Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa Mhashamu Baba Askofu Aloysious Balina wa Jimbo Katoliki la Shinyanga wakati wa mazishi wa Askofu huyo, kwenye Kanisa la Mama wa Huruma, Ngokolo, mjini Shinyanga leo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete akiweka udongo kwenye kaburi la Askofu Aloysius Balina wakati wa mazishi ya Askofu huyo leo, kwenye Kanisa la Mama wa Huruma, mjini Shinyanga.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete akiweka shada la maua kwenye kaburi la Askofu Aloysius Balina wa Jimbo Katoliki la Shinyanga wakati wa mazishi ya Askofu huyo kwenye Kanisa la Mama wa Huruma, Ngokolo, Shinyanga leo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete akimpa pole na kumfariji Mama Theresia Nigo, mama yake mzazi Askofu Aloysius Balina wakati wa mazishi ya Askofu huyo, kwenye Kanisa la Mama wa Huruma, Ngokolo, mjini Shinyanga leo.
Na Salvator Rweyemamu, Shinyanga.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameungana na mamia kwa mamia ya
waumini wa Kanisa Katoliki kumzika Askofu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga,
Mhashamu Baba Askofu Aloysius Balina yaliyofanyika kwenye Kanisa la Mama wa
Huruma, Parokia ya Ngokolo, mjini Shinyanga leo.
Rais Kikwete ambaye amekwenda Shinyanga
akitokea Dodoma ambako anaendesha vikao muhimu vya Chama cha Mapinduzi
amewasili kwenye Kanisa hilo kiasi cha saa sita mchana kwa ajili ya mazishi ya
Askofu Balina ambaye alifariki dunia Novemba 6, mwaka huu katika Hospitali ya
Rufaa, Mwanza kwa ugonjwa wa saratani.
Mara baada ya kuwasili Kanisani hapo,
Rais Kikwete ametia saini kitabu cha maombolezo na kujiunga na viongozi wa
Kanisa hilo na wa Serikali akiwamo Rais Mstaafu Mheshimiwa Banjamin Mkapa na
Mama Maria Nyerere kushiriki katika mazishi ya kiongozi huyo wa Kanisa
Katoliki.
Kabla ya kutoa salamu zake za
rambirambi, Rais Kikwete amesikiliza salamu za rambirambi za Kiongozi wa Kanisa
Katoliki Duniani, Baba Mtakatifu Benedict wa 16, na pia amesikiliza Amri ya Kitume
ya Kuhani Mkuu huyo wa Kanisa hilo, iliyotangaza kuteuliwa kwa Baba Askofu Mkuu
wa Jimbo Kuu la Mwanza, Mhashamu Juda Thaddeus Ruwa’ichi kuwa Msimamizi wa Kitume
wa Jimbo la Shinyanga hadi atakapoteuliwa askofu mpya wa jimbo hilo.
Amri hiyo imetolewa na kutiwa saini na
Katibu wa Kongresio ya Uinjilishaji wa Kimataifa na Rais wa Jumuia ya Kazi za
Kipapa Duniani, Askofu Mkuu Protase Rugambwa na kusomwa na Balozi wa Baba
Mtakatifu katika Tanzania, Askofu Mkuu Francisco Montecillo Padilla.
Katika salamu zake zake rambirambi
ambazo amezielekeza kwa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu
Tracisius Ngalalekumtwa na waumini wa Kanisa Katoliki, Rais Kikwete amemwelezea
Askofu Balina kama kiongozi mwadilifu na mchapakazi ambaye hukuchoka katika
maisha yake kutumia nafasi zake mbali mbali alizozishikilia katika maisha yake kuwasaidia
binadamu wenzake.
Rais Kikwete pia ameelezea jitihada
ambazo yeye na Askofu Balina walizifanya katika kusaka fedha za kupanuliwa kwa
Hospitali ya Rufaa ya Bugando iliyoko Mwanza.
Baada ya kutia udongo kwenye kaburi la
Askofu Balina na kuweka shaha ya maua kwenye kaburi hilo, Rais Kikwete alimpa
pole na kumfariji Bibi Theresia Nago ambaye ni mama yake mzazi Askofu Balina
kabla ya kuondoka Kanisani hapo.
Askofu Balina alikuwa Askofu wa nne wa
Jimbo la Shinyanga nafasi aliyoishikilia kwa miaka 16 na kabla ya hapo alikuwa
Askofu wa Jimbo la Geita kwa miaka 12. Askofu Balina alikuwa askofu kwa miaka
28 na padre kwa miaka 41.
Aidha, Askofu Balina alikuwa Mkuu wa
Idara ya Afya ya TEC kwa miaka mingi na pia alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya
Wakurugenzi ya Hospitali ya Bugando.
Rais Kikwete amerejea mjini Dodoma
jioni ya leo kuendelea na vikao vyake vya CCM.
No comments:
Post a Comment