Bi. Cheka akiwa kazini na kundi la Wanaume TMK Family |
Na Mwandishi Wetu
MSANII anayeibukia kwa kasi katika medani ya muziki wa kizazi kipya nchini Mwahija Cheka ‘Bi Cheka’, amewaomba wakazi wa mji wa Dodoma hususan akina mama kujitokeza kwa wingi Jumamosi hii kushuhudia vitu vyake jukwaani.
Bi Cheka atapanda ulingoni kumsindikiza Aslahi Isihaka ‘Dogo Aslay’ katika onyesho la aina yake la ‘Dogo Aslay Live’ litakalofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, Jumamosi ya Juni 9, mwaka huu.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jijini Dar es Salaam jana Bi Cheka aanyetoka kituo cha Mkubwa na Wanawe cha Temeke, alisema kuwa anataka kuwaonyesha akina mama wenzake kile kilichomfanya aamue kushika maiki licha ya umri kwenda.
“Ninawaomba akina mama wa Mkoa wa Dodoma wajitokeze kwa wingi Jumamosi hii kunishuhudia ninavyochana mistari, ninataka kuwathibitishia kuwa akina mama tukiamua tunaweza, nimefurahi kupata nafasi hii sibahatishi kama wanavyodhani,” alisema Bi Cheka.Bi. Cheka akiwa katika pozi la picha |
Msanii huyo ataungana na wakali kibao kumsindikiza Dogo Aslay ambaye naye anatokea kituo cha Mkubwa na Wanawe na ambaye amekuwa gumzo tangu alipouachia wimbo wake ‘Naenda Kusema’.
Wengine watakaotumbuiza siku hiyo ni pamoja na Mzee wa Kibodaboda, Ferooz Mrisho ‘Ferooz, ambaye wimbo wake mpya ‘Ndege Mtini’ ulio kwenye mahadhi ya Mchiriku umekubalika.
Msanii huyo aliyekaa kimya baada kutamba na wimbo wake ‘Starehe’ kwa sasa amerejea kutingisha na ‘Ndege Mtini’, ulio kwenye albamu yake mpya ya ‘Rizevu’ aliomnshiriki Shoz Dia wa Nyumba ya Vipaji Tanzania (THT).
Naye Mratibu wa onyesho hilo Jackline Masano, alisema Bi Cheka ataunga na Ferooz, wasanii kutoka kituo cha Mkubwa na Wanawe kundi zima la TMK Wanaume Family Mfalme wa Rhymes nchini Selemani Msindi ‘Afande Sele’ na 20 Pacent kutoka Morogoro.
Kiingilio kitakuwa sh 3,000 kwa kila mmoja atakayeingia kwenye uwanja wa Jamhuri na onyesho hilo litaanza saa 6:00 mchana hadi saa 12:00 jioni, lakini saa 2:00 usiku hadi 6:00 usiku, wasanii hao wote watahamishia burudani kwenye ukumbi wa Royal Village mjini Dodoma ambapo kiingilio chake kitatangzwa Jumatano.
No comments:
Post a Comment