Kaimu Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es Salaam (CBE), Athman Ahmed (kulia), akitoa taarifa kuhusu mahafali ya 47 na maendeleo ya chuo hicho, kwa mgeni rasmi wa mahafali hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Joyce Mapunjo (katikati), wakati wa mahafali hayo juzi jioni.
Baadhi ya wahitimu wa shahada ya Masoko katika Chuo cha Biashara Dar es Salaam wakiweka kofia zao sawa mara baada ya kumalizika kwa tamko la kuwatunuku shahada hiyo.
Wahitimu wa mahafali ya 47 ya Chuo cha CBE, wakifuatilia masuala mbalimbali yaliyokua yakiendelea wakati wa mahafali hayo, viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wananchi na wapiga picha wa kujitegemea waliohudhuria mahafali ya 47 ya Chuo cha CBE, Dar es salaam wakiendelea kufuatilia matukio mbalimbali wakati wa sherehe hizo. (Picha zote na Aron Msigwa – MAELEZO)
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
Dar es salaam.
WAHITIMU wa Chuo cha
Elimu ya Biashara Dar es Salaam wametakiwa kutumia fursa na elimu waliyoipata
wakati wa masomo yao, kujiajiri wenyewe badala ya kusubiri, ilI
kupunguza ongezeko kubwa la vijana wasio na ajira mitaani.
Akizungumza na wahitimu 2882 wa fani
mbalimbali wa chuo hicho wakati wa mahafali ya 47 yaliyofanyika juzi jioni
jijini Dar es salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Bi. Joyce
Mapunjo amewataka vijana hao kutumia elimu yao kujiajiri wenyewe na kutengeza
ajira kwa vijana wengine wanaohangaika kutafuta kazi kila kukicha.
Amewataka wahitimu hao kuwa mfano wa
kuigwa katika jamii na kutumia elimu yao kutatua matatizo mbalimbali
yanayoikabili jamii na kuwaasa kujiepusha na vitendo vya uhalifu, anasa na
kujikinga na maambukizi ya VVU.
Kuhusu kukisaidia chuo hicho Bi.
Joyce amesema kuwa serikali itaendelea kukisaidia chuo hicho kifedha ili
kiweze kutimiza malengo mbalimbali kiliyojiwekea na kutoa wito kwa viongozi
wa chuo hicho kuongeza ubunifu katika kutafuta vyanzo mbalimbali vya mapato
ya chuo hicho.
Aidha amesema kuwa ongezeko la
wahitimu wa kike kwa asilimia 49 katika fani mbalimbali katika
chuo hicho ni jambo la kujivunia na kuwapongeza wakufunzi wa chuo hicho kwa
kazi nzuri wanayoifanya ya utoaji wa elimu bora.
Naye kaimu mkuu wa Chuo hicho Bw.
Athman Ahmad amewapongeza wahitimu hao waliotunukiwa vyeti katika fani 30 na
kuwataka kutumia ipasvyo elimu waliyoipata kwa manufaa ya taifa kwa kufanya
kazi kwa bidii na kuepuka tama ya kutaka kupata utajiri kwa muda mfupi pindi
wanapofanikiwa kujiajiri au kuajiriwa.
“Nawaomba muwe wavumilivu na
mjiepushe na vitendo vya kihalifu na kutaka kupata utajiri kwa kipindi
kifupi, najua ninyi ni vijana na mnatamani vitu vingi kwa wakati mmoja cha
msingi mfanye kazi kwa bidii, uaminifu na kuepuka tamaa zinazoweza kuwafanya
muingie katika vitendo viovu” amesema.
Bw. Ahmad amesema licha ya chuo hicho
kukabiliwa na changamoto ya udogo wa eneo na uchakavu wa miundombinu pia kina
kabiriwa na uhaba wa walimu 20 kuongezea idadi ya 80 waliopo sasa na tayari
juhudi mbalimbali zinaendelea kufanyika ili kuboresha huduma za elimu chuoni
hapo na kuondoa tatizo la uhaba wa madarasa na walimu.
Amesema chuo hicho kina muda mrefu
tangu mwaka 1965 na tayari majengo yake hayana uwezo wa kuchukua wanafunzi
wengi kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi na mwamko mkubwa wa watanzania
katika masuala ya elimu jambo linalowafanya kulazimika kukodi madarasa nje ya
chuo.
“Chuo kilipoanzishwa mwaka 1965
kilikua na wanafunzi 30 na leo hii kwa eneo la Dar es salaam tuna wanafunzi
takribani 9000 hili ni jambo linalohitaji uboreshaji wa miundombinu na
uongezaji wa majengo mapya ili kukabiliana na changamoto hiyo” amesema Bw.
Ahamad .
Kaimu mkuu wa chuo hicho amefafanua
kuwa hivi sasa chuo kina mkakati wa kuongeza mafunzo ya shahada ya
uzamili na kuongeza majengo ya madarasa katika kampasi zote 3 za Dar es
salaam, Dodoma na Mwanza.
“Jambo hili tuko makini nalo na sasa
kazi ya uchoraji wa michoro na juhudi za kutafuta fedha wakiwemo
wafadhiri zinaendelea kufanyika ili kuweza kukamilisha mipango hiyo.
Mahafali hayo ya 47 yaliyofanyika
jana jioni katika viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar es salaam yalihudhuriwa
na wananchi kutoka maeneo mbalimbali na viongozi wa Bodi ya Chuo hicho
wakiongozwa na Prof. Mathew Luhanga kutoka Chuo kikuu cha Uhandisi na
Teknolojia cha Chuo kikuu cha Dar es salaa na yatafuatiwa na mahafali
mengine katika kampasi ya Dodoma tarehe 1 na tarehe 8 mwezi Desemba katika
kampasi ya Chuo cha Elimu ya Biashara Mwanza
|
No comments:
Post a Comment