TANGAZO


Tuesday, March 19, 2013

Rais Kikwete awataka TFDA kutobweteka na mafanikio wanayoyapata


Na Frank Shija – Maelezo
19/3/2013

RAIS Dk. Jakaya Mrisho Kikwete amewataka Watendaji wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), kutobweteka na mafanikio wanayoyapata bali  waendelee kufanya kazi kwa bidii na uadilifu kwa kuwa  taasisi hiyo ni muhimu kwa maisha ya Watanzania na nchi jirani ambao wameonesha imani na kuanza kuitumia kuchunguza sampuli zao.

Wito huo umetolewa leo, wakati wa  uzinduzi wa maabara ya kisasa ya uchunguzi wa bidhaa za chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba zilizopo Makao Makuu ya TFDA, jijini Dar es Salaam.

Rais Kikwete, alisema kuwa kazi inayofanywa na Taasisi hiyo ya kudhibiti, kusimamia ubora na usalama wa bidhaa za chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba ni nzuri na inatakiwa kuigwa na taasisi zingine kwani wanalinda na kuboresha afya ya mlaji.

Dk. Kikwete alisema, “Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi mbalimbali mnazozifanya  ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma  na hatimaye muweze kufikia malengo yenu  ikiwa ni pamoja na kuwa na maabara bora zaidi barani afrika”.

Katika kutekeleza hilo Rais Dk. Kikwete alisema  kwamba  Serikali itahakikisha kunakuwa na upatikanaji wa rasilimali zitakazosaidia kuongeza tija katika utendaji kazi na kutatua tatizo la wataalamu wa vifaa vya maabara na kuona jinsi gani  fani hiyo inafundishwa vyuoni.
Kwa upande wake Naibu waziri wa Afya na Ustawi wa jamii Dk. Seif Rashid aliishukuru Serikali na mashirika rafiki ambayo  yamechangia kwa kiasi kikubwa kukamilisha ujenzi wa maabara hiyo.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TFDA Hiiti Sillo liiomba Serikali kuboresha maslahi ya wafanyakazi wa taasisi hiyo ili waweze kufanya kazi wakiwa na hari nzuri na kuahidi kuwa wataendelea kuwajibika kadri wawezavyo ili waweze kutimiza wajibu wao kwa jamii.
“Pamoja na uhaba wa wafanyakazi na wataalamu wa maabara tulionao, tutaendelea kufanyakazi kwa weledi na uadilifu mkubwa ili kuhakikisha kuwa tunalinda usalama na ubora wa bidhaa za chakula zinazoingia nchini.” Alisema Hiiti.

Gharama za ujenzi na ukarabati wa maabara hiyo ni shilingi billion 2.7 fedha ambazo zimetokana na michango ya Serikali na wafadhili kutoka  Global Fund,Shirika la Misaada la Watu wa Marekani(USAID), Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo ya Viwanda (UNIDO), Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Watoto(UNICEF),Shirika la Kimataifa linaloshughulikia masuala ya chakula na lishe (Hellen Keller International - HKI) na Shirika la Afya Duniani(WHO).

No comments:

Post a Comment