Baadhi ya Viongozi wa Dini ya Kiislamu waliokutana na Waislamu, ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam leo, kwa ajili ya kuzindua Kitabu cha Maoni yao kuhusu Katiba Mpya na kujadili masuala mbalimbali yaliyojitokeza nchini hivi karibuni, yakiwemo ya kubadilishwa kwa matokeo ya mtihani wa somo la Maarifa ya Uislamu na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA). (Picha na Dotto Mwaibale)
Na Dotto Mwaibale
JUMUIYA na Taasisi za Kiislamu Tanzania zimecharuka na kutangaza kuwa itaitisha maandano ya Waislamu Ijumaa wiki hii kushinikiza kujiuzulu kwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Dk. Joyce Ndalichako na watendaji wengine wa baraza hilo, kwa madai kuwa wamekuwa wakihujumu matokeo ya mitihani ya wanafunzi wa Kiislamu.
Aidha wamelaani vikali uvunjaji wa heshima kwa kuchoma moto nyumba za ibada wakati wa vurugu zilizotokea visiwani Zanzibar ambapo zimeitaka Serikali kuunda tume huru kutoka pande zote Makanisa, Serikali na Kikundi cha Uamsho ili kuwapata waliohusika na uhalifu huo.
Kauli hiyo imetolewa leo kwenye mkutano wa kuzindua waraka wa maoni ya Waislamu katika mchakato wa Katiba mpya uliowashirikisha Waislamu wa jiji la Dar es Salaam na kufanyika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini.
Katibu Mkuu wa Baraza Kuu wa Jumuiya na Taasis za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ramadhani Sanza, akizungumza katika mkutano huo, alisema kila mwaka wanafunzi wa Kiislamu wamekuwa na matokeo mabaya hali inayotia mashaka kwamba yanachakachuliwa na NECTA.
"Ufaulu mkubwa umekuwa ni kwa wanafunzi wa Kikristo huku wa Kiislamu wakionekana kufanya vibaya, tunajua huo ni mpango maalum unaofanywa na NECTA wa kuwadidimiza kitaalum watoto wa Kiislamu na Uislamu kwa ujumla," alisema Sanza katika mkutano huo uliohudhuriwa na umati mkubwa wa Waislamu.
Kwaupande wake Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Kiislamu Tanzania, Shabani Mapeyo, alisema Waislamu wanalaami vikali kuchoma moto nyumba za ibada wakati wa vurugu zilizotokea visiwani Zanzibar ambapo wameitaka Serikali kuunda tume huru kutoka pande zote, makanisa, Serikali na kikundi cha Uamsho ili kuwapata waliohusika na uhalifu huo.
Mapeyo alisema kila upande uliohusika na kadhia hiyo kwa maana ya Wakristo, Waislamu na Serikali ushushe munkari na badala yake busara itumike ili kumpata muhusika wa uhalifu huo.
Alipendekeza iundwe tume huru yenye wajumbe toka pande zote ili ichungwe kwa undani zaidi kwa kuwa athari zake zinaweza zikawa za muda mrefu ambazo zinapandikiza kutoaminiana baina ya Wazanzibari hasa Wakristo na Waislamu jambo ambalo halikuwepo hapo awali.
Mapeyo alisema, atakayebainika kuhusika na jambo hilo, achukuliwe hatua kali bila ya kujali wadhifa wake iwe katika chama, Dini ama Serikali.
Fitina iliyopandikizwa baina ya Wakristo na Waislamu, Watanzania Bara na Wazanzibar zisipoangaliwa kwa umakini zinaweza kuvuka mipaka na kuenea nchi nzima na kuharibu hali ya nchi, hivyo ndugu zangu Waislamu tuwe makini tusije tukachokozwa na tukaingia katika vurugu hizo kirahisi, alisema Mapeyo.
Aliongeza kuwa Waislamu wafanye maombi maalum Misikitini, Sala za jamaa, faragha kumuomba Mwenyezi Mungu alete faraja na amani katika kadhia hii, ili hali ya amani na usalama irejee visiwani Zanzibar.
Naye Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, akizungumzia suala la sense, alitaka iundwe tume huru ya sense ambayo inawashirikisha Waislamu na Wakristo kabla ya Juni 20 mwaka huu.
Ponda alisema tume iliyopo ina wajumbe wengi wa Kikristo huku Waislamu wakiwa wachache jambo ambalo linawanyima haki Waislamu kushiriki katika zoezi hilo.
Alisema kama hadi kufikia Juni 20, mwaka huu Serikali itakuwa haijaunda tume huru yenye idadi sawa ya makundi hayo, Waislamu hawatashiriki sensa hiyo.
Ponda pia aliitupia dongo Idara ya Takwimu ya Taifa kwamba takwimu inazozitoa hawana imani nazo kwa mfano suala la idadi ya Waislamu na Wakristo hapa nchini.
No comments:
Post a Comment