Na Kassim Mbarouk
Sikuweza kuelewa mara moja nini kimetokea bandarini Zanzibar, mara tu baada ya kukanyaga gati ya Unguja, nilianza kuona mambo ya ajabu ajabu bandarini hapo, lakini nafikiri hiyo ilichangiwa sana na mimi kutofika Zanzibar mara kwa mara.
Sikuamini niliposikia mmoja wa askari aliyevalia sare ya magwanda ya bluu, akimjibu abiria aliyekuwa akilalamika usumbufu anaoupata pamoja na abiria wengine sehemu ya kukagulia mizigo mara ushukapo kwenye chombo, askari huyo, nilimsikia akipaza sauti yake akisema kuwa, "sisi tupo hapa makusudi kuwapotezea muda', na mwengine akadakia "leo tutasachi hata vipima joto (mikoba ya akinamama inayowekwa begani ambayo huweka vifaa wanavyovijua wenyewe), hizo zilikuwa ni kauli zinazotoka watu waliopewa dhamana na Serikalia ili kutekeleza majukumu yao kwa haki huku akitamka kwamba ataitumikia Serikali iliyopo bila upendeleo, chuki, ubaguzi na pia kutoa ahadi kuwa hatatoa wala kupokea rushwa.
Hafla na mimi nikaona ninavutwa begi langu na kuambiwa wewe mzee peleka kule begi lako (sehemu ya kukaguliwa), basi sikufanya ubishi, harakaharaka nikapeleka begi kwa kuwa nilitaka kuwahi ili usiku nisafiri kuelekea kisiwani Pemba ambako ziara yangu nilipanga ianzie huko, begi lililokuwa na nguo zangu tu nikalipeleka kukaguliwa lakini askari aliyefanya upekuzi huo, alipekuwa begi kama vile sijui amenihisi mimi ni gaidi anayetisha sana, maana hakuacha hata sehemu ya begi bila kuipekuwa.
Hali ile sikuweza kuivumilia kwa kuwa mimi ni mmoja wa watu wanaochukia mwingine kumtese mwenzake, nikauliza leo kulikoni ? Hapo hapo nilijibiwa na kijana ambaye alikuwa kando akisubiri abiria, sikujua kama alikuwa dereva tex ama mtu wa kati, lakini alibainisha kuwa alikamatwa kijana akiwa na unga (madawa ya kulevya) na akaongeza kuwa kijana huyo, alitoa fedha na kuachiwa.
Hapo mimi kichwa changu kilianza kuuma nikajiuliza moyoni mwangu hivi kweli kijana ameshikwa na unga halafu anaachiwa kwasababu ametoa hela, sasa sisi tunajenga taifa gani ? Askari hawa kumbe wanachangamkia kupekuwa mizigo na mifuko ya abiria kwa ajili kumbe wanatafuta watu waliobeba unga halafu wapate kupewa hela, baasi kazi imeisha, halafu mwisho wa mwezi anasubiri kupokea mshahara wake, jee sisi kunahaja ya kuwa na watu kama hawa ?
Ikaja zamu ya kutaka kusafiri kuelekea Pemba, ilikuwepo meli ya Kampuni ya Serengeti, ambayo kwa kuwa sikutaka usumbufu siku niliyotaka kusafiri kuja Zanzibar, niliwaeleza vijana wangu wanaoishi hapo, kwamba mimi nakuja hapo nikielekea Pemba, wakaniambia sasa baba tukukatie tiketi kabisa, hiyo ikiwa ni siku ya Jumamosi, nikawajibu ndio, lakini wakanieleza kitambulisho lazima, nikawajibu nyinyi fanyeni booking kabisa mimi nikija nitaonesha kitambulisho ili nikabidhiwe tiketi yangu, vijana walifanya kama nilivyowaagizo na niliposhuka tu kutoka kwenye boti ya Kilimanjaro, nikitokea Dar es Salaam, kijana wangu mmoja alinilaki na tukaenda moja kwa moja hadi kwenye Ofisi ya Kampuni ya Meli ya Serengeti walikonifanyia booking ya safari ya kwenda Pemba, kweli nikaonesha kitambulisho wakathibitisha kwamba ndiye mimi mwenye jina lile, wakanipa tiketi yangu.
Yaliyonikuta wakati naenda kupanda meli ile yalikuwa ni mambo sijapatapo kuyaona hata siku moja kwa muda wote nilioisha visiwani Unguja na Pemba nilikozaliwa.
Nilijikongoja na uchovu wangu ili niwahi meli hiyo, lakini cha kushangaza nilipofika bandarini kwenye lango la kuingilia yapata saa 1:30 nikakuta kuna wasafiri wamezuilia kuingia na geti limefungwa, nikajongelea nione kinachoendelea, nikapiga kelele kumwita mmoja wa walinzi getini pale nikamwambia mimi ni msafiri wa meli ya kwenda Pemba, askari yule hakuonesha hata kuali nilichukuwa nikikisema.
Niliwaona wenzangu wakiwaita wengine na kuwapa tiketi na vitambulisho vyao, nikaone wengine wanafunguliwa mlango wanaingia, sikujua kulichokuwa kikiendele mlangoni pale.
Nikamwita askari kwa mara ya pili, alikuja nikamwambia mimi nasafiri kwenda Pemba na tiketi na kitambulisho changu hiki hapa, akinaniambia hebu kitambulisho chako, kumuonesha akanijibu "kumbe kitambulisho chenyewe ni hicho, hicho kampe Sheha", akaenda kukaa kitako, mimi sikuelewa alikuwa na maana gani, lakini kila muda ulivyokuwa ukienda niona mambo tofauti kabisa wengine kumbe hukunja noti ya sh. 5,000 ndani ya tiketi halafu humkabidhi askari wa mlangoni hapo naye hufungua geti kumuingiza, hicho ndicho nilichokigundua bandarini pale.
Hali hiyo, iliendelea mpaka yapata saa mbili na dakika kumi, ndipo alipokuja askari mwingine na kuwaeleza wenzake, kuwa abiri wote wenye tiketi na vitambulisho vyao, waruhusuni wapite, kwa kuwa pale tulikuwepo wengi nasi tukaanza kusukumana kutaka kuwahi tukihofia kuzuiwa tena, halafu askari yule alitueleza kuwa tukimbie kuwahi chombo kwani sasa hivi wataondoa ngazi.
Hiyo mimi ikanishangaza kuwa kumbe hawa wanatuchelewesha kwenye geti hili ili tuwapatie kitu kidogo ? Halfu wakiona sasa muda umeisha ndiyo waturuhusu.
Nikakimbia kuiwahi meli, nilifika kwenye meli ile, nilipotaka kuigusa ngazi kupanda, nikazuiwa hata baada ya kujieleza na kuonesha tiketi na kitambulisho changu sikuruhusiwa kupanda huku akiwepo askari Polisi aliyekuwa na cheo, ambaye yeye kabisa hakutaka hata kusikia kitu kutoka kwangu.
Jawabu nililolipata baadaye ni kuwa meli imejaa, hairuhusiwa tena kupakia abiria, nikajiuliza hii meli si ndiyo inayokata tiketi kwa kutumia vitambulisho na kwa idadi ya watu maalum, sasa inakuwaje ijaye watu huku baadhi tukiwa hatujapanda, ni kajiuliza tena hizi nafasi zetu zimechukuliwa na nani ?
Kijana mmoja aliyekuwa karibu yangu, akanijibu hapa sasa hivi kunashida ya safari ya kwenda Pemba, vyombo vinaenda karibu kila siku lakini mambo ndiyo hayo, akaongeza tiketi huuzwa mpaka sh. 50,000.
Nikagundua kumbe hapa kuna mchezo mchafu huchezwa hapa bandarini kwa ajili watu wajipatie hela chafu kwa kuwadhulumu na kuwaonea wengine, tena watu wanaofanya mchezo huo, wakiwa ni wale waliopewa dhamana ya kuwatumikia wananchi.
Hii haileti sura nzuri kwa Serikali iliyopo madarakani, wanaididimiza, wananchi waichukie na kuiona hapo kwa ajili ya maslahi yao huku wao wapate kile wanachokitarajia nyoyoni mwao.
Napenda kumweleza Waziri mwenye dhamana kuwa usafiri wa Pemba hauna shida bali yote hayo yanaletwa na watu waliopewa dhamana ambao hawataki kuwatumikia wananchi kutokana na udhaifu wa nafsi zao unaoongozwa na tamaa ya kujipatia fedha kwa njia chafu huku wakikiuka viapo vyao vya kazi.
Watu hawa ni maadui na wahujumu wa ustawi wa hali za wananchi ambazo Serikali yetu tukufu inataka kuwafanyia wananchi wake lakini wao wakizirudisha nyuma juhudi hizo.
Mwisho napenda kumalizia kwa kusema kuwa wakati ni huu, tusipoziba ufa tutajenga ukuta.
Mawasiliano kwa matukio mbalimbali muda wote nitakapokuwa visiwani Unguja na Pemba, wiki mbili kuanzia sasa nikiwaletea matukio ya picha na habari mbalimbali ni kassimmrajab@yahoo.co.uk na kassimrajab@gmail.com na kwa simu tuwasiliane kwa 0773830004, 0767830004 na 0715830004.
Hapa nikiwa na baadhi ya abiria wenzangu kwenye meli ya Mv. Kilimanjaro, tukielekea Zanzibar
|
Madhumuni ya safari yangu hii mbali ya kufika nyumbani nilikozaliwa ni pia kuitangaza Zanzibar kitalii ili Serikali iweze kunyanyuka kiuchumi kwa ajili ya maslahi ya wananchi wake lakini pia pale penye kasoro hatutasita kupaeleza ili Serikali ijue ni wapi penye kasoro na iweze kuchukua hatua haraka kwa madhumuni yale yale ya maendeleo na ustawi wa wanachi wake, kielimu, afya na kiuchumi. Mungu Ibariki Zanzibar, Mungu wabariki Wazanzibari wote. Amin
No comments:
Post a Comment