Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Fakihi Haji Mbarouk akitoa hotuba ya makaribisho kwa waandishi wa habari waliohudhuria katika Mkutano wa kutoa mapendekezo ya marekebisho ya Sheria namba 5 ya mwaka 1985, hapo katika ukumbi wa Hoteli ya Bwawani Zanzibar, mjini Zanizibar leo. (Picha zote na Yussuf Simai - Maelezo, Zanzibar)
Afisa wa Habari kutoka Idara ya Habari Maelezo, Zanzibar, Faki
Mjaka akitoa ufafanuzi wa baadhi ya mambo katika Mkutano wa
kutoa mapendekezo ya marekebisho ya sheria namba 5 ya mwaka
1985 hapo katika ukumbi wa Hoteli ya Bwawani Zanzibar. Kulia ni
mwandishi kutoka Redio Adhana, Said Suleiman.
Waandishi mbalimbali wakipitia sheria namba 5 ya mwaka 1985, inayotaka kufanyiwa marekebisho hapo katika ukumbi wa Hoteli ya Bwawani, mjini Zanzibar leo.
Baadhi ya Waandishi wa Habari waliohudhuria katika Mkutano wa kutoa mapendekezo ya marekebisho ya Sheria namba 5 ya mwaka 1985, wakiwa katika mkutano huo, ukumbi wa Hoteli ya Bwawani Zanzibar.
Mwandishi wa Habari wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar, Miza Kona
Ngwali akitoa maoni kuhusu marekebisho ya Sheria namba 5 ya mwaka 1985 hapo
katika ukumbi wa Hoteli ya Bwawani, mjini Zanzibar.
Na Ali Issa Maelezo Zanzibar 19/3/2013
IMEELEZWA kuwa ipo haja ya kufanywa marekebisho ya haraka
kwa Sheria ya Magazeti ya Zanzibar ya mwaka 1988 kutokana na sheria hiyo
kupitwa na wakati.
Aidha, katika zama hizi za uwazi na demokrasia suala la
upatikanaji wa habari ni muhimu sana katika kukuza uwajibikaji lakini sheria
hiyo ya Magazeti inawanyima watu fursa ya kupata habari hizo.
Hayo yameelezwa na Waandishi wa Vyombo mbali mbali vya
habari katika Mkutano wao wa kutoa mapendekezo yanayohusu marekebisho ya Sheria
namba 5 ya mwaka 1988 huko katika Hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar leo.
Akichangia katika Mkutano huo mmoja wa Washiriki alisema
katika sheria hiyo Polisi wamepewa Mamlaka ya kupekuwa katika Chumba chochote
cha habari bila kipingamizi chochete kwa kile kinachodaiwa kumtilia mwandishi
mashaka.
“Kwa kweli sheria hii inamfanya hata Mwandishi kuwa muoga wa
kazi yake maana Polisi kapewa Mamlaka ya kupekuwa hata chumba cha habari iwapo tu
atakutuhumu hivyo tunaomba sheria ambayo walau Jeshi la Polisi litafanya
upekuzi kwa kushirikiana na wadau wengine wa habari” Alisema Mwashamba Juma.
Aidha Waandishi hao waliilezea Sheria hiyo kuwa inatoa
Mamlaka kupindukia kwa Waziri wa habari na Mkurugenzi wa Habari kufanya maamuzi
wanayoyataka bila hata kuwekewa kipingamizi chochote.
“Kwa mujibu wa sheria hii Waziri tu pengine kwa utashi wake
bila hata kushirikiana na mtu yeyote anaweza kuamka na kusema Gazeti fulani
nimelifungia na ikakubalika kulingana na Mamlaka aliyopewa kisheria” Alisema
Ali Bakar.
Waandishi hao pia waligusia kipengele cha adhabu kwa mtu
atakayekiuka sheria hiyo nakupendekeza kuwa kunahitajika marekebisho ili
iendane na wakati.
“Tunapendekeza adhabu ya kifungo na faini vilingane viwe na
uwiano,haiwezekani faini shilingi elfu tano na kifungo miaka mitatu,”
alibainisha Miza Kona.
Awali akitoa nasaha zake Kaimu Mkurugezi wa Idara ya Habari
Maelezo Zanzibar Fakih Haji Mbaruok aliwataka Waandishi hao kutoa mawazo
yatakayowezesha kupatikana kwa sheria inayokidhi maslahi ya Taifa na wakati
uliopo.
Amesema umakini unahitajika kwa waandishi hao ili kupatikana
kwa sheria ambayo haitotoa upendeleo au kumkomoa mtu yeyote katika kufanya kazi
zake.
“sheria ni sheria ikipitishwa imepita wandishi tuwe makini
kwa kuiangalia sheria hii kwa mapana na kupendekeza maoni yetu kwani sheria
kawaida inagusa maisha ya watu na sisi ni wahusika wa moja kwa moja wa sheria
hiyo”, alisema Fakih.
Mkutano huo ambao umefadhiliwa na Shirika la Maendeleo la
Umoja wa mataifa la Elimu,Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ni watatu kufanyika
katika kutoa mapendekezo kwa ajili ya marekebisho ya sheria ya namba tano ya magazeti
ya mwaka 1988
No comments:
Post a Comment