Makamu wa Rais Dk. Mohamed Gharib Bilal |
Na Aron Msigwa – MAELEZO, Tabora.
Makamu wa Rais Dkt. Maohammed Gharib Bilal amewataka viongozi kote nchini wawe mfano wa kuigwa kwa kutoa ushirikiano na kukubali kuhesabiwa wakati wa zoezi la sensa ya watu na makazi itakayofanyika nchi nzima mwezi Agosi mwaka huu.
Akizungumza na viongozi wa mkoa wa Tabora leo mara baada ya kuwasili kwa ziara ya siku mbili Dkt. Bilal amesema sensa ya watu na makazi ni muhimu kwa taifa kwani itatoa mwelekeo wa nini cha kufanya kwa maendeleo ya taifa.
Amesema viongozi bila kujali nafasi walizonazo wanalojukumu kubwa la kuhahkikisha kuwa zoezi la sensa ya watu na makazi linafanyika kwa ufanisi mkubwa kutokana na mikakakati na maandalizi mazuri yaliyofanywa na ofisi ya taifa ya Takwimu.
Amefafanua kuwa kila mtanzania ni mshiriki wa zoezi hilo huku akitoa wito kwa wananchi wote kujitokeza na kutoa ushirikiano siku ya sensa ili waweze kuhesabiwa katika maeneo yao.
“Sisi sote ni washiriki wa zoezi hili , sote lazima tukubali kuhesabiwa hivyo jukumu letu ni kuhamasishaba ili tuweze kuleta mabadiliko” amesema .
Ameongeza kuwa upatikanaji wa takwimu sahihi za idadi ya watu na makazi pamoja na hali ya kiuchumi utatoa dira ya upangaji wa mipango mizuri ya maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Tabora Bi. Fatma Mwasa akitoa salaam za mkoa huo na taarifa ya utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo amesema mkoa wake umepiga hatua kimaendeleo licha ya changamoto mbalimbali zilizopo.
Amezitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na tatizo la ajira, bei za bidhaa kupanda mara kwa mara kutokana na ukosefu wa miundombinu inayoufungua mkoa huo na mikoa mingine pamoja na tatizo la upatikanaji wa maji ambalo ameiomba serikali kutekeleza mradi wa maji kutoka ziwa Victoria.
Aidha ameipongeza serikali kwa kuuchagua mkoa wa Tabora kuwa mwenyeji wa ufungaji wa awamu ya kwanza kitaifa ya kutenga maeneo ya maandalizi ya sensa ya watu na makazi itakayofanyika nchi nzima mwezi Agosti mwaka huu.
Ikumbukwe kuwa zoezi lz sensa ya watu na makazi la mwaka huu litakalodumu kwa siku saba linafanyika ikiwa ni miaka 10 baada ya sensa ya mwisho iliyofanyika mwaka 2002 wakati sensa nyingine zilifanyika nchini miaka ya 1967, 1978 na mwaka 1988.
No comments:
Post a Comment