kituoni hapo wakidai wapewe huyo kijana wamuadhibu wao. Jeshi la Polisi lilikataa. Kukatokea mzozo kati ya waumini hao na Polisi
na baada ya kushindwa walichokitaka baadhi yao walipotoka pale, wakaenda
kufanya uhalifu wa kuvunja, kuiba na kuchoma moto Makanisa.
Ndugu Wananchi;
Baada
ya tukio la Mbagala hapajakuwepo na tukio la kuchomwa Kanisa mahali popote kwa
upande wa Bara. Aidha, hapajawahi kuwepo
tishio lililothibitika la watu kutaka kuchoma Kanisa popote. Lakini maneno ya vitisho vya kuchoma Makanisa
yako mengi hasa kupitia mitandao ya simu za mkononi. Kila ujumbe wa namna hiyo ulipofikishwa
kwenye vyombo vya usalama uchunguzi umefanywa na hata hatua za tahadhari kuchukuliwa
lakini hakuna hata taarifa moja iliyothibitika kuwa na chembe ya ukweli. Hata dalili hazijakuwepo.
Tulichojifunza
ni kuwa ujumbe na vitisho vya aina mbalimbali hupelekwa kote, kwa Wakristo na
Waislamu. Upo unaowalenga Wakristo
ukiwaambia wenzao Waislamu wanapanga kuwadhuru.
Na upo wanaopelekewa Waislamu wakiambiwa Wakristo wanao mipango mibaya
dhidi yao. Watanzania wenzangu nawaomba
mtanabahi na mjue kuwa wapo watu wanacheza mchezo mchafu wa kuwagonganisha na kutaka
kuwagombanisha Wakristo na Waislamu kwa sababu wanazozijua wao na kwa faida
yao. Wanapandikiza chuki kwa lengo la
kutaka Wakristo na Waislamu wagombane.
Wanapandikiza chuki baina ya Serikali na waumini wa dini zetu kuu mbili
ili ionekane Serikali imewatelekeza raia wake.
Ni mchezo mbaya, tusikubali kucheza ngoma tusiyoijua. Hivi ndugu zangu
mmekaa chini na kujiuliza kumetokea nini kipya hata leo kuwa na mhemko kama huu
kati ya Wakristo na Waislamu na kutishia kuleta vita baina nchini kote?
Ndugu Wananchi;
Serikali haijapuuzia kila palipotokea matukio ya uhalifu. Watu 76 wanaotuhumiwa kuharibu na kuchoma
moto Makanisa kule Mbagala na kufanya fujo kituo cha Polisi wamekamatwa na kesi
zao zinaendelea Mahakamani. Kwa upande
wa tukio la Buseresere lililosababisha kifo cha Mchungaji Mathayo Kachila, watu
17, wakiwemo waumini wa dini ya
Kikristo na Kiislamu walikamatwa na kesi zao zinaendelea. Wapo walioshitakiwa
kwa mauaji na wapo walioshitakiwa kwa kufanya vurugu. Jeshi la Polisi bado linawatafuta watu
wengine waliohusika na uhalifu huo ili na wao wakamatwe. Kwa upande wa Zanzibar,
watu 10 wanaotuhumiwa kuchoma
Makanisa wamekamatwa na kesi zao zinaendelea.
Bado hajakamatwa mtu kwa tukio la mwisho la kuchoma Kanisa baada ya
kuuawa Padri Evaristus Mushi. Uchunguzi
unaendelea.
Ndugu Wananchi;
Kwa
upande wa kujeruhiwa kwa Padre Mkenda, bado uchunguzi haujakamilika pamoja na
kuwapo taarifa kadhaa zinazoendelea kufanyiwa kazi. Kuhusu uchunguzi wa mauaji ya Padre Mushi,
baada ya jitihada kubwa kufanyika ikiwa ni pamoja na kushirikisha nchi zilizobobea
katika uchunguzi wa makosa ya aina hii, hatua ya kutia moyo imefikiwa. Mtu mmoja amekamatwa na wengine wanaendelea
kutafutwa.
Ndugu Wananchi;
Kwa
upande wa kanda na vituo vya redio nako pia Serikali imechukua hatua. Watu kadhaa wamekamatwa na kufikishwa
Mahakamani katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwa kurekodi na kusambaza kanda
zinazochochea chuki na vurugu za kidini.
Wapo Waislamu na Wakristo. Wapo watu wengine ambao wanaendelea kutafutwa. Zipo taarifa kuwa baadhi yao wamekimbilia
nchi za nje. Jeshi la Polisi limeomba msaada wa Polisi wa Kimataifa, yaani
Interpol, kusaidia kuwatafuta na kuwarejesha nchini. Vituo viwili vya radio yaani Kwa Neema FM cha
Sengereme na Radio Imani cha Morogoro vimefungiwa kwa muda wa miezi sita. Baada ya muda huo kupita, Kamati ya Maudhui
ya Mamlaka ya Mawasiliano itaamua ipasavyo.
Ndugu Wananchi;
Nimeyaeleza haya kwa kirefu kuwahakikishia kuwa Serikali inajali usalama
wa raia wake wa mali zao na amani na utulivu wa nchi yetu. Kamwe hatujashindwa kulinda raia wa nchi wa
yetu na yapo mambo mengi yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika kuhakikisha
kuwa Watanzania wa dini zote, makabila yote, rangi zote na mahali po pote
walipo wako salama. Tunataka kuona watu wanaendelea
kuishi kwa amani, upendo, ushirikiano na mshikamano kama tulivyokuwa tunaishi siku
zote. Tunapenda kuona Watanzania
wanaepuka mambo yanayowabagua na kusisitiza yale yanayowaunganisha. Tujiepushe kuyapa kipaumbele yale
yanayotugawa.
Ndugu Wananchi;
Athari za mzozo kuhusu kuchinja kule Geita iwe fundisho kwetu
sote. Tuazimie sote kuwa yaliyopita si
ndwele, tugange yajayo. Hebu tufikirie
maisha yetu Watanzania yatakuwaje kwenye shughuli za kijamii kama vile sherehe,
harusi, ngoma na misiba iwapo tutaanza kuwa na chakula tofauti kwa Waislamu na
Wakristo. Fikiria itakuwaje kwenye hospitali, shule na vyuo pawe na majiko mawili au labda hata mabwalo
mawili ya chakula kwa Waislamu na Wakristo. Jeshini nako kuwe na majiko na mabwalo
ya Waislamu na Wakristo. Hali iwe hivyo
hivyo kwenye migahawa na maeneo mengine yenye huduma ya chakula.
Ndugu
zangu, tunataka kuipeleka wapi nchi yetu? Tunataka kujenga nchi ya namna gani?
Mimi naamini tukifanya hivyo huo utakuwa ndiyo mwanzo wa kubaguana kwa kila
kitu na kila jambo na kuligawa taifa kwa namna ambayo hatutakuwa wamoja tena. Huko tunakoelekea siko, ni kubaya. Tubadilike,
na wakati ni huu. Viongozi wa dini waongoze
njia wawaepushe waumini wao na taifa letu na janga hili.
Ndugu Wananchi;
Bado narudia kusisitiza umuhimu wa viongozi wa dini zetu kubwa
mbili kukutana na kuizungumzia hali hii na kuipatia ufumbuzi. Ni wao kuliko mtu mwingine ye yote wenye
majawabu ya matatizo haya. Ni masuala
yanayohusu imani za dini na yanafanywa na viongozi wa dini na wafuasi wao kwa
jina la dini zao. Serikali ina wajibu wa
kulinda amani. Kazi yetu itakuwa rahisi kama waumini hawatafanya vitendo
vitakavyosababisha uvunjifu wa amani. Wa kuongoza waumini lipi jema na lipi
baya ni viongozi wa dini.
Ndugu Wananchi;
Nimeshakutana na viongozi kadhaa wa madhehebu
na taasisi za dini za Kikristo na Kiislamu kuzungumza nao kuhusu jambo
hilo. Nimepata faraja kuona kuwa wote
wanasikitishwa na mambo yanayotokea hivi sasa na wameona busara ya viongozi wa
dini kuzungumza ili kuondoa tofauti zilizojitokeza. Wanakiri kuwa hali ilivyo sasa siyo ya
kawaida kwa Tanzania na Watanzania. Kuna
upepo mbaya wa shetani unapita ambao viongozi wa dini wana wajibu wa kuhakikisha
kuwa hali ya hewa inasafishwa na kurejesha nchi yetu na watu wake katika maisha
tuliyoyazoea. Maisha ambayo waumini wa
dini tofauti wanaishi pamoja kwa udugu, upendo, ushirikiano na mshikamano kwa misingi
ya ubinadamu wao na Utanzania wao.
Waziri
Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda, ameshaeleza dhamira ya Serikali ya kuitisha
mkutano wa viongozi wa dini mapema mwezi ujao.
Ni matumaini yangu kuwa wote watashiriki wenyewe bila ya kutuma
wawakilishi. Lazima tupate jawabu kwa
maslahi ya taifa letu na watu wake.
Ndugu Wananchi;
Kabla
ya kumaliza hotuba yangu napenda kutumia nafasi hii kuwaomba na kuwasihi
waandishi wa habari wasaidie kuliepusha taifa letu kuingia katika vita vya
kidini. Waache kushabikia taarifa
zinazochochea na kujenga uhasama baina ya waumini wa dini zetu. Nawaomba wapime athari za taarifa zao kabla
ya kuziandika au kuzitangaza. Wawe
makini na maneno wanayotumia. Katika
hali tuliyonayo sasa lazima sote tuazimie kuondoa tofauti za kidini na kujenga
umoja miongoni mwa Watanzania wa dini zote.
Wasipofanya hivyo, wataliingiza taifa katika mgogoro mkubwa ambao hauna
msingi kama ilivyotokea katika nchi jirani.
Nawaomba wamiliki wa vyombo vya habari kutambua kuwa wanao wajibu wa
kuhakikisha vyombo vyao havitumiki kuleta mifarakano kwa kuchochea uhasama
baina ya Wakristo na Waislamu.
Hitimisho
Ndugu Wananchi;
Naomba kumaliza kuwa kusisitiza kuwa wananchi wote kudumisha
umoja na mshikamano wetu. Tuishi kwa
upendo, umoja, mshikamano na ushirikiano bila kujali tofauti ya dini zetu,
kabila, rangi au mahali atokako mtu.
Hizo ndizo tunu za taifa letu la Tanzania ambazo hatuna budi kuzienzi,
kuzilinda na kuzidumisha. Narudia kuwahakikishia kuwa Serikali haipendelei dini
yo yote na wala haina mpango wa kushiriki kuangamiza dini yo yote au waumini
wao. Serikali kupitia vyombo vyake vya
usalama itaendelea kuhakikisha ulinzi na usalama wa raia wake na mali zao kama
inavyofanya siku zote. Kama kuna mtu
anaona kuwa maisha yake au mali zake zipo hatarini, aende kutoa taarifa Polisi. Hatua zipasazo zitachukuliwa.
Ndugu Wananchi;
Mwisho
nawatakia sikukuu njema ya Pasaka.
Tusherehekee kwa amani na utulivu.
Tusherehekee pamoja.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa Kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment