Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete, ameyataka Makampuni na Mashirika binafsi
kuwasaidia yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi ili nao
wajisikie kuwa wanahaki ya kupata furaha na mapenzi kama watoto wengine na kuongeza kuwa hali hiyo itazidi kuwajengea upendo baina yao na watoto
wengine.
Mama
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA)
ameyasema hayo leo wakati wa chakula cha mchana kwenye sherehe ya mwisho wa
mwaka ya watoto yatima iliyofanyika katika viwanja vya Taasisi hiyo vilivyopo
jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti
huyo wa WAMA alisema kuwa alipoanzisha taasisi hiyo moja ya malengo yake ilikuwa
ni kuwasaidia watoto yatima na wale wenye uhitaji maalum katika nyanja zote
hususani ya elimu.
“Nilipata
msukumo wa kufanya shughuli hizi kwani nimeona ni wajibu wangu nikiwa kama
mwanamke na vilevile mama wa familia na pia kwa kufahamu kuwa Serikali ya
Tanzania inatambua umuhimu wa kuboresha elimu kwa jamii hususani watoto hivyo
inahitaji kusaidiwa na taasisis zisizo za kiserikali ili kufanikisha suala
hili”, alisema Mama Kikwete.
Aliyaomba
makampuni hayo wasichoke kuwasaidia watoto hao bali waendelee na moyo wa
kuwasaidia kwa kupeleka mahitaji muhimu ya kibinadamu kwenye vituo vyao na kisha
kujumuika nao katika hafla kama hiyo kwani ni jambo muhimu sana kwa taifa na kwa
watoto kwakuwa wanapata faraja kubwa.
Chakula
hicho cha mchana kiliandaliwa na Taasisi ya WAMA kwa kushirikiana na kampuni ya
Simenti ya Twiga na Rotary Club. Watoto waliohudhuria sherehe hizo ni kutoka
Kituo cha watoto yatima cha Malaika cha Mkuranga, Umra cha
Magomeni, Kurasini, Mama Lenga kutoka Kigogo na Kituo cha watoto Yatima
cha Kiislamu cha Mwandamila cha Boko.
No comments:
Post a Comment