TANGAZO


Saturday, November 10, 2012

TPB yawakutanisha Wakuu wa benki hiyo kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kujadili uboreshaji huduma

Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Posta, S. Moshingi

Na Mery Kitosio, Arusha

BENKI ya Posta Tanzania (TPB),  imewakutanisha Wakurugenzi Wakuu wa benki hiyo pamoja na  wajumbe wa bodi wa benki hiyo, kutoka  nchi wanachama wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki kwa lengo la kuangalia jinsi ya kuboresha huduma zake kwa wateja wadogo wadogo na kuhakikisha wanapata huduma bora.

Hayo, yalielezwa leo na Mkurugenzi Mkuu wa benki ya Posta Tanzania, Bw. Sabasaba Moshingi wakati alipokuwa akizungumza na wajumbe wa bodi wa benki hiyo kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika  mkutano wa siku mbili uliofanyika mjini hapa.

Alisema kuwa  kupitia mkutano huo ambao umekutanisha wajumbe wa bodi kutoka nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki, wataweza kujadili mambo mbalimbali, hususan ambayo yanalenga kuboresha huduma za wateja wadogo wadogo katika jamii inayowazunguka.

“Benki ya Posta, imejiwekea utaratibu maalum wa kuhakikisha kuwa kila mahali wateja walipo, wanapata huduma nzuri na yenye uhakika hivyo kupitia umoja wetu wa hizi nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki tutaweza kuungana kwa pamoja tukawa na nguvu kubwa zaidi,” alisema Moshingi.

Aidha, alieleza kuwa kupitia mkutano huo pia wataweza kuangalia uwezekano wa kujiunganisha katika mtandao  wa nchi za Kenya, Uganda na Tanzania ili kuhakikisha kuwa wateja wao wanapata huduma bora pindi wakiwa katika moja ya nchi hizo.

“Tukishajiunganisha katika mtandao wa nchi hizi, itasaidia sana kurahisisha huduma kwani ukiwa nchi nyingine unaweza kupata huduma nzuri na wakati tofauti na pale ambapo wateja wetu wanategemea tu nchi moja,“ aliongeza.

Aliongeza kuwa kuunganika kwa mtandao wa nchi hizo, kutasaidia hata kurahisisha shuguli za maendelao kama vile biashara na kulipa hata ada ya mtoto endapo atakuwa anasoma nje ya nchi husika.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa benki hiyo, kutoka nchini Kenya Nyambura Koigi, alisema kuwa kupitia mkutano huo uliokutanisha wakuu wa benki hiyo, utasaidia kwa kiasi kikubwa kuunganisha wateja wa benki hiyo na kuwa na umoja ambao utaimarisha mahusiano mazuri.

Aidha, alisema kuwa benki hiyo, imeshaweka mpango mkakati wa kuhakikisha kuwa inaboresha huduma popote pale walipo ili wateja wadogo wadogo wanufaike nazo kwa muda wowote.

No comments:

Post a Comment