Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma, akilijaribu moja kati ya matrekta 7, yaliyotolewa mkopo kwa wakulima wa Wilaya ya Mufindi mkoani humo na SUMA-JKT. Jumla ya matrekta 27, yanategemewa kukopeshwa kwa wakulima wa wilaya hiyo, ili kuhamasisha sera ya Kilimo Kwanza.
Wakulima saba Mufindi wakopeshwa matrekta 7 na SUMA - JKT
Na Francis Godwin, Mufindi
SERIKALI wilayani Mufindi, mkoani Iringa imeendelea kuwahamasisha wakulima kuongeza uzalishaji zaidi kupitia sera ya Kilimo Kwanza kwa kuwakopesha matrekta 7, yenye thamani ya shilingi milioni 310,962,220.
Akikabidhi matrekta hayo jana, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma, alisema kuwa hatua ya kukabidhi matrekta hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kutimiza dhana ya kilimo bora .
Hivyo alisema kuwa Mkoa wa Iringa ni moja kati ya mikoa ambayo imekuwa ikitegemewa kwa uzalishaji wa mazao ya chakula na hivyo lazima wakulima kuendelea kuhamasishwa zaidi ili kujitokeza kukopa matrekta hayo kwa Taasisi ya Suma JTK ili kuweza kunufaika na zana hizo za kilimo.
Dkt Ishengoma alisema kuwa katika wilaya ya Mufindi jumla ya matrekta 27 yanategemewa kufika katika wilaya hiyo kwa ajili ya wakulima hivyo lazima matrekta hayo kutumika vema katika kilimo na watakaopata matrekta hayo kuweza kuwasaidia wakulima wengine katika kilimo.
Hata hivyo alisema tayari wabunge walimwomba waziri mkuu kuwasaidia ili mikopo hiyo ya Matrekta wakulima warejeshe kwa kipindi cha miaka minne badala ya miaka mitatu kama Suma JKT walivyotaka.
Alisema maombi hayo ya wabunge yalifikishwa kwa waziri mkuu Mizengo Pinda na tayari waziri mkuu alilifikisha ombi hilo la wabunge kwa SUMAJKT na wamekubali iwe hivyo japo bado hawajabadilisha katika fomu zao na kuwaomba kufanya hivyo.
Pia Mkuu huyo wa mkoa aliwataka wakulima hao ambao wamekopeshwa matrekta hayo mbali ya kutumia katika kilimo cha zao la chai pia kuhakikisha wanalima hata mazao ya chakula kwa wingi ili kuendelea kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula katika wilaya ya Mufindi na mkoa wa Iringa kwa ujumla.
Kuhusu maofisa ugani mkuu huyo wa mkoa aliwataka kushirikiana na wakulima hao ili kuweza kuyatumia vema matrekta hayo kwa kulima na kupanda kwa kuzingatia ushauri wa wataalam .
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Mufindi Evalista Kalalu alimweleza mkuu huyo wa mkoa kuwa wilaya ya Mufindi imekuwa ni moja ya wilaya za mkoa wa Iringa ambazo wananchi wake wamekuwa na mwamko mkubwa wa kujitokeza kukopa mkopo wa matrekta hayo na hivyo ana hakika Mufindi itaendelea kusonga mbele katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara kupitia sera ya Kilimo Kwanza.
Alisema kuwa kati ya wakulima ambao wamejitokeza kuchukua mkopo huo wa Matrekta baadhi yao ni wanawake ambao ndio wamekuwa wakinyanyasika zaidi kwa kilimo cha jembe la mikono.
Afisa kilimo wa wilaya ya Mufindi Edna Kaduma alisema kuwa kati ya wakulima 31 waliofanyiwa tathimini ya mali zao kama sehemu ya dhamana ya kukopeshwa Matrekta , wakulima 27 wamekidhi vigezo vya kukopeshwa na kati ya hao saba wameshalipia asilimia 30 ya mkopo wote.
Aliwataja wakulima walioanza kunufaika na mkopo huo kuwa ni Bertha Kilimila, Chedy Ng'umbi, Gabriel Mlyuka, Hawad Ng'umbi, Boniface Ng'umbi, Godfrey Ndyendya na James Msigala .
Alisema wakulima hao wanatarajia kulima hekta 2100 za mazao ya chakula kama mahindi , alizeti, ngano, viazi mviringo na mikunde .
Hata hivyo akizungumza kwa niaba ya wakulima wenzake Bertha Kilimila alipongeza serikali kwa kuwakumbuka wakulima hao na kuomba kuwezeshwa kupewa pembejeo za kilimo kwa wakati ili matumizi ya zana hizo yaendane sambamba na pembejeo
|
No comments:
Post a Comment