TANGAZO


Wednesday, September 12, 2012

SMZ, Kampuni ya DB Shapriya & Co. Ltd zatiliana saini ujenzi wa barabara



Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano na Miundombinu wa serikali ya Zanzibar, Dk.Vuai Lila (kushoto) na Meneja Ujenzi wa Kampuni ya DBS Shapriya ya Tanzania, Sathish Babu wakitia saini  mkataba wa ujenzi wa barabara mbili za Unguja katika Hoteli ya Bwawani, mjini Unguja leo. (Picha na Nafisa Madai-Maelezo Zanzibar).
Na Nafisa Madai-Maelezo ZanzĂ­bar
 SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imetiliana saini Ujenzi wa Barabara mbili  za Koani-Jumbi, Jendele, Cheju hadi Kaebona na barabara ya Kizimbani-Kiboje kwa kiwango cha lami ambao utagharimu  shilingi bilioni 14.833.
 Hayo yamefahamika wakati wa utiaji saini wa makubaliano ya ujenzi huo kati ya Wizara ya Mawasiliano na Miundombinu na Kampuni ya M/S db Shapriya + Co.Ltd yaliyofanyika Ukumbi wa Hoteli ya Bwawani mjini Unguja.
 Makubaliano hayo yametiwa saini na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Miundombinu Dk Vuai Lila kwa niaba ya Serikali ambapo kwa upande wa Kampuni hiyo iliwakilishwa na Fundi Mkuu Sathish Babu.
 Akizungumza mara baada ya utiaji saini katika hafla hiyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano, Dk Vuai Lila, alisema fedha hizo zimetolewa na Benki ya Maendeleo ya Kiarabu kwa Maendeleo ya nchi za Afrika (BADEA), ambayo imetoa dola za marekani milioni 8 wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa dola za kimarekani milioni 2.36.
 Katibu Mkuu huyo ameongeza kuwa BADEA itachangia shilingi bilioni 11.454 ikiwa ni sawa na asilimia 72.22, ambapo Serikali itachangia shilingi bilioni 3.379 sawa na asilimia 22.78.

No comments:

Post a Comment