TANGAZO


Wednesday, May 30, 2012

 20 Pacent naye kumpiga tafu Dogo Aslay



Na Mwandishi Wetu,
Mei 30, 2012

MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini Abbas Hamisi ‘20%’ naye ataungana na wasanii wengine nyota nchini, kumsindikiza Asilahi Isihaka ‘Dogo Aslay’ katika maonesho yajulikanayo kama Dogo Aslay Live, yatakayofanyika katika miji ya Dodoma na Arusha mwezi ujao.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu jana, Mratibu wa onesho la Dodoma, Jackline Masano wa Kampuni ya Ruhazi Promotion ya Dar es Salaam, alisema kuwa 20% amekubali kuungana na Selemani Msindi ‘Afande Sele’ wa Morogoro, TMK Wanaume Family na Kituo cha kuibua vipaji cha Mkubwa na Wanawe cha jijini Dar es Salaam, kumsindikiza Dogo Aslay.
Jackline, alisema kuwa maonesho hayo, yatafanyika Juni 9 mwaka huu kwenye uwanja wa Jamhuri na kwenye ukumbi wa Royal Village mjini Dodoma na kwamba maandalizi kwa ujumla yanaendelea vizuri.
“Tunapenda kuwaambia wakazi wa Dodoma kuwa mambo yamezidi kunoga, hivyo wapenzi wa burudani wasikose kuhudhuria maonesho ya Dogo Aslay Live, kwani Mfalme wa Rhymes Tanzania Afande Sele, TMK Family, Mkubwa na Wanawe na na sasa 20% watakuwepo kutumbuiza siku hiyo,” alisema Jackline.
Aidha, Jackline alisema kuwa wanaendelea kufanya mazungumzo na wasanii zaidi na kwamba burudani yote hiyo, wataipata kwa kiingilio cha sh. 3,000 tu kwa kila mtu na akawataka wapenzi na mashabiki wa muziki wa mji wa Dodoma na maeneo jirani kuanza kujiandaa kwa onesho hilo.
Wakati huo huo, Kampuni ya Ruhazi Promotion, inayoandaa onesho hilo imeweka wazi kuwa baada ya Dogo Aslay Live kufanyika mjini Dodoma , burudani hiyo itahamia kwenye jiji  la burudani la Arusha ambako nako onesho kama hilo litarindima, Juni 16, 2012 kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

No comments:

Post a Comment