Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akitoa hotuba ya Ufunguzi wa Mkutano wa 36 wa Baraza la Utawala la ARIPO, linaloratibu na kusimamia haki za Mali za wabunifu Barani Afrika huko katika Ukumbi wa Zanzibar Beach Resort, ulioko Mazizini, nje ya Mji wa Zanzibar. (Picha na Yussuf Simai-Maelezo, Zanzibar)
Na Ramadhan Ali, Habari Maelezo Zanzibar
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema ipo haja kwa Baraza la Utawala linaloratibu na kusimamia haki za Mali za Ubunifu Afrika (ARIPO) na Jumuiya za Kimataifa zinazosimamia sekta hiyo, kuandaa miongozo na kuimarisha mikakati itakayo wabana wezi wa haki miliki.
Amesema uporaji wa haki miliki umekuwa ukiendelea kwa kasi Duniani kote na kupelekea hasara kwa vitega uchumi vya Wasanii, Watengenezaji filamu na muziki ambapo hupelekea hasara kwao na mataifa yao kwa jumla.
Makamu wa kwanza wa Rais ameeleza hayo leo, alipokuwa akifungua mkutano wa 36 wa ARIPO unaofanyika kwa mara ya kwanza Zanzibar katika Hoteli ya Zanzibar Beach Resort, Mbweni.
Amesema Tasnia ya haki miliki inamchango mkuwa katika kukuza maendeleo ya kiuchumi ndani ya nchi na kuongeza maslahi kwa wamiliki wa kazi za ubunifu iwapo zitalindwa.
Amewaeleza wajumbe wa Mkutano huo kwamba Zanzibar imeamua kuanzisha utaratibu wa Haki Miliki kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania ya kuweka alama ya utambulisho (nembo) kwa zao lake la karafuu na viungo ili kuimarisha usafirishaji wa mazo hayo na kuongeza pato la taifa.
Amesema Serikali kwa msaada mkubwa wa Shirika la Mali za Ubunifu Duniani (WIPO) zinaandaa utaratibu mwengine wa kuweka sera ya kulinda mali za ubunifu nchini ili kuzilinda na maharamia wa kazi hizo.
Makamu wa kwanza wa Rais ameipongeza ARIPO kwa kuendeleza utaratibu wa kuandaa mafunzo ya muda mrefu na mfupi wa kuzijengea uwezo Taasisi na wadau wengine wanaohusika na kazi za ubunifu katika Bara la Afrika.
Hata hivyo amewaeleza wajumbe wa Baraza la Utawala la ARIPO kwamba masuala ya Utawala wa mali za ubunifu na haki miliki sio ya Muungano na kila upande unahaki ya kuandaa utaratibu na sera zake zinazokubaliana na mazingira yao licha ya kuwa na lengo moja.
Maalim Seifa amelipongeza Shirika la Kimataifa la Ushirikiano la Korea (KOICA) kwa kazi kubwa wanayofanya ya kuisaidia ARIPO na nchi wanachama wa Baraza hilo kuimarisha mfumo wa Teknolojia ya Habari na kupunguza tofauti iliyopo kati ya mataifa yaliyoendelea na yale yanayoendelea duniani.
Mwenyekiti wa Mkutano huo ambae ni Naibu Mrajisi nchini Ghana Bi Jemima Oware amesema ulinzi wa mali za ubunifu na masuala ya haki miliki yanapewa umuhimu mkubwa katika Baraza la ARIPO ili kunyanyua maslahi kwa wabunifu.
Mkutano huo wa wiki moja unahudhuriwa na wajumbe zaidi ya 75 wakiwemo nchi 18 wanachama wa ARIPO, Shirika la Dunia la Mali za Ubunifu WIPO, Wawakilishi wa Jumuiya ya Ulaya, Shirika la Kimataifa la KOICA na wajumbe kutoka nchi waalikwa.
No comments:
Post a Comment