TANGAZO


Saturday, June 2, 2012

Rais Dk. Shein aipongeza Marekani kwa kuinga mkono Zanzibar


Na Rajab Mkasaba

Zanzibar                                                                                               2.6.2012


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kuimarisha sekta za maendeleo nchini na kupongeza juhudi za Serikali ya Marekani kwa jinsi inavyoiunga mkono Zanzibar katika juhudi hizo.

Dk. Shein aliyasema hayo, leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Seneta Christopher Coons kutoka Jimbo la Delaware Marekani aliefuatana na ujumbe wake ukiwa ni pamoja na Balozi wa Marekani nchini Balozi Alfonso Lenhartd.

Katika maelezo yake Dk. Shein alitoa shukurani kwa Serikali ya Marekani kwa kuendelea kuiunga mkno Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo na na kupongeza juhudi za Serikali ya Marekani jinsi inavyoendelea kuiunga mkono Zanzibar.

Dk. Shein alieleza kuridhishwa kwake na ushirikiano mkubwa ambao ni wa kihistoria uliopo kati ya Zanzibar na Marekani ambao umechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha sekta za maendeleo hapa nchini.

Kwa upande wa sekta ya afya, Dk. Shein aliishukuru Marekani kwa juhudi zake za kuiunga mkono Zanzibar katika kupambana na Malaria, hatua ambayo imeipelekea Zanzibar kuwa mfano katika nchini zinazoendelea katika kupambana na Malaria kwa kupunguza kutoka asilimia zaidi ya 40 hadi kufikia chini ya asilimia moja.

Kutokana na mafanikio hayo, Dk. Shein alimueleza Seneta huyo kuwa Serikiali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya Wizara yake ya Afya itaendeleza mikakati ya kupambana na Malaria pamoja na kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto.

Dk. Shein alieleza kuwa Serikali anayoiongoza itaendelea kupambana na maradhi mengine yanayoambukiza na yasiyoambukiza ukiwemo UKIMWI na kueleza kuwa mafanikio hayo yote yamepatikana kutokana na utendaji mzuri wa kazi na uwajibikaji na mashirikiano ya wataalamu na wafanyakazi pamoja na viongozi wa Wizara hiyo.

Kwa upande wa sekta ya elimu, Dk. Shein alitoa shukurani kwa nchi hiyo kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kusaidia ‘Mradi wa Elimu wa Karne ya 21’ ambao alieleza utasaidia kuwapa watoto elimu bora ya msingi ambayo itaendana na wakati uliopo sanjari na kuwasaidia wale wenye uwezo mdogo kiuchumi ambao hawawezi kumiliki kompyuta.

Kwa upande wa sekta ya miundombinu, Dk. Shein alitoa pongezi kwa Marekani kwa kuiunga mkono sekta hiyo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara pamoja na Mradi Mkubwa wa umeme unaotoka Tanzania Bara hadi Unguja ulio chini ya Shirika la MCC.

Akizungumzia sekta ya kilimo, Dk. Shein alieleza kuwa Marekani imeweza kutoa ushirikiano wake kwa Zanzibar katika kuimarisha sekta hiyo pamoja na usalama wa chakula na lishe bora nchini.

Aidha, Dk. Shein alitoa shukurani kwa Marekani kwa juhudi zake za kusaidia katika suala zima la kupambana na uharamia katika maeneo ya bahari ya Hindi.

Dk. Shein pia, aliueleza ujumbe huo kuwa Zanzibar Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kuimarisha amani na utulivu nchini na kusisitiza kuwa juhudi hizo zitaendelea.

Nae Seneta Coons  wka upande wake alitoa shukurani kwa Rais Dk. Shein kwa mapokezi mazuri aliyoyapata pamoja na mashirikiano yaliopo kati ya Zanzibar na Marekani na kueleza kufurahishwa kwake na hatua zilizofikiwa katika miradi inayodhaminiwa na serikali yake ikiwemo ile ya MCC.

Seneta huyo Jimbo la Delaware liliopo Marekani alimuahidi Dk. Shein kuwa nchi yake itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya afya, kilimo, elimu, umeme, miundombinu na nyenginezo.

Kwa upande wa sekta ya afya, Seneta Coons alimuhakikishia Dk. Shein kuwa Marekani itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika mapambano dhidi ya Malaria licha ya mafanikio makubwa yaliopatikana na kuwa mfano katika nchi zinazoendelea.

Katika mazungumzo hayo, Seneta Coons alitoa rai ya kulipa uhumuhi suala la chanjo kwa maradhi mbali mbali huku akimuhakikishia Dk. Shein kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Zanzibar katika suala zima la utafiti.

Balozi wa Marekani nchini Tanzania Mhe. Alfonso Lenhardt kwa upande wake alipongeza juhudi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa za kuendelea kufanya kazi kwa pamoja hali ambayo imepelekea kuimarisha amani na utulivu.

Lenhardt  alitoa pongezi  kwa Serikali kwa kuweza kukabiliana na kudhibiti matokeo ya uvunjifu wa amani bila ya kuwepo kwa madhara makubwa kwa wananchi na kutoa pongezi maalum kwa Rais Dk. Shein kwa njia bora alizozichukua kutuliza vitendo hivyo vya uvunjifu wa amani vilivyotoa hivi karibuni hapa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment