Kikundi cha sanaa kitumbuiza wake wa marais wa SADC
Rais Joachim Chisano (kulia) wa Msumbuji akiwa kwenye kikao hicho.
Wake wa Marais wa Kusini mwa Afrika wakiwa kwenye chumba cha majadiliano. Kutoka kushoto ni mke wa Rais wa Mozambique, Dk. Maria da Luiz Dai Guebuza, wa pili kushoto ni mke wa Rais wa Namibia Penehupifo Pohamba, mke wa Rais wa Zambia Dk. Christine Kaseba _Sata (wa tatu kushoto) na kulia ni mke wa Rais wa Tanzania, mama Salma Kikwete, wakisubiri kusaini azimio la mkataba wa kuondoa ukimwi kutoka kwa mama kwenda mtoto, mjini Maputo, Msumbiji leo.
Kamati ya wake wa viongozi wa Wakuu wa Kusini mwa Afrika (SADC), wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya mapumziko mjini Maputo kabla hawajasini azimio la mkataba wa kuondoa maambukizo ya ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
mke wa Rais wa Tanzania, mama Salma Kikwete na mke wa Rais wa Zambia Dk. Christine Kaseba _Sata wakiangalia azimio la mkataba wa kuondoa ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, mkataba uliosainiwa mjini Maputo, Msumbiji leo. (Picha zote na Anna Itenda - MAELEZO)
Wake wa viongozi wakuu wa SADC wapitisha azimio la kutokomeza maambukizi ya ukimwi
Na Anna Nkinda – Maelezo, Maputo
19/8/2012
Wake wa viongozi wa wakuu wa nchi na Serikali za Kusini mwa Afrika (SADC) wamepitisha azimio la kutokomeza maambukizi ya Virusi Vya Ugonjwa wa Ukimwi (VVU) kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na kuhakikisha kuwa wanapunguza vifo vya kina mama na watoto vinavyotokana na tatizo la uzazi.
Azimio hilo lilisainiwa leo, mjini Maputo na wake wa wakuu wa nchi za SADC waliohudhuria mkutano wa siku mbili wa kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ni hitaji la awali kwa maendeleo ya Kikanda ulioenda sambamba na mkutano wa 32 wa SADC.
Akisoma Azimio hilo mbele ya waandishi wa habari, Katibu wa kamati iliyoandaa azimio hilo Daud Nasibu alisema kuwa nia kubwa ya SADC ni kuimarisha biashara na mahusiano ya kikanda ambayo matokeo yake ni kusafiri kwa watu na bidhaa kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine jambo linapelekea kupatikana kwa ajira na kupunguza umaskini lakini kwa upande mwingine kumekuwa na kasi ya maambukizi ya magonjwa ya kuambukiza ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa ukimwi.
Nasibu alisema kuwa wake hao wa wakuu wa nchi watahakikisha kwamba wanafanya kazi na Serikali za nchi zao pamoja na wadau wengine wa maendeleo ili kupunguza maambakizi ya ugonjwa huo na kutokuwa na maambukizi katika nchi zao kwani wanaamini kuwa inawezekana kwa kizazi kijacho katika SADC kuzaliwa kwa watoto wasiokuwa na maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi .
“Tutawahamasisha wanawake ili waweze kuhudhuria katika vituo vya Afya na kupata huduma za mama na mtoto ikiwa ni pamoja na huduma ya kuzuia maambukizi ya Ugonjwa wa Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT) kabla na baada ya kujifungua.
“Pia tutawahamasisha viongozi wa sekta zote wakiwemo wa dini, wa Serikali na wa jadi pamoja na wakunga wa jadi ili tuweze kufanya kazi kwa pamoja katika jitihada zetu za za kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto katika nchi za kanda ya Kusini mwa Afrika”, lilisema Azimio hilo.
Kwa upande wake Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa kitu kikubwa ni kuhakikisha kwamba azimio walilolisaini likishapata baraka za wakuu wa nchi lianze kufanyiwa kazi ili kuweza kutimiza lengo walilojiwekea la kutokomeza janga la Ukimwi ambalo ni tishio kwao, kwa vizazi vyao na vizazi vijavyo.
“Sisi kama wake wa wakuu wa nchi za SADC ambayo ina nchi wanachama 14 sote tukiwa na sauti moja kwani jambo hili linatuhusu wote, hakuna kitu kitakachoshindikana na tutaweza kupambana na kutokomeza ugonjwa huu ambao unatishia maendeleo ya nchi zetu na Dunia kwa ujumla”, alisema Mama Kikwete.
Naye Rais wa Umoja wa wake wa Marais wa Afrika wa Kupambana na Ugonjwa wa Ukimwi (OAFLA) ambaye pia ni Mke wa Rais wa Namibia Penehupifo Pohamba aliwashukuru wajumbe wa mkutano huo na kusema kuwa kazi iliyobaki ni moja ya kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha kuwa malengo waliyojiwekea yanatimia.
Mama Pohamba alisema, “Mimi kama rais wa OAFLA nimefurahi sana kwani hivi sasa nimepata nguvu kwa kuwa tunaazimio ambalo linatubana katika kufanya kazi zetu hivyo basi nitahakikisha kuwa malengo yetu yanafanikiwa, jambo la muhimu ni kwetu sote kufanya kazi kwa pamoja”.
Ugonjwa wa Ukimwi umekuwa ni tishio Ulimwenguni hususani kwa maendeleo ya nchi zinazoendelea kwani takwimu zinaonyesha kuwa kwa mwaka 2011 zaidi ya watu milioni 34 wanamaambukizi ya VVU kati ya hao milioni 30.7 ni watu wazima, milioni 16.7 wanawake na milioni 3.4 watoto wenye umri wa chini ya miaka 15.
No comments:
Post a Comment