Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete |
Na Anna Nkinda – Maelezo, Sumbawanga
KINAMAMA wajawazito wametakiwa kuhudhuria kliniki mapema pale wanapojitambua kuwa na
ujauzito, hii itawasaidia kupata huduma mbalimbali za afya ikiwa ni pamoja na
kupima afya zao na kuona kama wana maambumbukizi ya Virusi Vya Ukimwi
(VVU) au la, na hivyo kujifungua salama mtoto asiye na maambukizi ya ugonjwa
huo.
Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete alipokuwa akiongea na wananchi wa Wilaya ya Kalambo, mkoani Rukwa wakati akikabidhi pikipiki 10 za programu ya kuzuiya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT), zilizotolewa kwa ufadhili wa Walter Reed HIV/AIDS Program.
Mama
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na
Maendeleo (WAMA) alisema kuwa Serikali pamoja na wadau mbalimbali wa afya
wanahangaika kuhakikisha kuwa watoto watakaozaliwa hawana maambukizi ya VVU
kwani dawa za kuzuia maambukizi zipo ni jukumu la kina mama kuhudhuria kliniki
mapema na kupima afya zao.
“Janga la
Ukimwi ni tatizo kubwa kwa jamii yetu. Natoa Rai kwa wananchi wote
tuwe waangalifu kujikinga na ugonjwa huu. Kutokana na takwimu
zinaonyesha kuwa hali ya maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda
kwa mtoto (PMTCT) kwa Mkoa huu ni 5.6% hivyo basi uwepo wa baba unatakiwa
ili kuboresha afya ya mama na mtoto”, alisema Mama Kikwete.
Mwenyekiti huyo wa WAMA pia aliwaasa wote waliokabidhiwa pikipiki hizo kuzitunza na kuzitumia kwa malengo yaliyokusudiwa. Na kuwakumbusha kuwa pikipiki hizo ni kwa ajili ya ukusanyaji wa sampuli za damu kutoka vituo vilivyo mbali zaidi na wilaya na kuvipeleka kwenye Maabara ya Kanda na pia kuimarisha mawasiliano kati ya kituo na kituo na si vinginevyo.
Akisoma
taarifa ya mradi huo Mratibu wa Kudhibiti Ukimwi Mkoa wa Rukwa Dk.
Shadrack Mtulla alisema kuwa wana vituo vya kutolea huduma za afya 267 kati ya
hivyo 177 vinatoa huduma PMTCT ambavyo ni sawa na asilimia 66 ya vituo vyote
na kipindi cha mwaka 2012 jumla ya akina mama 3189 waliandikishwa
katika vituo vya kutolea huduma na malezi yaani CTC na kupewa dawa za
ARV.
Alisema
kuwa , kwa kushirikiana na Walter Reed HIV/AIDS Program katika mapambano dhidi
ya ugonjwa wa Ukimwi kwa kipindi cha mwaka 2012/2013 wamenunua pikipiki 10
ambazo zitagawanywa katika vituo vya afya ambavyo viko mbali na
makao makuu ya wilaya katika wilaya zote za mkoa huu.
Dk.
Shadrack Mtulla alisema, “Upatikanaji wa pikipiki hizi utarahisisha ukusanyaji
wa sampuli za damu kutoka vituo vilivyopo mbali zaidi na wilaya, na kuzileta
katika maabara tayari kwa kuzisafirisha kwenda katika maabara za kanda
pia zitaboresha mawasiliano kati ya kituo na kituo na hivyo kurahisisha
ukusanyaji wa takwimu kutoka vituo mbalimbali kwa muda uliopangwa”, Dk. Shadrack
Mtulla.
Dk.
huyo alizitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni upungufu mkubwa
wa vyombo vya usafiri hususani magari kwani mkoa huo una magari mawili na
mahitaji halisi ni sita, upungufu wa wataalamu wa afya vituoni
,watumishi walioko katika vituo vya kutolea huduma ni asilimia 35 na upatikanaji
wa vitendanishi usiokidhi mahitaji ya mkoa na wilaya zake.
Pikipiki hizo zilikabidhiwa kwa wakurugenzi
wa halmashauri za wilaya ya Sumbawanga tatu kwa ajili ya vituo vya Afya vya
Milepa, Kasanga na Mwitu, Nkasi mbili kwa ajili ya vituo vya afya Kirando na
Kilangalanga, Manispaa ya Sumbawanga mbili ambazo zitatumika katika vituo vya
afya vya Ntembo na Ulinji, Mji wa Mpanda moja kwa ajili ya kituo cha Afya
Mwangaza na wilaya ya Mpanda ambazo zitatumika katika vituo vya afya Mamba na
Mishano.
No comments:
Post a Comment