TANGAZO


Wednesday, June 13, 2012

Bajet ya Zanzibar, ushuru, kodi, huduma mbalimbali kupanda



Waziri wa Fedha na Uchumi Zanzibar, Omar Mzee
Na Juma Mohammed,
MAELEZO  Zanzibar
Juni 13, 2012.

BAJETI ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, imesomwa leo, ikipendekeza
maeneo manane ya kuongeza kodi ikiwemo mafuta ya petrol na dezeli, ada ya bandari, ushuru wa stempu, leseni ya njia, VAT kwa hoteli, mikahawa na watembeza watalii na maeneo mengine.
Katika hotuba yake ya bajeti kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi
leo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha Uchumi na Mipango ya
Maendeleo, Omar Yussuf Mzee alisema  ada ya bandari imependekezwa
kuongezwa kutoka shilingi 1,000 ya sasa hadi shilingi 2,000 kwa abiria
wanaosafiri baina ya Zanzibar na Tanzania bara.
Waziri huyo alisema pia kwa upande wa Pemba, Serikali inapendekeza
ongezeko la ada kufikia shilingi 1,000 kwa abiria wanaosafiri baina ya
Visiwa vya  Unguja na Pemba .
Waziri Mzee alisema sheria ya ushuru wa stempu namba 6 ya mwaka 1996
sheria ya kodi za hoteli namba 1 ya mwaka 1995, sheria ya ada za
bandari namba 2 ya mwaka 1999, sheria ya ushuru wa petrol namba 7 ya
mwaka 2001.
Waziri huyo alisema Sheria nyengine ni pamoja na ile ya usimamizi na
utaratibu wa kodi namba 7 ya mwaka 2009, sheria ya kodi ya ongezeko la
thamani namba 4 ya mwaka 1998, sheria ya bodi ya mapato Zanzibar namba
7 ya mwaka 1996 na sheria ya mafunzo ya amali namba 8 ya mwaka 2006.
Aidha, SMZ inapendekeza pia kuongeza ushuru wa ongezeko la mafuta kwa
shilingi 50 kwa lita inayoingia nchini kwa mafuta ya petrol na diseli
tu ambapo hatua hiyo inatarajiwa kuiingizia SMZ shilingi bilioni 3.3.
Akizungumzia ongezeko la ushuru wa stempu, waziri huyo alisema
serikali inapendekeza kuongeza kutoka asilimia moja na nusu ya sasa
hadi asilimia tatu ambapo wanatarajia kuongeza mapato kwa Serikali ya
shilingi bilioni 2.10.
Eneo jengine ambalo linafanyiwa marekebisho ni sheria ya usafiri
barabarani, inapendekeza kurekebisha kiwango cha leseni za njia ili
kiendane na uzito wa gari au ukubwa wa injini yake.
Alisema kiwango cha sasa cha ada ya leseni ya njia shilingi 24,000 kwa
gari kwa mwaka, hakizingatii matumizi ya njia tofauti za gari.
Waziri huyo alisema kwamba Seriakli inapendekeza kutozwa shilingi
15,000 kwa kila gari kwa mwaka na shilingi 3,000 kwa chombo cha moto
cha magurudumu mawili au matatu hiyo ni kutokana na idadi ya magari
nchini inaongezeka kila mwaka na hivyo kuathiri mazingira kutokana na
moshi unaotokana na magari hayo.
Aidha, katika marekebisho mengine, ni yale ya viwango vya ada za huduma
mbali mbali zinazotolewa na Serikali na taasisi zake baada ya
kubainika ada hizo zimepitwa na wakati.
Waziri huyo alisema katika mwaka wa fedha, Serikali inakusudia kufanya
marekebisho kiwango cha kodi huduma za mahoteli, mikahawa, na
kutembeza wageni.
Alisema inapendekeza kuongeza kiwango cha kodi kwa mahoteli, mikahawa
na watembeza wageni wasiosajiliwa kwenye VAT kutoka asilimia 15 ya
sasa hadi asilimia 18.
Mzee alisema uchumi wa Zanzibar unatarajiw akukuwa kwa asilimia 7.5
kutoka ukuaji wa asilimia 6.8 mwaka 2011.
Waziri alisema mfumko wa bei unatarajiwa kushuka hadi kufikia asilimia
8.7 kwa mwaka wa 2012 ambapo mwaka jana mfumko wa bei ulikuwa asilimia
14.7.
Alisema kwamba uchumi wa Zanzibar kwa mwaka huu unatarajiwa kuimarika
zaidi kutokana na mipango mbali mbali ya Serikali katika ukusanyaji wa
mapato kutoka vyanzo mbalimbali.
Katika bajeti hiyo SMZ, imeweka maeneo ya vipaumbele kama afya,
kuimarisha ajira kwa vijana, kuimarisha ustawi wa wazee, kuimarisha
elimu, kuimarisha uchumi, pamoja na kuhifadhi mazingira na kukabiliana
na tabia nchi.
SMZ katika bajeti yake mwaka huu imepanga kutumia shilingi bilioni
mia tatu na saba na mia saba tisini na saba milioni (307, 797m) kwa
kazi za kawaida na shilingi bilioni mia tatu na arubaini na moja na
mia moja na arubaini na saba milioni (341,147 m).
Aidha, Serikali inatarajia kukusanya shilingi bilioni mia sita na
arubaini na nane na mia tisa na arubaini na nne milioni (648,944m).

No comments:

Post a Comment