| Dk. Mahanga, akitoka Mahakama Kuu leo |
Na Mwandishi wetu, Dar.
MBUNGE wa Jimbo la Segerea Dk Makongoro Mahanga, amensurika kuvuliwa ubunge huo, baada ya Mahakama Kuu kumtangaza mshindi dhidi ya kesi ya kupingwa kwa matokeo ya jimbo hilo, iliyofunguliwa dhidi yake.
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, jana ilimtangaza Mahanga kuibuka na ushindi huo katika hukumu ya kesi hiyo iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa Jimbo hilo kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Fredy Mpendazoe.
Katika kesi ya msingi namba 98/2010, Mahakama kupitia Jaji Profesa Ibrahimu Juma, ilitupilia mbali madai 11 yaliyowasilishwa mahakamani hapo na Mpendazoe, yaliyokusudia kuitaka mahakama kutengua ubunge huo wa Mahanga ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kazi na Ajira.
Mbali na Dk Mahanga ambaye ni mdaiwa wa pili katika kesi hiyo, mdaiwa wa kwanza ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na wa tatu ni Msimamizi wa Uchaguzi (RO), katika jimbo hilo.
Wakati wa ushahidi katika kesi hiyo, upande wa madai uliwaita mahakamani mashahidi 13 akiwemo mlalamikaji mwenyewe Mpendazoe na wadaiwa wote watatu kwa pamoja waliwaita jumla ya mashahidi 16.
Akisoma hukumu hiyo iliyosomwa kwa saa 3 mfururizo, Jaji Juma alisema kuwa katika hoja ya dai la tatu, mlalamikaji ambaye ni Mpendazoe alishindwa kuithibishia mahakama kweli palikuwa na mapungufu ya fomu kujumlishia matokeo kwa vituo 249 katika jimbo hilo.
Katika dai hilo, Mpendazoe alidai kwamba hapakuwapo na fomu hiyo ya kuandikia matokeo ya kura, hivyo kufanya mawakala wake kujaza matokeo katika karatasi ambazo hazikuwa rasmi.
"Mpendazoe alidai kwamba hakukuwa na fomu ya kujazia matokeo, kiasi cha kuwafanya mawakala wake waliokuwa katika vituo hivyo kutumia karatasi za kawaida kujaza matokeo hayo"alisema Jaji Juma.
Kufuati hilo, upande wa walalamikiwa uliokuwa ukiongozwa na mawakili Jerome Msemwa, Aliko Mwamanenge, David Kakwaya na Seth Mkemwa ulileta mashahidi wake wakiwamo waliokuwa wasimamizi wa uchaguzi, ambao waliithibitishia mahakama kuwa vifaa vyote vilikuwa vimetimia katika vituo kabla ya kura kupigwa.
Alisema mashahidi hao walisema kwamba vifaa hivyo vilisambazwa kwa wakati kama ambavyo sheria inataka, na hakukuwa na fomu ya matokeo ya wakala yoyote iliyojazwa kwa karatasi hisiyokuwa rasmi.
Mahakama pia ilisema kuwa kinyume na Mpendazoe alivyodai awali kuwa angekuwa na vielelezo vya kuthibisha hilo, alishindwa kuwasilisha vielelezo hivyo hata alivyoombwa kufanya hivyo, hivyo mahakama iliitupilia mbali hoja hiyo kwakuwa haikuthibishwa.
Hoja ya tano iliyodai kuwa kulikuwa na msimamizi wa uchaguzi msahidizi aliyekutwa na karatasi ya matokeo iliyokuwa batili, mahakama iliitupa hoja hiyo kwakuwa hakukuwa na uthibitisho wa kutosha kama kweli msimamizi huyo alikamtwa na kufikishwa polisi.
Jaji Juma alisema kuwa kinyume na Mpendazoe alivyoieleza mahakama kuwa alikuwa na mkanda wa video ukimuonesha msimamizi huyo aliyetajwa kwa jina la Imelda Kafanabo katika tukio hilo, hakuleta kama kielelezo mahakamani hapo hivyo mahakama imeshindwa kujiridhisha.
Vivyo hivyo katika hoja ya sita ya mtu mmoja kukukamatwa akidaiwa kuwa na mihuri eneo la kituo cha kujumushia matokeo, mahakama iliitupa hoja hiyo kwakuwa hakukuwa na ushahidi wa kukamatwa mtu huyo na kuuchukulia huo kama ulikuwa uvumi.
Mbali na hoja hiyo kutupwa, mahakama hiyo pia ilituopa hoja ya saba na nane ambapo Mpendazoe alidai kuwa yeye pamoja na wagombea wenzie wa upinzani walimgomea msimamizi wa uchaguzi kutangaza matokeo kwakuwa hayakuwa yamekamilika.
Katika hoja hiyo, Jaji Juma alisema kwamba Mpendazoe alikuwa akidai kwamba angewapeleka mahakamani hapo wagombea hao wenzie kama mashahidi, lakini hakuweza kuwaleta na wala hakuthibitisha kama kweli kulikuwa na kuchelewa kuletwa kwa baadhi ya matokeo ya baadhi ya vituo.
Jaji Juma pia alijibu hoja ya 10 na 11 kwa pamoja, ambayo ilimtaka kueleza kama ni kweli mpendazoe alishinda kwa madai kuwa majumuisho kutoka kwa mawakala wake yalionesha kuwa alikuwa mshindi.
Katika majibu yake Jaji Juma alisema kuwa Mpendazoe alitakiwa kuithibishia mahakama kwa kuleta nakala za matokeo hizo alizopewa na mawakala, lakini alishindwa kufanya hivyo na kwamba mahakama haiwezi kukubaliana na hoja hiyo kwa kusikiliza madai yake pekee bila uthibitisho.
Mbali na hoja hizo zilizokuwa katika hati ya madai, Mahakama hiyo pia ilitupilia mbali hoja za ziada zilizowasilishwa mahakamani hapo na Wakili anayemtetea Mpendazoe Peter Kibatala, alizotaka mahakama kuzizingatia.
Katika hoja hizo za Kibatala, alidai kuwa Dk Mahanga alikamatwa na masanduku ya kura ambapo baada ya kukamatwa alipelekwa Polisi.
Kibatala alikuwa na mashahidi wawili kuiunga mkono hoja hiyo, ambapo mahakama haikuridhika na ushahidi wao wote, huku ikiichukulia hoja hiyo kama uvumi.
Kufuatia hoja zote hizo, mahakama hiyo ilifikia maamuzi ya kuzitupilia mbali hoja za Mpendazoe, na kumtangaza Mahanga kuwa mbunge halali aliyechaguliwa kwa kufuata sheria na taratibu zote.
Mpendazoe aipinga Hukumu.
Baada ya mahakama kuwa imemalizwa kusomwa na Jaji kuondoka Mahakamani hapo, Mpendazoe alidai kuwa hakubaliani na hukumu hiyo.
Alisema kuwa amedhamilia kushauriana na chama chake, pamoja na wakili wake hili kujua kama atakata rufaa ama la, na kwamba baada ya majadiliano hayo atatafuta ufumbuzi.
"Mimi kwakweli sijakubaliana na hukumu hii, na nina nia ya kukutana na chama changu kutafuta ushauri wa cha kufanya, na nitakuwa na maamuzi baada ya kushauriana nao pamoja na mwanasheria wangu"alisema Mpendazoe
Alisema sababu kubwa inayomfanya kutokubaliana na hukumu hiyo, ni kutokubali uchambuliwaji wa baadhi ya hoja alizoziwasilisha kama madai katika kesi hiyo.
Aliongeza kuwa kuna baadhi ya hoja hazikufanyiwa kazi na mahakama hiyo, hivyo hajakubaliana na hukumu hiyo.
Nje ya Mahakama.
Eneo la mahakama hiyo lilikuwa limezingirwa na watu wengi waliokuwa wameshika bendera za CCM huku wengine wakiwa wameshika bendela za Chadema na kuvalia mavazi ya chama hicho.
Licha ya kuwa ulinzi mkali ulikuwa umeimarishwa, haikuwazuia watu hao kuimba huku mvutano ukionekana baina yao, baadhi yao walikuwa wakishangilia huku wengine wakizomea.
Dk Mahanga alipotoka nje ya mahakama, alikutana na kundi hilo, ambapo awali walionekana wafuasi walioshika bendera za CCM wakimkumbatia na kumshangilia, huku wale walio wa chadema wakizomea.
Baadaye kundi la CCM lilionekana kuzidiwa na kundi la wafuasi wa Chadema waliokuwa wakimzoea Dk Mahanga, huku zikisikika sauti za"CCM...Mafisadi".
Hatua hiyo ilimfanya Dk Mahanga kuingia katika gari lake kwa nia ya kuondoka, lakini kundi hilo liliendelea kumzonga huku likikimbiza gari na kupiga kelele za 'mwizi huyo'.
Watu hao waliendelea kutawanyika katika mahakama hiyo huku kila kundi likishangilia kwa upande wake, na kujitapa kuwa lilikuwa limeibuka mshindi.

No comments:
Post a Comment