Mwanafunzi Herieth Kitunduru, akiwakumbusha masomo wanafunzi wenzake wa darasa wa darasa hilo, shuleni hapo, mjini Iringa leo.
Mkuu wa shule ya Msingi Wilolesi, mjini Iringa, George Kameka akiwa darasani, akiendelea na kazi leo. (Picha zote na Francis Godwin)
Walimu Iringa waomba ulinzi wa polisi,
*wapinga mgomo wadai anayepaswa kugomewa na CWT, si serikali
Na Francis Godwin, Iringa
WAKATI mgomo wa walimu nchini ukiendelea kupoteza mwelekeo baada ya baadhi ya viongozi wa walimu kuonyesha kusaliti mgomo huo , walimu mkoani Iringa wameomba kupewa ulinzi na jeshi la polisi ili kuwawezesha kuendelea na kazi kama kawaida kwa madai kuwa wanatishwa na wenzao.
Hatua ya walimu hao, kuomba ulinzi wa polisi imekuja siku moja baada ya mgomo huo wa walimu kuanza na jeshi la polisi kutoa tamko kuhusu mgomo huo huku likiahidi kuwabana wote watakaotoa vitisho kwa walimu ambao hawaungi mkono mgomo huo.
Mkuu wa shule ya msingi Mtwivila katika Manispaa ya Iringa Christabela Alfani alisema kwa upande wake hadi jana alijikuta akitelekezewa shule hiyo na walimu wenzake ambao walifika na kusaini kitabu cha mahudhuria na kuondoka shuleni hapo.
Hivyo alisema kuwa kutokana na mazingira ya shule hiyo, kuzungushiwa uzio hali ya usalama wake na walimu ambao wapo tayari kuendelea na kazi ni mdogo kutokana na kuhofu kuvamiwa na walimu hao ambao wanaunga mkono mgomo huo.
Kwani alisema baadhi ya walimu katika shule hiyo, wapo tayari kuendelea na kazi ila wanaogopa kuvamiwa na walimu wenzao hao hivyo iwapo jeshi la polisi litawawekea ulinzi katika mazingira ya shule watakuwa tayari kuendelea na kazi.
"Kama jeshi la polisi limetoa tamko juu ya mgomo huo tunashukuru ila tunaomba sasa tamko hilo litekelezwe kwa vitendo kwa kutuwekea ulinzi katika mazingira ya shule ili tuweze kuendelea na kazi kama kawaida"
Hata hivyo mwandishi wa habari hizi aliyetembelea shule hiyo alishuhudia wanafunzi wa darasa la saba wakikumbushana masoni mbali mbali kwa kumteua mwanafunzi mwezao Herieth Kitunguru ili kusimama kama mwalimu wao kwa kuwaelekeza baadhi ya masomo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya msingi ya Wilolesi George Kameka alisema kabla ya kumgomea mwajiri wao, wanataka kufahamu tangu kutoka kwa chama chao hicho cha wafanyakazi tangu walimu nchini kote waanze kukatwa asilimia mbili kwa ajili ya kukichangia, mapato na matumizi yake yakoje.
Hata hivyo alisema inashangaza kuona CWT wanahimiza mgomo wakati wao wanaongoza kwa kuwanyanyasa wanachama wake kwa kuwalipa kiasi cha shilingi 20,000 pekee pale wanapofiwa kama rambi rambi huku mwanachama wa CWT anapostafu kazi CWT hakuna fedha yeyote inayomlipa mwanachama huyo zaidi ya kujinufaisha wao viongozi .
"Hawa viongozi wa CWT wanataka kutufanya sisi kama watoto wa kudanganywa na pipi hivi serikali ambayo imetufikisha hapa tulipo na ipo katika mkakati wa kufanya mazungumzo na walimu ili kutuongeza kile tunachodai .....leo CWT inatuambia tumgomee mwajiri anayetulipa wakati wao wanaendelea kutukandamiza ....tunasema hatupo tayari kutumiwa na CWT ambao si waajiri wetu ...leo wanatuhamasisha tugome ila viongozi wetu wanakwenda kazini ....tunasema sisi si watoto tumekua sasa"
Huku mwalimu mkuu wa shule ya Msingi Kihesa Zabihu Hassan akidai kuwa ameongea na walimu wake na wote wamekubali kuendelea na kazi kama kawaida na hawapo tayari kuingizwa katika mgomo huo.
Kwani alisema kwa sasa watoto wa darasa la saba wapo katika maandalizi ya mtihani wa Taifa hivyo kugoma ni kuwakwamisha watoto hao.
Alisema kuna taarifa zisizo rasmi kwamba CWT iko katika mstari wa mbele kudai maslai ya walimu ili mishahara yao ikipandishwa na wao wapandishe michango yao.
Hata hivyo alitaka Chama cha Walimu Tanzania (CWT) iwaeleze kwanza mapato na matumizi ya michango yao ya kila mwezi kwa chama hicho ndipo waitishe mgomo .
“Tunasikia kuna majengo ya walimu yanajengwa nchi nzima, makatibu wa cwt wananuliwa magari, sasa kuna mpango wa kuanzisha benki, lakini hatupewi taarifa ya mapato na matumizi, na hata magari waliyopewa makatibu hayana msaada kwa walimu ambao ndio wenye mali hata kama wakiumwa,”alisema mwalimu huyo.
Alisema mgomo huo unawapa umaarufu viongozi wa chama hicho na hauna maana yoyote kwa walimu wa kawaida kwasababu taratibu za kuongeza mishahara ya walimu hazina tofauti na zile za watumishi wengine wa umma hivyo kuigomea serikali ili kuongeza misharaha si jibu kwa utendaji wao wa kazi kwani hata wakiongeza bado CWT imeendelea kuwachangisha michango walimu hao ambayo mwisho wa siku inaliwa na wajanja wachache.
Alisema mgomo huo una madhara makubwa yatakayoonekana kwenye mitihani ikiwemo ile ya kitaifa.
Alisema kuna haja kwa serikali kusikiliza kero za walimu hao na kuzifanyia kazi kwa kuzingatia uwezo wake badala ya kila mara kulalamika kwamba haina uwezo jambo ambalo linaonyesha wazi walimu kutumika kisiasa zaidi .
Huku baadhi ya wazazi na wananchi wa kada mbali mbali mjini Iringa wameonyesha kupinga mgomo huo huku baadhi ya wazazi wakidai kuwa watawawajibisha walimu hao iwapo watagoma kwani pamoja na serikali kufuta ada ila walimu hao wamekuwa wakichangisha michango kwa ajili ya masomo ya ziada kiasi cha shilingi 50,000 kwa kila mwezi hivyo iwapo watagoma wawe tayari kurudisha chenji zao .
Mary Haule ambaye alipata kuwa afisa elimu Manispaa ya Iringa alisema kuwa mgomo huo kwa walimu hauna tija na kuwataka kusubiri ahadi ya serikali.
Kaimu Katibu wa CWT Mkoa wa Iringa, Peter Mvilli alisema katika baadhi ya vituo, zipo taarifa za mgomo huo kutokwenda vyema kama walivyotarajia.
Tayari mkuu wa mkoa wa Iringa Dkt Christine Ishengoma jana amekutana na viongozi wa CWT ili kuwasihi kusitisha mgomo huo .
Jeshi la polisi mkoa wa Iringa kupitia kwa kamanda wake wa polisi Michael Kamhanda limewahakikishia ulinzi walimu hao ambao wapo tayari kufanya kazi na kuahidi kuwachukulia hatua kali wale wote watakaowafanyia vurugu walimu wasiounga mkono mgomo huo ama kuwatumia watoto kufanya vurugu.
Kamanda huyo wa polisi alisema kuanzia leo ulinzi utawekwa katika maeneo yote ya shule ili kuwabana wale wote watakaofika kwa lengo la kuvuruga amani shuleni.
No comments:
Post a Comment