Na Mwanaisha Muhammed Maelezo Zanzibar
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Mjini Kichama, Borafya Silima Juma amewataka wanachama wa chama hicho, kuzidisha umoja na mashirikiano ili kukiletea maendeleo chama hicho na taifa kwa ujumla.
Ameyasema hayo huko Tawi la CCM Magomeni Mzalendo leo katika hafla ya kuwapongeza viongozi wa Jimbo hilo waliochaguliwa hivi karibuni kushika nyadhifa mbali mbali za Wilaya, Mkoa na Taifa kufuatia chaguzi za Chama hicho.
Borafya amesema hali ya kisiasa katika Chama cha Mapinduzi imetengemaa baada ya kufanyika kwa chaguzi hizo.
Aliwaomba viongozi wa Chama kuwa karibu na wananchama sambamba na kupokea matatizo yao kwa usikivu na ustahamilivu mkubwa.
“Ndugu zangu naomba nikufahamisheni kuwa uongozi ni dhamana hivyo muwe tayari kukosolewa pindi yanapotokezea matatizo kwani hakuna mkamilifu isipokuwa Mungu”.
Hata hivyo amevitaka vyama vya siasa Zanzibar viachane na siasa za chuki na uhasama ili ifikapo mwaka 2015 uchaguzi uwe huru na salama pasi na fujo wala vurugu .
Naye Katibu wa Uchumi na Fedha wa Jimbo hilo Arafa Ali wakati akisoma Risala amesema hafla hiyo imekuja ikiwa ni mkakati wa kuimarisha chama chao kwa lengo la kuendelea kuongoza dola.
Arafa alisema kuwa kwa sasa wameamua kuendeleza uboreshaji wa michango kwa wanachama wote ili waweze kukabiliana na jambo lolote litakalowakabili .
Mapema viongozi hao na wananchama wao wamewapongeza viongozi wote wa Tanzania bara na Zanzibar kwa ushindi mkubwa walioupata huko Kizota Dodoma na kuwataka waongeze nguvu za ziada katika kuwaletea maendeleo wananchi siku hadi siku.
No comments:
Post a Comment